Dk Shein auwaza Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020

Muktasari:

Akizindua tawi la CCM Kitope ‘B’ huko Mahonda akiwa katika ziara ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk Shein alisema viongozi na wanachama wa chama hicho wanatakiwa kutumia vyema ofisi za tawi hilo ambalo ni la kisasa kutekeleza kwa ufanisi kazi za kisiasa zitakazozaa matunda ya ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameuwaza Uchaguzi Mkuu wa 2020 na kuwataka viongozi na watendaji wa chama hicho kufanya kazi za kujiimarisha ili chama hicho kishinde na kuendelea kuongoza dola.

Akizindua tawi la CCM Kitope ‘B’ huko Mahonda akiwa katika ziara ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk Shein alisema viongozi na wanachama wa chama hicho wanatakiwa kutumia vyema ofisi za tawi hilo ambalo ni la kisasa kutekeleza kwa ufanisi kazi za kisiasa zitakazozaa matunda ya ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2020.

“Kwanza nakupongezeni viongozi na wanachama wote wa jimbo la Mahonda mlioshiriki kujenga tawi hili la kisasa linaloendana na hadhi ya chama chetu kimaendeleo kwani lina ofisi zote ambazo ngazi zote kiutendaji ndani ya tawi mtafanya kazi zenu kwa utulivu.

Alisema lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayotokana na CCM ni kuimarisha huduma zote za kijamii na kiuchumi ili wananchi wa mijini na vijijini waweze kunufaika na fursa hizo.

Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia alitembelea ujenzi wa kituo kipya cha mashine za kutibia maji kinachojengwa katika eneo la Donge Mbiji. Mradi huo uliofadhiliwa na Serikali ya China, utagharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 5.5.

Dk Shein alitembelea shamba la karafuu na kuzungumza na mkulima, Haroun Abou Mbarouk alimweleza kwamba amekuwa akivuna zaidi ya magunia 25 kutoka kwenue mikarufuu zaidi ya 170.