Mkataba uwekezaji ‘wamfunga’ Mo Dewji

Muktasari:

Wanachama 1,310 waliohudhuria mkutano mkuu wa Simba uliofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam waliunga mkono ushindi wa Dewji.

Dar es Salaam. Licha ya Klabu ya Simba kuingia katika historia mpya baada ya kumtangaza Mohammed Dewji ‘Mo’ kushinda zabuni ya uwekezaji, mkataba aliyoingia mfanyabiashara huyo maarufu nchini ‘unamfunga’.

Wanachama 1,310 waliohudhuria mkutano mkuu wa Simba uliofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam waliunga mkono ushindi wa Dewji.

Dewji ambaye ni mwanachama wa muda mrefu katika klabu hiyo, amekubali kutoa Sh20 bilioni kupata asilimia 49 ya hisa kwa mujibu wa sheria za Serikali.

Pamoja na mkataba huo wa mabadiliko, Dewji hatakuwa na nguvu ya kisheria kununua hisa nyingine kutoka kwa wanachama.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ ameliambia gazeti hili jana kwamba kipengele cha Dewji kununua hisa zaidi kwa siku za baadaye kimefungwa.

“Mkataba haumruhusu MO kununua hisa zaidi ya ambazo atanunua sasa, hizo alizonuanua ndizo zitakuwa hizo hizo mkataba haumruhusu kuongeza zaidi,” alisema Abdallah ambaye anakaimu nafasi ya Evance Aveva ambaye yuko gerezani.

Mabadiliko ya mfumo

Mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo utabadilika ukihusisha viongozi waliochaguliwa na wanachama katika uchaguzi mkuu kwa nafasi za Rais, Makamu na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Mfumo mpya utakuwa na wajumbe 14, saba watatoka kwa Dewji na wengine saba watachaguliwa na wanachama na baadhi ya kazi zao ni kupitisha masuala yote makubwa ndani ya klabu ikiwemo usajili, uwekezaji, bajeti, kuajiri, udhamini huku Dewji akiwa mwenyekiti.

Kilomoni aikomalia Simba

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Simba, Hamisi Kilomoni ambaye alifungua kesi mahakamani kupinga mchakato huo, amesisitiza hana mpango wa kufuta kesi hiyo.

“Siwezi kufuta kesi hadi nijiridhishe mchakato huo unafanyika kama ambavyo Serikali imetaka iwe kwa mwekezaji kupewa asilimia 49 na wanachama asilimia 51 za hisa.

“Hicho ndicho ambacho hata mimi nakitaka, lakini naona kama hawa waheshimiwa (viongozi wa Simba) wanataka kutoa asilimia 50 kwa 50 kwa habari nilizozipata, kitu ambacho sikubaliani nacho hata kidogo.

“Ili nifute kesi, kwanza mchakato huo umalizike na twende sawa kama ambavyo Serikali imesisitiza, tukienda sawa sina haja ya kuendelea na kesi, maana lengo langu mimi sio Simba isibadili mfumo, napinga mwekezaji kupewa hisa sawa na wanachama.

“Hicho kitu nitakipinga milele, lakini wakifuata maelekezo ya Serikali, mchakato ukafanywa kwa haki sina tatizo na masuala ya kesi, lakini kwa sasa sifuti hadi mambo yawe sawa,” alisisitiza Kilomoni aliyesimamishwa uanachama kutokana na msimamo wake wa kupinga mabadiliko.

Hata hivyo, Abdallah hakutaka kuzungumzia mpango huo wa asilimia 50 za hisa kupewa Dewji kama ambavyo Kilomoni ameonyesha wasiwasi na kusisitiza kwamba hayuko katika nafasi ya kuzungumzia suala hilo.

Katibu Yanga atoa neno

Wakati klabu ya Simba ikifanya mabadiliko ya mfumo, watani wao wa jadi Yanga wameanza mchakato huo kimyakimya.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa aliliambia gazeti hili jana kwamba mchakato huo kwao umeanza.

“Mabadiliko ya uendeshaji wa klabu kwa Yanga bado yanaendelea, mpango huo uko pale pale na hivi tunavyozungumza kuna michakato inaendelea.

“Hata hivyo, siwezi kuiweka wazi kwa sasa kwa kuwa ni mambo ya ndani ya klabu itakapofika wakati wa kuyaweka wazi tutafanya hivyo, lakini wana Yanga wakae mkao wa ‘kula’ siku si nyingi tutaanza mchakato huo,” alisema Mkwasa.

Kipingu, Dalali wafunguka

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu, Iddi Kipingu alisema anaunga mkono mabadiliko ya Simba.

“Tunaposema michezo ni ajira lazima tuwe na sehemu tunazalisha, iwepo mikataba yakinifu lakini pia vyanzo vya mapato ambavyo vilikuwa havipo mfano yale ya jezi yakidhibitiwa maana yake ni kwamba mapato yataingia kwenye kapu la maendeleo.

“Matamshi aliyotoa mwekezaji hayo ndiyo tunayataka, Simba imeanza na wengine wafuate timu hizi za Simba na Yanga kwa miaka sasa zimecheza soka bila maendeleo ila Simba sasa imevunja mwiko na wengine waige,” alisema Kipingu.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba, Hassani Dalali alisema mpango huo unaipeleka katika hatua nyingine klabu hiyo kujiendesha kimataifa.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) sasa TFF, Said El Maamry ameunga mkono mchakato wa Simba kufanya mabadiliko, lakini alisisitiza Simba inatakiwa kuimarisha umoja na mshikamano.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Nchini, Yusufu Singo alisema Simba haipaswi kubadili chochote katika utaratibu wa hisa kwa kuwa mwekezaji ataendelea kubaki na asilimia 49 na wanachama asilimia 51.

“Hiyo ni sheria ambayo imepitishwa, haiwezi kubadilika,” alisema Singo

Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji Jaji Mstaafu Thomas Mihayo alimtangaza Dewji kushinda zabuni hiyo baada ya kukidhi vigezo stahiki.

Ahadi za Dewji

Baada ya kutangazwa mshindi, Dewji alitangaza ‘mambo’ saba ambayo atafanyia kazi ikiwemo ujenzi wa viwanja viwili vya mazoezi ambapo kimoja kitakuwa cha nyasi bandia na kawaida.

Pia ameahidi ujenzi wa hosteli yenye vyumba 35 ambavyo ndani vitakuwa vimesheheni samani, sebule na jiko.

Ameahidi ujenzi wa mgahawa na eneo la kuburudika wachezaji, studio ya kuzalisha vipindi vya televisheni vya Simba, ‘gym’ na akademia za timu za vijana ili kuuza ndani na nje ya nchi.

Kukamilika mchakato wa kumpata mshindi wa zabuni ya uwekezaji katika klabu ya Simba, kumetimiza ndoto ya muda mrefu waliyokuwa nayo wanachama.

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, wanachama wa klabu hiyo watapewa asilimia 10 ya hisa na nyingine 40 zitaachwa kama akiba kwa ajili ya kuuzwa baadaye.

Hata hivyo, mabadiliko hayo pia yanaweza kuwa shubiri kwa klabu hiyo kwenye baadhi ya maeneo kutokana na mazoea ya wanachama na mashabiki wa soka nchini.