‘Fastafasta’ ya intaneti haiwezi kuua magazeti

Muktasari:

  • Magazeti yamekuwepo kabla ya intaneti; na mengine yamekufa kabla ya intaneti. Tekinolojia, katika kinachoitwa “mifumo mipya ya mawasiliano,” ingetarajiwa kuboresha kuliko kuua mifereji ya mawasiliano.

        Mjadala umerudishwa mezani; kwamba upatikanaji taarifa kwa njia ya simu na mitandao ya intaneti, utaua haraka njia za awali za mawasiliano, hasa magazeti. Uko wapi ukweli na usahihi?

Magazeti yamekuwepo kabla ya intaneti; na mengine yamekufa kabla ya intaneti. Tekinolojia, katika kinachoitwa “mifumo mipya ya mawasiliano,” ingetarajiwa kuboresha kuliko kuua mifereji ya mawasiliano.

Hoja ya kuua inatetemesha. Ni majuzi tu nilisikia wakisema hoja hiyo “inazunguzungisha;” eti hiyo ndiyo kuleta kizunguzungu. Wanasema tekinolojia itaua magazeti kwani siku hizi “walaji wanataka vya muda huohuo.”

Teknolojia inatarajiwa kuleta wepesi, urahisi wa kupeleka, kutawanya, kupokea taarifa; wepesi wa kushindana hata katika ubunifu; na kuongeza uhuru wa wengi kusema na kuwasiliana hata kama hawana vyombo vya habari.

Wahaya wana usemi kwamba “Ekileta eifa, nikyo kileta obushako.” (Kiletacho njaa ndicho kiletacho mahali pa kuhemea!). Wengi wa wanaochapisha magazeti ni haohao wanaoendesha au wanaoshirikiana na wapya katika kuendesha mifumo mipya kutoka vyumba vyao vya habari.

Leo hii mwandishi mmoja wa habari anaandikia vyombo vyote vya habari vya kampuni yake: anabeba kalamu na notibuku; kamera kwa picha za mnato na video; anaandika kwa ajili ya gazeti (la karatasi), gazeti la mtandaoni (online), redio, televisheni, facebook, Youtube, blogu, twitter na vingine.

Kwa njia hii, gazeti linaendelea kuwepo kwa usomaji unaohitaji kumbukumbu na kina cha taarifa na habari zake. Bali mwandishi mmoja anachukua nafasi za waandishi wanne au watano; na mpigapicha; na vyombo vyote vinahitajiana.

Hapa, atakayekufa haraka si gazeti bali mwandishi – mzembe, mvivu, asiyejituma, asiyeenda na nyakati, asiye na maarifa na utaalamu, asiye mbunifu na anayeng’ang’ania “lipualipua” na “fastafasta” isiyothamini weledi.

Salome Kitomari, Mwenyekiti wa MISA-Tan, akiandika kutoka Roma, Italia ambako amehudhuria Mkutano wa Baraza la Uongozi wa Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kilimo (International Fund for Agricultural Development) (IFAD), anasema walaji wanataka vya muda huohuo” – chakula motomoto. Anaeleza, “waandishi wa habari za social media wametengewa eneo la mbele na sisi wa vyombo vingine, yaani traditional media, tupo nyuma yao. Tafsiri ya haraka ni kuwa social media inaongoza kwa sasa na ndiyo mwelekeo wa dunia. Mabadiliko hayakwepeki…”

Anachosema Salome ni kweli. Watoa fedha wanaelekeza penye wepesi wa kuwasilisha taarifa. Pamoja na umuhimu wa mawasiliano ya kitekinolojia, wanataka taarifa zao zifike haraka; waone na waonekane wanafanya nini.

Wanataka kufikia washirika na vibarua wao kwa urahisi na wepesi; wapate haraka mrejesho juu ya fedha zao; waweze kutoa taarifa kwa watoa fedha na kusiwepo kudainana ripoti kwa miezi na miaka.

Lakini ni katika mazingira gani; yenye vyombo vipi; kiwango gani cha maendeleo na utamaduni gani – hata utamaduni wa mawasiliano?

Woga kwamba magazeti yanakufa upo kwa zaidi ya miaka 20 sasa na muuaji wake mkuu ni “ukosefu wa matangazo” kutoka watangazaji wakuu ambao sasa wanataka kujiona kwenye uhai wa kusikika na kuonekana katika vyombo vikubwa zaidi na vinavyosikika na kuonekana mbali zaidi.

Matangazo yamekuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato vilivyowezesha magazeti kukua haraka – kuongeza idadi ya waandishi bora, kusomesha wengine, kuongeza idadi ya nakala zinazochapishwa na kufikishwa vijijini.

Wauaji wengine wakuu ni ugumu wa kuwafikia walengwa – ukosefu wa mipabgo na miundombinu ya mawasiliano; ukosefu wa utaalamu ambao unakabili pia mitandao ya intaneti; na ukosefu wa nidhamu ya matumizi na udhibiti wa raslimali.

Utakuta basi, majigambo yako katika mbwembwe za “njia mpya na kasi ya mawasiliano;” siyo katika ubora wa bidhaa inayozalishwa na kusambazwa kwa walaji – taarifa na habari. Ukiondoa tunachoweza kuita “uhuru wa kuwasiliana,” kansa za vyombo vya kale na vya kisasa ni zilezile. Maadui wake ni walewale. Upya siyo kinga.

Katika hili, bila maarifa na weledi; bila mbinu na kujituma, njia mpya za mawasiliano zinaweza kufa haraka na kuacha magazeti yakichechemea. Bali mazingira ya sasa yanaelekeza kuwa hakuna cha kushangilia au kuhuzunisha.

Chombo kitakachoshindwa kutafuta, kutafiti, kuripoti taarifa na habari za kweli, za kina na zilizoandikwa kwa weledi, utondoti, usahihi na zinazothibitika, kitakufa kabla hakijauawa na yeyote.