Bashe, Zitto waikosoa Serikali ndoto ya Tanzania ya viwanda

Muktasari:

Mbunge wa Nzega Mjini, (CCM), Hussein Bashe, alienda mbali na kudai hata Waziri wa Viwanda, Charles Mwijage akihubiri sera hiyo kwa Injili na Quran, bado hatatoboa kwa mazingira yaliyopo.

Dodoma. Wabunge jana waliendelea kuibana Serikali juu ya ndoto yake ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025, wakisema kwa mazingira ya kodi yaliyopo, ndoto hiyo haiwezekani.

Mbunge wa Nzega Mjini, (CCM), Hussein Bashe, alienda mbali na kudai hata Waziri wa Viwanda, Charles Mwijage akihubiri sera hiyo kwa Injili na Quran, bado hatatoboa kwa mazingira yaliyopo.

Wabunge hao walitoa mashambulizi hayo bila kujali tofauti za itikadi zao bungeni jana wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya Viwanda, Biashara na Uwezeshaji kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Bashe alisema kuna tatizo kubwa nchini la kuunganisha visheni ya Rais John Magufuli ya kuifanya Tanzania ya viwanda, na utekelezaji halisi unaofanywa na wale wanaousimamia.

Alisema adui mkubwa wa ukuaji wa uchumi na uwekezaji wa viwanda Tanzania ni Wizara ya Fedha kutokana na sera zake zisizotabirika na zinazobadilika badilika katika utozaji kodi.

Huku akitoa takwimu kuonyesha jinsi Tanzania inavyoporomoka, Bashe alitolea mfano wa Sheria ya Uwekezaji iliyobadilishwa mara tano tangu 2009, namna inavyoweka vivutio na kuviondoa.

“Sheria hii tumeibadilisha mwaka 2009, 2010, 2012, 2014 na 2015. Tunafuta na kurudisha. Tunaweka incentive (vivutio) kesho tunafuta. Mwijage hata aihubiri kwa Injili na Quran hatutatoboa,” alisema.

Mbunge huyo alisema taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Aprili mwaka huu, inaonyesha sekta ya uzalishaji imeshuka kutoka Dola 1.4 milioni za Marekani hadi Dola 870,000.

Alitolea mfano wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ya 2012 ambayo inamtaka mfanyabiashara alipe ushuru wa huduma (service levy) wa asilimia 0.3 wakati huohuo wakala naye akitozwa na kusema kwa namna Wizara ya Fedha inavyotoza kodi katika sekta ya ngozi, hakuna mwekezaji anayeweza kushindana soko la kimataifa.

“Hapa Tanzania kuzalisha mufti moja ya mraba ya ngozi ni Dola senti 14, Ethiopia ni senti 8, India ni senti 7, Pakistani ni senti 8. Tunawezaje kushindana?” alihoji Bashe.

“Tumeweka kodi kwa ngozi tunayouza nje, ukiagiza kemikali kwa ajili ya kuzalisha ngozi unalipa kodi asilimia 25 na VAT asilimia 18. How can we grow (Tutakuaje?” alihoji Bashe.

Akichangia hotuba hiyo juzi jioni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe alisema mwaka jana Tanzania iliuza bidhaa za viwanda zenye thamani ya Dola 1.4 bilioni za Marekani.

Alisema takwimu za Machi mwaka huu zinaonyesha kuwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi yameshuka kwa Dola milioni 500 za Marekani ambazo ni sawa na Sh110 bilioni.

“Hii maana yake viwanda vyetu vya ndani vimepunguza uzalishaji. Maana yake kuna watu wamepoteza kazi, maana yake kuna mapato ya Serikali ambayo yamepotea. Maana yake viwanda vyetu vya ndani vimepunguza uzalishaji. Kama tumepunguza mauzo namna hii sijui kama ikifika mwaka 2020 tutakuwa na mauzo.”

Aidha, Zitto alisema uwezo wa nchi katika kulinda viwanda ni mdogo na kwamba Waziri Mwijage ni shahidi, “Kila mwezi amekuwa akipokea malalamiko ya wanaoingiza nguo, mafuta ya kula, betri kinyemela katika nchi yetu na zinakuwa na bei ndogo, matokeo yake zinashindwa kushindana na viwanda vya ndani na matokeo yake tunapoteza ajira.”

Alisema Idara ya Ushuru wa Forodha ya China inaonyesha kuwa kati ya Januari na Septemba Tanzania iliagiza betri kutoka China zenye thamani ya Dola 36.5 milioni lakini takwimu za Idara ya Forodha na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa betri zinazotoka nje ya nchi walizofanyia ukaguzi, zina thamani ya Dola 5.5 milioni tu. “Hii mana yake kuna betri nyingi zinaingizwa nchini kinyume cha taratibu. Haya ni mambo ambayo tunategemea kuona waziri unahangaika nayo,” alisema Zitto. Mbunge wa Busega (CCM), Dk Rafael Chegeni alisema bado kuna ukakasi wa namna viwanda vinavyotafsiriwa na kueleza kuwa kuna tatizo kubwa la mazingira ya uwekezaji.

Alisema ufanyaji wa biashara nchini ni ghali na kueleza kuwa katika sekta ya utalii, kuna kodi mbalimbali 36 na kumtaka Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango awe kiungo na sio mtenganishi.

Mbunge wa Manonga (CCM), Seif Gulamali alisema kuna urasimu mkubwa kwa mwekezaji anayetaka kuanzisha kiwanda, ambaye hulazimika kupata idhini kutoka zaidi ya taasisi sita. “Madubwasha yako mengi kwa mwekezaji anayetaka kuanzisha kiwanda. Kuna Osha, NEMC, TRA, TFDA, TBS. Serikali iwasaidie wanaotaka kuanzisha viwanda sio kuwawekea vikwazo.”

Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Jaffar Michael alisema vikwazo vilivyokuwa vinaikabili Tanzania mwaka 1996 wakati ikipitisha Sera ya Mapinduzi ya Viwanda, bado viko hadi leo. Aomba Serikali kufufua viwanda vikubwa vilivyokuwapo Moshi vikiwamo Kilimanjaro Machine Tools na Magunia, kama ina dhamira ya kweli ya kuanzisha viwanda.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Gimbi Masaba, alimpiga kijembe Waziri Mwijage na kusema katika jimbo analotoka hakuna hata kiwanda cha kuchakata ndizi.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Maria Kangoye alisema Tanzania kumekuwa na tozo nyingi na kodi zinazowakimbiza wawekezaji na kutolea mfano wa kampuni ya Omni Care ambao walikuwa wajenge kiwanda kikubwa cha sukari nchini, lakini urasimu katika upatikanaji wa vibali na leseni, uliwalazimu kuwekeza Maritius.

Mbunge wa Bagamoyo (CCM), Dk Shukuru Kawambwa alitishia kuondoa shilingi ikiwa Waziri hatatoa maelezo ni lini wananchi waliotoa maeneo yao kwa ajili ya uwekezaji watalipwa fidia.

Alisema miaka karibu 10 iliyopita, wananchi hao walitoa hekta 9,080 na uthamini ulionyesha zilihitajika Sh60 bilioni kulipa fidia, lakini hadi sasa zilizolipwa ni Sh26 bilioni tu.