#WC2018: Nyota Man United aifanya kitu mbaya Costa Rica

Muktasari:

  • Serbia inaongoza Kundi E ikifuatiwa na Brazil na Uswisi na Costa Rica

Moscow, Russia. Nyota wa zamani wa Manchester City, Aleksandar Kolarov alipiga mpira wa adhabu hatari katika kipindi cha pili na kuiongoza Serbia kuitandika Costa Rica 1-0, katika mchezo mkali wa kundi E uliochezwa kwenye Uwanja wa Samara Arena.

Baada ya kushambulia lango la Costa Rica mfululizo tangu kuanza kwa kipindi cha pili, Serbia inayoundwa na nyota kadhaa akiwemo kiungo a Manchester United, Nemanja Matic, ilipata faulu, ambapo Nahodha huyo alipita mbele kujaribu bahati yake, akafumua shuti kali lililomuacha kipa wa Costa Rica, Kayla Navas, akishangaa tu.

Bao la Kolarov lilifikisha idadi ya mabao matatu yaliyofungwa kwa mipira ya adhabu katika Kombe la Dunia 2018.

Costa Rica walipata nafasi kibao za kubadilisha matokeo, katika kipindi cha kwanza, lakini uimara wa beki ya Serbia, ikiongozwa na Ivanovic.

Hii ni mechi ya nne kwa Serbia kushinda 1-0 katika Kombe la Dunia. Kabla ya mchezo huo, Serbia ilicheza kwenye mashindano matatu ya Kombe la Dunia na kutoka na matokeo kama ya leo. Walishinda 1-0 dhidi ya Ujerumani, (mwaka 2010), Iran na USA, mwaka 1998.