#WC2018: Eti nini? Ujerumani unaichukulia poa

Muktasari:

  • Hata hivyo, wakati kila mtu akiamini mabingwa hao watetezi hawataweza kutetea taji lao walilochukua mwaka 2014, wakiipiga Argentina 1-0 kwa goli la dakika za lala salama lililotiwa kimiani na Mario Gotze, kuna mtu anayeamini Wajerumani watazinduka na kutetea ubingwa wao.

Moscow, Russia. Watu wameanza kuchonga, watu wanawabeza sana tu. Kila mtu anasema lake, baada ya kunyukwa na Mexico bao 1-0, katika mechi yao ya kwanza ya Kombe la Dunia, kila mtu anaamini Ujerumani hawana jipya, wanaichukulia poa tu.

Hata hivyo, wakati kila mtu akiamini mabingwa hao watetezi hawataweza kutetea taji lao walilochukua mwaka 2014, wakiipiga Argentina 1-0 kwa goli la dakika za lala salama lililotiwa kimiani na Mario Gotze, kuna mtu anayeamini Wajerumani watazinduka na kutetea ubingwa wao.

Timo Werner, anayeunda kikosi cha 'German Machine', anaamini Kombe la Dunia 2018 ni lao kama ambavyo baadhi ya watu wanavyoamini huu ni mwaka wa Lionel Messi. Itawezekana kweli? Msikilize Timo Werner.

Baada ya Hirving Lozano, kuitekenya Ujerumani kwa bao la mapema, katika mchezo wa Kundi F uliopigwa jana, Werner anasema Ujerumani ambayo iliingia katika michuano hii, kwa kushinda mechi moja kati ya sita za kirafiki, watawashangaza wengi katika mechi zinazofuata.

Kikosi cha Joackim Low, kitajitosa uwanjani Jumamosi ijayo kuwakabili Sweden na Werner, mwenye umri wa miaka 22, anaamini wana kila sababu ya kujipanga upya na kuwa timu ya kwanza kutetea ubingwa wao kwa mara ya kwanza, tangu Brazil walivyofanya hivyo mwaka 1962.

"Eti nini, nani kasema tumeshindwa, tuko njiani kufanya maajabu, tutazinduka na kutetea ubingwa wetu. Tuliteleza lakini tumejiandaa kwa ajili ya mechi ijayo, sisi ni Ujerumani, hatujawahi kukata tamaa, tunataka kushinda kila mechi inayofuata," alisema Werner.