Kesi ya Wema na wenzake kuunguruma Agosti Mosi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itaanza kusikiliza kesi ya aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu na wenzake ifikapo Agosti Mosi mwaka huu.

Wema na wenzake wanaotetetewa na Wakili Peter Kibatala walifika mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mwambapa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa, lakini wakili wa Serikali Esterzia Wilison aliomba ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kusikilizwa.

Wema na wenzake wanakabiliwa na mashtaka  mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.

Kwa upande wa Wema yeye anadaiwa kuwa Februari Mosi, 2017 katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam,  alitumia dawa za kulevya  aina ya bangi.

Wema na wenzake wawili ambao ni Angelina Msigwa (21) na Matilda Seleman Abbas tayari walishasomewa  maelezo ya awali.

Kadhalika Wakili Kakula amedai kuwa Wema ni miongoni mwa watu waliotajwa na Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, akituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.

Aprili 2, 2017 ukaguzi ulifanyika nyumbani kwa Wema  ambapo alipatikana na vitu vinavyodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya na kwamba ulifanyika mbele ya Wema mwenyewe, polisi na mashahidi huru.

Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa Februari 6, 2017 vitu hivyo vilivyopatikana nyumbani kwa  Wema, vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na Februari 8,2017 Mkemia Mkuu wa Serikali alitoa taarifa ya uthibitisho juu ya vielelezo hivyo kuwa ni bangi yenye uzito wa gramu 1.08.

Februari 8, 2017 Wema naye alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupimwa mkojo na majibu ya uchunguzi  wa mkojo wake yalionyesha kuwa alikuwa akivuta bangi.

 Baada ya kusomewa maelezo hayo ya awali, Wema alikubali majina yake, mahali anapoishi na kwamba alikuwa miongoni mwa watu waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wakituhumiwa  kujihusisha na dawa za kulevya.

Wakili Esterzia amesema ushaidi umekamilika na kesi iko tayari kwa ajiili ya kuanza kusikilizwa.