TFF ijitathmini hukumu ya Wambura

Ijumaa iliyopita Mahakama Kuu ilitengua uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka (TFF) ambayo ilimfungia maisha makamu wa rais wa chombo hicho, Michael Wambura.

Mahakama ilibaini kuwa Kamati ya Rufaa ya TFF haikuzingatia katiba ya shirikisho hilo wakati ilipofikia uamuzi wa kumfungia maisha kujihusisha na soka baada ya kumkuta na hatia ya makosa matatu; kupokea fedha za malipo ambayo hayakuwa halali, kughushi barua ya kutaka alipwe fedha za kampuni ya Jeck System na kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho hilo.

Hata hivyo, suala lake liliendeshwa katika hali ambayo ilizua maswali na kuacha mwanya kwa Wambura kuhoji maamuzi hayo na hatimaye kwenda nje ya mfumo wa utoaji haki wa TFF, yaani kwenda mahakamani.

Ni dhahiri kuwa sheria za nchi ndizo sheria kuu zinazoongoza shughuli zote, hata pale jumuiya, chama au shirikisho linapounda vyombo vyake vya maamuzi ili viamue kulingana na mahitaji na mazingira ya shughuli za chama hicho.

Ni kwa sababu hiyo, waendeshaji mpira wa miguu waliona busara kukataza wanachama wao na wadau wengine kupeleka masuala ya mpira mahakamani kwa sababu kwanza mahakama za kawaida huchukua muda kufanya uamuzi wakati mchezo wenyewe unahitaji maamuzi ya haraka ili uendelee.

Pia shughuli za maendeleo zinaweza kukwama ikiwa wadau wake watakwenda mahakamani kupinga baadhi ya mambo na hivyo kulazimika kusubiri hadi uamuzi wa mahakama utolewe.

Lakini huwezi kukataza wadau kwenda mahakamani kabla ya kwanza kutengeneza vyombo vya haki ambavyo vina uhuru wa kutoingiliwa na viongozi ili kunapotokea matatizo yaamuliwe bila ya kamati kulazimishwa au kushawishiwa.

Ndio maana TFF ikaunda Kamati ya Maadili kushughulikia masuala ya kimaadili na iwapo mmoja hataridhika na uamuzi huo, analazimika kwenda Kamati ya Rufaa ya Maadili na asiporidhika tena, basi aende Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) au Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo.

Na vyombo hivyo vyote ni lazima vitende haki kwa uhuru na haki ionekane inatendeka ili vijijengee hali ya kuaminika na kuzuia wanachama wake kukimbilia mahakamani. Hata mahakama inapoona vyombo hivyo vilifuata taratibu zake vizuri na kuheshimu katiba, hujifunga mikono.

Katika siku za karibuni, kamati hizo za TFF zimekuwa zikifanya maamuzi ambayo yameibua maswali. Baadhi ya walioadhibiwa wamepuuza adhabu hizo kwa sababu hawaoni athari zake na wengine kama Wambura wameamua kupambana mahakamani kudai haki zao.

Hii ni kutokana na kamati hizo kufanya maamuzi yanayoonekana yana dosari, kiasi cha baadhi ya watu kutuhumu kuwa viongozi wa TFF wanashughulikia wapinzani wao au watu wanaoweza kuwa wapinzani wao katika uchaguzi ujao.

Fikra za aina hii hazitakiwi ziendelee kujijenga miongoni mwa wanachama na wadau wa soka kwa kuwa zikizidi, itaonekana kuna matatizo na uthibitisho utaonekana dhahiri. Kibaya zaidi idadi ya watu watakaokimbilia mahakamani inaweza kuongezeka na kufikia hatua shughuli za soka zikaanza kusimamishwa kusubiri maamuzi ya mahakama.

Hivyo ni lazima kamati huru za TFF zifanye maamuzi bila ya kuacha maswali na bila dosari ili zianze kuaminika na kuondoa fikra kuwa zinatumiwa na viongozi waliopo madarakani ama kukomoa watu au kushughulikia wapinzani wao katika uchaguzi.

Ni lazima Kamati ya Utendaji ya TFF, ambayo ni chombo cha pili kwa ukubwa baada ya Mkutano Mkuu, iliangalie suala hilo kwa mapana na marefu na pale panapostahili marekebisho, yafanyike mapema.