‘Asilimia 95 tunaumwa magonjwa zaidi ya matano’

Muktasari:

  • Hii ni ripoti mpya iliyotolewa na jarida la kimataifa la sayansi na tiba, Lancet. Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 95 ya watu duniani wanaumwa.

Wanaamka asubuhi, wanakwenda kazini, wengine kwenye biashara zao na wengine shuleni. Wanakula, wanakunywa, wanaabudu na wanacheza lakini wote wana maradhi. Tena hawaumwi ugonjwa mmoja tu bali zaidi ya matano.

Hii ni ripoti mpya iliyotolewa na jarida la kimataifa la sayansi na tiba, Lancet. Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 95 ya watu duniani wanaumwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo magonjwa matano ambayo watu wengi wanaugua duniani ni maumivu ya mgongo, msongo wa mawazo, ukosefu wa madini ya chuma na maumivu ya shingo. Magonjwa mengine ni kama usikivu hafifu na ulegevu wa viungo yanatokana na uzee.

Kwa takwimu hizo, kama asilimia 95 ya watu wote ni wagonjwa, ni sawa na kusema; kati ya watu 10 wanaoonekana barabarani, ni mmoja tu ndiye mwenye afya njema kwa asilimia 100. Hiyo ni sawa na asilimia 4.3 tu, ya watu wote duniani.

Kwa mujibu wa utafiti wa magonjwa uliofanywa mwaka jana kidunia na kuchapishwa na Lancet, watu 2.3 bilioni waliohusishwa, ambao ni sawa na asilimia 95, wanaumwa magonjwa zaidi ya matano. Utafiti unaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 23 iliyopita magonjwa yaliyoongoza kwa kuathiri watu wengi ni maumivu ya mgongo, msongo wa mawazo, ukosefu wa madini ya chuma, maumivu ya shingo. Magonjwa mengine ni yanayotokana na uzee, kama usikivu hafifu na ulegevu wa viungo vya mwili.

Kwa mwaka 2013, maumivu ya mgongo, shingo, akili, msongo wa mawazo na magonjwa yatokanayo na dawa za kulevya au pombe yalikuwa ni nusu ya magonjwa yote duniani.

Kwa mfano, taarifa hiyo inaeleza, kisukari kiliongezeka kwa asilimia 43 katika miaka 23 iliyopita. Hata hivyo, kiwango cha vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kimeongezeka kwa asilimia tisa tu.

Katika utafiti huo, madaktari walifanya utafiti kwa kutumia sampuli za watu 35,620 kutoka katika nchi 188 mwaka 1990 hadi 2014. Lengo lilikuwa kuangalia ukubwa wa ulemavu, maradhi na mfumo wa afya. Kadhalika walichukua sampuli za magonjwa sugu na yasiyoambukiza kwa kuangalia yanaathiri watu kwa kiasi gani.

Mtafiti mkuu katika jopo hilo kutoka Chuo Kikuu cha Washington D.C, Dk Theo Vos anasema waliangalia madhara zaidi ya 2,337 ambayo yanaweza kusababisha watu kuugua magonjwa matano.

Magonjwa 10 yanayoathiri wengi

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo na msongo wa mawazo yalikuwa ni magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha ulemavu duniani kote.

“Magonjwa hayo yalisababisha madhara kuliko hata kisukari, pumu, na magonjwa ya mfumo wa upumuaji,” anasema Dk Vos.

Duniani, idadi ya watu wenye magonjwa zaidi ya moja imeonekana kuongezeka kadri umri unavyoongezeka.

Idadi ya watu wenye maradhi zaidi ya 10 iliongezeka kwa asilimia 52 katika kipindi cha mwaka 1990 hadi 2014.

Sababu nane zilielezwa kuwa ndiyo chanzo cha watu kuwa na magonjwa sugu yanayoathiri asilimia 10 ya watu duniani.

Sababu hizo ni kichwa kisababishwacho na wingi wa kazi au mshtuko. Upungufu wa damu, upungufu wa madini chuma, malengelenge sehemu za siri, maumivu ya kichwa yasiyokoma, minyoo wakubwa, meno, ukosefu wa sukari na uziwi utokanao na uzee.

Watafiti hao walisema yapo magonjwa yanayosababishwa na maradhi ya kisukari, kwa mfano kushindwa kufanya kazi kwa mishipa ya fahamu, matumizi makubwa ya dawa za maumivu na maumivu au kufa ganzi kwa viungio vya mwili, kiuno na magoti.

Profesa Vos anasema chanzo kikubwa cha magonjwa hayo ni watu kupuuza baadhi ya dalili kwa mfano, magonjwa ya akili ambayo hayapewi kipaumbele kwenye nchi zinazoendelea.

“Kufanyia kazi masuala haya, kunahitaji mabadiliko makubwa ya kiafya duniani kote. Suluhisho siyo kuwaongezea watu muda wa kuishi hadi uzeeni, kwa sababu wengine wanaendelea kuishi na magonjwa yanayotesa, wanatakiwa kuwa na afya,” anasema.

Akizungumzia ripoti hiyo, Daktari Bingwa wa Afya ya Jamii na Familia, Ali Nzige wa Hospitali ya Al Hilal anasema utafiti huo una ukweli hasa katika nchi zinazoendelea.

Anasema kuna sababu nyingi za watu kuumwa ikiwamo mazingira machafu, maji yasiyo safi na salama, mlo duni, vyakula vya kusindikwa na foleni barabarani.

Dk Nzige anasema kuwa asilimia 20 ya wagonjwa wa kisukari nchini ni watoto.

“Wamarekani wanaougua kisukari wanafika milioni 24, lakini wanaojijua ni milioni 18. Milioni sita hawajijui. Hii inadhihirisha kuwa watu wengi hawajijui kama wanaumwa,” anasema

Anasema upo umuhimu wa kuwa na takwimu za wagonjwa.

Anataja sababu nyingine ya watu kuumwa ni kuwa na uzito kupita kiasi. Anaeleza, kwa mfano, mwanaume mwenye urefu wa futi tano na inchi 10 anatakiwa awe na kilo 68.

Kwa mwanamke mwenye urefu wa sentimita 164, kabla hajashika mimba ya kwanza anatakiwa awe na kilo 58. Baada ya hapo, lazima uzito wake utaongezeka.

“Mtu mnene kupita kiasi lazima apate maumivu ya mgongo na miguu. Tunatakiwa tuwe na afya njema kwa namna nyingi; kwa nje na ndani,” anasema.

Dk Nzige anatolea mfano ugonjwa wa kisukari nchini katika kila watu wazima watatu, mmoja ana shinikizo la damu.

Anasema maradhi mengi yanatokana na kula vibaya, kutofanya maoezi na msongo wa mawazo unaotokana na ugumu wa maisha, foleni au machafuko.

“Zipo sababu nyingi, ukikaa siku nzima bila kufanya kazi hauna tofauti na mtu ambaye amevuta sigara 14. Wazazi wanapaswa kuwa waangalifu, baadaye hakutakuwa na mtoto mwenye meno imara, kwa sababu ya kuzagaa kwa pipi hapa nchini,” anasisitiza.