Chuma hunoa chuma, jifunze kwa magwiji kuitofautisha biashara yako

Kila kitu ni tofauti na kingine. Hata binadamu hutofautiana kwa mwonekano na sayansi inasema chembe za ndani kabisa za binadamu humtofautisha mtu mmoja na mwingine.

Utofauti huu huwa unaendelea kujionyesha kwenye vipaji vya kila mtu. Ndiyo maana utakuta watu wawili wanaimba aina fulani ya muziki, lakini kila mtu anakuwa na ladha yake ambayo inamtofautisha na mwingine. Au unaweza kukuta watu wawili wanachora ila kila mmoja wao ana upekee wake ambao unamtofautisha.

Pia kwenye biashara utofauti ni jambo muhimu sana na unapaswa kutengenezwa na mmiliki husika au watu unaofanya nao kazi. Watu wengi huwa hawajui jinsi ya kuzitofautisha biashara zao, hivyo kujikuta wakiziendesha kwa mazoea.

Leo naomba nikuongezee uelewa kidogo utakaokusaidia kuitofautisha biashara yako. Zipo mbinu kadhaa za kufanikisha hilo. Nitazieleza.

Mosi ni kuwa na malengo makubwa na biashara yako. Unatakiwa uione biashara yako ikikua kadri muda unavyoenda. Haijalishi umeanza kidogo kiasi gani lakini baada ya miaka kadhaa mradi wako unatakiwa uwe tofauti. Mtaji uongezeke na usambaji wa bidhaa au huduma zako nao uwe umepanuka.

Unapaswa kuwa na ndoto kubwa ili biashara yako isibaki jinsi ilivyo miaka mitano ijayo kwa mfano. Hii haiji hivihivi tu, unatakiwa kuona mbali. Kama sasa hivi biashara yako ina wateja 100, waongezeke mpaka maelefu baada ya miezi kadhaa na uweke juhudi ya kuwafikia wateja wapya.

Kama biashara yako inategemea uwepo wako muda wote, anza kuiona ikiajiri wafanyakazi ili upate muda wa kushughulika na mambo mengine ya kuikuza.

Tengeneza malengo makubwa na muda mrefu na anza kuyafanyia kazi leo, taratibu na usikate tamaa. Kumbuka, hata anayetaka kuhamisha mlima, anaanza na kutoa jiwe moja.

Utunzaji wa hesabu za fedha ni eneo ambalo watu wengi hawalipi kipaumbele. Kati ya masomo yanayowashinda wengi katika biashara ni utunzaji wa hesabu. Na tatizo hili linawakumba zaidi wenye biashara ndogo ambao hawawezi kuwaajiri wataalamu hivyo kuwanyima uwezo wa kukuza biashara zao.

Kila mmiliki wa biashara ni lazima afahamu kiasi cha mapato na matumizi ya biashara yake kwa ufasaha. Ni muhimu wakati wote awe anajua kiasi cha fedha kilichotumika wiki moja iliyopita na bidhaa iliyouza zaidi ya nyingine.

Vitu hivi unapaswa kuvifahamu. Na kama bado hujajenga utaratibu wa kutunza hesabu za biashara yako, basi anza leo kwani hujachelewa.

Suala la tatu ni kuwa mwanafunzi wa kudumu. Inawezekana biashara unayofanya wewe si wa kwanza. Kwa mfano kama unauza viatu viwe vya mtumba au vipya, bila shaka utakubaliana na mimi kwamba kuna watu waliwahi kuifanya biashara hii.

Kila wakati huwa tunajifunza kutoka kwa wengine. Jaribu kujifunza wafanyabiashara kutoka kwa waliofanikiwa ili ukuze biashara yako huku ukitumia makosa ya walioshindwa kuiimarisha ya kwako.

Unapaswa kufungua macho yako na kuwa mtu wa kujifunza wakati wote. Maarifa utakayoyapata yatakusaidia kujua cha kufanya unapokabiliwa na changamoto wakati wowote.

Kama una uwezo wa kuwaona watu waliowahi kufanya biashara kama yako, watembelee ujifunze kutoka kwao na kama huwezi kukutana nao basi soma vitabu vinavyoihusu biashara yako.

Jifunze wakati wote. Badilishana mawazo na wanaoijua biashara unayoifany aau unayopanga kuifanya kwani usipokuwa na maarifa ya kutosha, biashara yako itaangamia. Kumbuka, mfanyabiashara huwa hahitimu.

Usijizuie kujua zaidi ya kitu kimoja. Usikazane kujua kitu kimoja tu kwenye biashara vkwani kuna wakati utakutana na vitu tofauti ambavyo vinahitaji uamuzi wako. Mfanyabiashara anapaswa kujua mambo kadha wa kadha.

Unapaswa kujua kuhusu hesabu za fedha, uongozi, huduma kwa wateja, kuzingatia muda na mambo mengine mengi. Yaani, ijue biashara yako nje ndani zaidi ya mtu wa kawaida ili uwe kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza na wateja, mamlaka za kodi na wadau wengine.

Usisahau kujifunza kuuza huduma au bidhaa uliyonayo. Biashara hutegemea mzunguko wa fedha, usipokuwapo, hufa. Fedha inapatikana kwa kuuza. Unapaswa kujifunza kuuza ili mzunguko uwepo.

Haitoshi kuwa na bidhaa bora kwani unaweza kuwa nazo lakini ukashindwa kuziuza hivyo kuwa kwenye uwezekano wa kuharibika na kukutia hasara kama si kuua biashara yako kabisa.

Ipo siri moja muhimu. Kama unataka kuwa muuzaji bora jiunge na wauzaji bora zaidi ya wewe. Kumbuka, chuma hunoa chuma. Usitegemee kuwa chuma wakati umezungukwa na mbao. Tuwasiliane kwa 0755 848 391