Friday, March 22, 2013

Kitunguu swaumu; mambo mengi usiyoyajua

By Shita Samwel

Wengi wetu tunakifahamu kitunguu swaumu kwa kuwa wamekionau kukitumia kwa shughuli mbalimbali katika maisha yao.

Hii ni jamii kubwa ya vitunguu ambayo kwa kitaalamu huitwa Allium sativum.
Jamii hii ilianza kutumika katika mabara mbalimbali duniani hususani Asia, Afrika na Ulaya, takribani miaka 6,000 iliyopita.

Matumizi makuu nyakati hizo yalikuwa viungo katika mboga na tiba.

Ushahidi wa kitafiti
Katika utafiti uliofanyika Jamhuri ya Czech ilionekana kuwa matumizi ya kitunguu swaumu yalisaidia katika kupunguza kusanyiko la lehemu (cholesterol) pamoja na mafuta yasiyofaa mwilini katika mishipa ya damu.

Aidha, mwaka 2007, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) liliripoti matumizi ya kitunguu swaumu katika kusaidia kumkinga mtumiaji dhidi ya aina fulani ya mafua iliyosababishwa na virusi.

Mwaka 2010, ulifanyika utafiti mwingine ambao ulijumuisha wagonjwa 50 wenye shinikizo la damu sugu ambalo lilikuwa ni vigumu kudhibitiwa hata kwa matibabu yaliyozoeleka ya dawa na njia nyingine.

Kama njia ya kuchunguza ufanisi wa kitunguu swaumu katika kutibu shinikizo la damu, baadhi ya wagonjwa hao walipewa kitunguu swaumu wakati wengine walipewa dawa isiyohusika na matibabu ya shinikizo la damu (au placebo).

Ilionekana kuwa wale waliopewa kitunguu swaumu kama dawa ya shinikizo la damu walionyesha maendeleo mazuri kwa kitunguu swaumu kushusha kwa mafanikio kiwango cha shinikizo la damu, hususani systolic pressure, tofauti na wale waliopewa placebo.

-->