Wakati wa kubadilika ni huu kuelekea Tanzania ya Viwanda

Muktasari:

  • Rais anasisitiza hivyo kwa kuwa anatambua nchi mbalimbali duniani zilizoendelea zimejengwa na uchumi wa viwanda.

Serikali imeendelea kusisitiza nchi lazima ielekee kwenye uchumi wa viwanda kama Rais John Magufuli anavyosema, “Tunataka Tanzania ya Viwanda”.

Rais anasisitiza hivyo kwa kuwa anatambua nchi mbalimbali duniani zilizoendelea zimejengwa na uchumi wa viwanda.

Lakini ukitazama kwa undani, nchi hizo zilipoanza harakati za kujijengea uchumi wa viwanda hazikuiacha nyuma sekta ya kilimo, bali ilikwenda nayo sambamba.

Hii itasaidia kutoa mwanga kuwa kila penye kilimo cha uhakika kinachozalisha malighafi za kutosha ndipo panakuwa na viwanda vya uhakika.

Unapokuwa kwenye nchi ambayo asilimia zaidi ya 80 ya watu wake wanategemea kilimo kama chanzo cha mapato, kisha ajenda yako ikawa ni kujenga viwanda, si jambo baya, lakini unapaswa kuwekeza nguvu zaidi kwenye kilimo ili viwanda vijengwe na vidumu kwa uhakika.

Na kwa hakika, ili kukuza kilimo katika nchi yetu yako mambo ambayo tunapaswa kuyazingatia kwa haraka na tukishayafanikisha tutakuwa na uwezo wa kutengeneza viwanda vya uhakika.

Nasema hivyo kwasababu ukuaji wa kilimo unategemea umewekeza nini na kina thamani kiasi gani.

Pamoja na kwamba takribani robo tatu ya Watanzania wanategemea kilimo, kilimo hicho kinachangia walau asilimia 28 kwenye Pato la Taifa ukikijumuisha na uvuvi na ufugaji.

Kwa maana nyingine, wakati tunaendelea na mipango ya kujenga na kufufua viwanda, yatupasa kuonyesha pia kwa kivitendo namna ya kuboresha kilimo cha kisasa nchini.

Bila kufanya hivyo, tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu kama usemi wa mababu usemavyo.

Ni lazima tuanze kupandisha thamani yake ili kichangie kwa asilimia kubwa zaidi kwenye pato la Taifa ili safari tuliyoianza ya kuelekea kwenye uchumi wa viwanda tuisafiri bila vikwazo. Kwa mfano kilimo cha umwagiliaji kinapaswa kutazamwa kwa jicho pevu wakati huu. Hatupaswi kuendelea kung’ang’ania kilimo cha majira ya mvua ambacho kwa kiwango kikubwa kinaathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa kila mwaka.

Lakini, umwagiliaji utaondoa matatizo ya mabadiliko ya hali ya hewa yasiyo rafiki kwa kilimo.

Takwimu za Serikali zinaonyesha kwa mwaka 2015 ukuaji wa shughuli za kilimo kwa maana ya mazao, ufugaji, misitu na uwindaji ulipungua na kufika asilimia 2.3 kutoka 3.4 kwa mwaka 2014. Kiwango hicho ni kidogo kwa wastani wa ukuaji wa asilimia 3.2 kwa kipindi cha mwaka 2010/ 2013.

Ili tufikie lengo, Serikali inatakiwa ijenge miundombinu ya umwagiliaji kusudi iende sambamba na utoaji wa taarifa na elimu ya kutosha kwa wakulima. Kwa mfano hivi sasa, ukisikiliza redio na televisheni za umma na binafsi, zinatumia muda mchache kuelimisha wananchi na wakulima juu ya kilimo bora na cha kisasa.

Hata matangazo yanayohamasisha kilimo bora hayapo, wakulima wameachwa kama watoto yatima.

Kama kweli tutataka tufikie adhma ya Tanzania ya Viwanda, tuimarishe kwanza kilimo itasaidia kuepuka gharama za kusaka mali ghafi nyingi nje ya nchi. Lakini pia Tanzania ina upungufu mkubwa wa wataalamu wa kilimo, ukienda vijijini mabibi na mabwana shamba ni wa kuhesabu na hawawatembelei wakulima kwa mwendelezo endelevu.

Unaweza kumkuta Bwana Shamba amekaa ofisini katikati ya msimu wa kilimo wakati alipaswa awe shambani kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima.

Kwa mwendo huu, inapasa watu wabadilike, nchi inahitaji maendeleo ili siku moja na sisi tusimame kama Wachina wanavyojivunia maendeleo yao. Serikali ina rekodi ya kusimamia miradi mingi ya kilimo, lakini mingi imeonekana kutoleta tija kwa Taifa kwa sababu tu ya utekelezaji wake usio na tija.

Tusipobadili mbinu zetu kwenye wataalamu, mipango yetu na usimamizi wa miradi ya kilimo, hatutaweza kutekeleza kile tunachokihitaji kwenye marathoni tuliyoianza ya Tanzania ya Viwanda.

Ikumbukwe tunapozungumzia kilimo, tunapaswa pia kutazama suala la mbegu bora sambamba na mbolea. Kwani kilimo hakiwezi kwenda bila mbolea za kisasa.

Wakati mahitaji ya nchi kwa mujibu wa takwimu za Serikali ni tani 485,000 za mbolea kwa mwaka, utafiti unaonyesha hadi Machi mwaka jana, Serikali iliagiza tani 297,000 za mbolea kutoka nje huku tani 140,000 ya mbolea iliyotengenezwa nchini ilisafirishwa kuuzwa nje ya nchi.

Hatuwezi kuzalisha mbolea kisha kuiuza nje wakati bado tuna mahitaji makubwa, hatutaweza kuhudumia viwanda kama hatuna mbolea ya uhakika.

0713235309