#WC2018: Suarez apiga bao la 52

Muktasari:

  • Bao hilo sio tu kuwa lilimuongezea idadi ya mabao aliyopata kuifungia nchi yake, lakini pia lilitosha kuipeleka Uruguay katika raundi ya pili ya fainali hizo, kutokana na kufikisha pointi sita ambazo kimsingi imefuzu kwa hatua ya mtoano ya 16 bora licha ya kuwa na mchezo mmoja mkononi.

Moscow, Russia. Bao alilofunga mshambuliaji mahiri wa Uruguay, Luis Suarez walipocheza na Saudi Arabia jana katika mechi ya pili ya fainali ya Kombe la Dunia kutoka kundi A, lilikua bao lake la 52 katika mechi yake ya 100 tangu alipoanza kulitumikia taifa lake.

Bao hilo sio tu kuwa lilimuongezea idadi ya mabao aliyopata kuifungia nchi yake, lakini pia lilitosha kuipeleka Uruguay katika raundi ya pili ya fainali hizo, kutokana na kufikisha pointi sita ambazo kimsingi imefuzu kwa hatua ya mtoano ya 16 bora licha ya kuwa na mchezo mmoja mkononi.

Aidha bao hilo la Suarez liliwaondosha rasmi mashindanoni Saudi Arabia kwa kuwa huo ulikua mchezo wao wa pili kupoteza baada ya ule wa kwanza dhidi ya wenyeji Russia kupigwa mabao 5-0 hata hivyo watasubiri kucheza mechi ya mwisho ya kukamilisha ratiba dhidi ya Misri ambayo nayo imeng’oka, wakati Uruguay itacheza mechi ya mwisho ya makundi na wenyeji Russia kujua timu itakayoongoza kundi A.

Suarez mwenye miaka 31 alianza kuitumikia Uruguay mwaka 2007 lakini hivi sasa amekua tegemeo mno kwenye taifa lake kutokana na kupambana kwake kusaka matokeo katika kima mchezo na amekua na wastani wa kufunga katika kila michezo miwili.