Unahitajika mjadala wa kitaifa kujadili michezo nchini

Muktasari:

  • Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kesho itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Cape Verde kuwania kufuzu fainali za Afrika ‘Afcon 2019’ ikiongozwa na kocha Emmanuel Amunike baada ya kufungwa magoli 3-0 ugenini.

Timu ya Taifa (Taifa Stars) iko katika vita ya kuwania nafasi ya kufuzu Fainali za Afrika, zilizopangwa kufanyika nchini Cameroon, mwakani.

Karata ya Taifa Stars kucheza fainali hizo mara ya pili baada ya kufuzu mwaka 1980 imeshikiliwa na Cape Verde katika mchezo wa marudiano utakaochezwa kesho.

Timu hizo zitarudiana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya Taifa Stars kupoteza ugenini mjini Praia kwa kufungwa mabao 3-0.

Taifa Stars bado ina nafasi ya kusonga mbele katika fainali hizo licha ya kuvuna pointi mbili katika msimamo wa Kundi L lenye timu za Uganda, Cape Verde, Lesotho na Tanzania. Uganda inaongoza kwa pointi saba ikifuatiwa na Cape Verde (nne), Tanzania na Lesotho zina pointi mbili kila moja.

Timu hiyo inayonolewa na kocha na mshambuliaji nyota wa zamani wa Nigeria Emmanuel Amunike, ilianza kampeni kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Lesotho kabla ya kulazimisha suluhu na Uganda ‘The ‘Cranes mjini Kampala.

Matokeo dhidi ya Cape Verde, yameibua mjadala kwa wadau na viongozi wa vyama vya michezo kila mmoja akitoa maoni kuhusu mwenendo wa Taifa Stars.

Baadhi ya wanamichezo walikwenda mbali na kuhoji uimara wa kikosi cha Taifa Stars na wengine walikosoa upangaji wa kocha Amunike.

Wengine walidai kuwa Amunike hana njia ya mkato ya kupata ushindi katika mchezo wa kesho kwa kuwarejesha katika kikosi baadhi ya wachezaji aliowaengua kwa utovu wa nidhamu.

Pia wapo waliohoji kudorora kwa sekta ya michezo nchini hasa katika ushiriki wa timu za Taifa kwenye mashindano ya kimataifa.

Kauli hizo tofauti zinaonyesha jinsi gani wadau wanavyoguswa moja kwa moja na matokeo mabaya kwa klabu na timu zetu za Taifa zinaposhiriki mashindano ya kimataifa.

Matamko ya wadau hao ni mwendelezo wa kauli aliyotoa hivi karibuni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leodegar Tenga alipozungumza na viongozi wa vyama vya michezo.

Tenga alisema Tanzania itapata mafanikio endapo kutakuwa na mjadala wa pamoja kujadili kwa kina maendeleo ya michezo, vinginevyo sekta hiyo haiwezi kufanya vyema katika mashindano ya kimataifa.

Ingawa matokeo ya Taifa Stars yamechukuliwa kama kigezo, lakini ukweli unabaki kuwa michezo imedorora na kila mmoja analalamika wakiwemo viongozi waandamizi.

Kauli nyingi zimekuwa zikitolewa kuhusu kuzorota kwa michezo nchini, lakini hakuna majibu stahiki ya maswali ambayo mara kwa mara yamekuwa yakiulizwa na wadau.

Wachezaji ngazi ya klabu, timu za Taifa na viongozi wa vyama vya michezo ni walewale, lakini hakuna mabadiliko siku zote Watanzania wamekuwa wakiumizwa na matokeo mabaya ya timu zetu katika mashindano ya kimataifa.

Pia uchaguzi wa viongozi wa klabu na vyama vya michezo umekuwa ukifanyika kwa mujibu wa kalenda, lakini hakuna maendeleo ambayo Watanzania wanaweza kujivunia zaidi ya kupata ‘majeraha’ ndani ya mioyo.

Hakuna mchezo tunaoweza kujivunia unaoweza kututoa kimasomaso kama ilivyokuwa miaka ya 1970 hadi mwishoni mwa 1990 ambapo Tanzania ilikuwa kinara katika riadha, ngumi, kuogelea na netiboli.

Ukiondoa mafanikio waliyopata baadhi ya wanamichezo akina Filbert Bayi, Selemani Nyambui, Juma Ikangaa, Gidamis Shahanga (riadha), Makoye na Willy Isangura, Koba Kimanga, Timothy Kingu na Michael Yombayomba kwa upande wa ngumi waliovuma katika Olimpiki na Madola, hakuna majina mengine yaliyovuma katika mashindano ya kimataifa kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Bila shaka kauli ya Tenga inapaswa kufanyiwa kazi ili kupata majibu stahiki ili kuhakikisha sekta ya michezo kwa ujumla inapata mafanikio.

Hakuna sababu za msingi zinazotolewa na viongozi, makocha au wachezaji timu inapofanya vibaya katika mashindano ya kimataifa.

Kwa mtazamo wangu mjadala wa pamoja wa kitaifa unaweza kuwa mwarobaini wa kutibu ‘ugonjwa’ wa muda mrefu unaotusumbua wa kushindwa kupata maendeleo katika medani ya michezo.

Mjadala wa pamoja ambao kimsingi utashirikisha wataalamu waliobobea na weledi wa maeneo tofauti ambao mchango wao utakuwa msingi wa kutibu ugonjwa wa muda mrefu unaotusumbua.

Bila kuwekwa mkakati wa pamoja, timu za Tanzania zitaendelea kuwa wasindikizaji na itakuwa ndoto kuwapa akina Yombayomba wapya wakati tuna idadi kubwa ya wanamichezo wenye vipaji kuanzia ngazi za shule ya msingi, sekondari na vyuo.