#WC2018: Serbia yaanza kwa kasi kundi la kifo

Muktasari:

  • Bao la Serbia liliwekwa wavuni na Aleksandar Kolarov baada ya kupiga faulo dakika ya 56 ya kipindi cha pili.

Moscow, Russia. Timu ya Serbia imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Costa Rica katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia uliopigwa leo Jumapili.

Bao la Serbia liliwekwa wavuni na Aleksandar Kolarov baada ya kupiga faulo dakika ya 56 ya kipindi cha pili.

 Awali, kabla ya mchezo huo, kiungo wa Manchester United na Serbia Nemanja Matic, alisema anaamini taifa lake halina presha yoyote kuelekea mchezo wao wa kwanza wa E dhidi ya Costa Rica, uliopigwa kuanzia saa 9 alasiri.

Ushindi huo unaipa nafasi Serbia kuanza kampeni yake ya kupenya kundi E, linaloundwa na wagumu Brazil na pamoja wabishi Switzerland lakini Matic anaamini hilo halitakuwa tatizo kwao kwani wamejiandaa kucheza mechi moja baada ya nyingine.

 Hata hivyo, Matic anaamini kukata tiketi ya kucheza michuano hii, ambayo wamekuwa wakishiriki tangu mwaka 2010, imewafanya wapate kiburi cha kucheza na timu yoyote inayokatiza mbele yao.

"Tulikuwa na presha kubwa kabla ya kufuzu michuano hii, kwa kuwa hatukuwepo Brazil, huu ndio muda wa kuonesha uwezo wetu na sio kuanza kuogopa," Matic aliuambia mtandao wa Manchester United. Kiungo huyo ambaye anashiriki fainali yake ya kwanza ya Kombe la Dunia, alikataa kuzungumzia suala la hatma ya timu yake katika kundi E ambayo inadaiwa kuwa miongoni mwa makundi ya vifo kwenye michuano ya mwaka huu..