JWTZ yataja askari waliouawa Congo

Muktasari:

JWTZ imesema umma utajulishwa kuhusu mapokezi, kuaga na mazishi ya askari hao baada ya utaratibu kukamilika.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewataja askari wawili waliouawa na kundi la wapiganaji la ADF wakati wakilinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Askari hao wametajwa kuwa ni Koplo Maselino Paschal Fubusi na Praiveti Venance Moses Chimboni.

Imeelezwa askari wengine 12 wamejeruhiwa katika shambulio lililofanywa na kundi hilo.

Taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya JWTZ iliyotolewa leo Jumanne imesema, “Askari hao wamefariki baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi na kundi la waasi, tukio lililotokea Oktoba 9 umbali wa kilomita 24 mashariki mwa mji wa Beni.”

Amesema, “Majeshi yetu yamewarudisha nyuma waasi hao na kudhibiti eneo. Kutokana na shambulio hilo, Umoja wa Mataifa umeunda bodi ya uchunguzi wa tukio hilo,” imesema taarifa hiyo.

Imeelezwa maofisa na askari wa JWTZ wanaendelea kutekeleza majukumu yao katika operesheni hiyo.

Kuhusu miili ya askari hao kurejeshwa nchini, taarifa imesema Umoja wa Mataifa unaandaa utaratibu na itakapokamilisha wataujulisha umma mapokezi, kuaga na mazishi yatakavyokuwa.