Kesi ya mbunge Sugu ilivyotikisa jiji la Mbeya

Muktasari:

  • Viongozi mbalimbali wa Chadema na wafuasi wao waliingia mahakamani hapo mapema huku wakiongozwa na Mbunge wa Mikumi Joseph Haule ‘Profesa Jay’ akiwa na Wakili Peter Kibatala.

 Kila aliyekuwa akiingia Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya jana, alilazimika kukaguliwa kabla ya kusikilizwa kwa kesi inayowakabili mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga.

Viongozi mbalimbali wa Chadema na wafuasi wao waliingia mahakamani hapo mapema huku wakiongozwa na Mbunge wa Mikumi Joseph Haule ‘Profesa Jay’ akiwa na Wakili Peter Kibatala.

Kibatala ambaye aliwasili hapa jana asubuhi kwa ndege alianza kazi ya kuwatetea Sugu na Masonga baada ya mawakili wao wa awali, Boniface Mwakubusi, Sabina Yongo na Hekima Mwasipu kujitoa.

Kabla ya kesi hiyo kuanza, Polisi waliwatawanya wananchi waliokuwa wameweka magogo na matairi katika barabara kuu maeneo ya Mafiati, Kabwe na Mwanjelwa wakishinikiza Mahakama kumpatia dhamana Sugu na mwenzake.

Hali hiyo ilizua tafarani baada ya watu kuanza kukimbia ovyo na wengine kuanguka baada ya kubaini kuwa polisi wamefika eneo la tukio.

Kesi ilipoanza, ubishani wa kisheria uliibuka baada ya hoja ya wakili Kibatala kutaka kuanza na shahidi wa kwanza ambaye ni mkuu upelelezi mkoa wa Mbeya (RCO) huku upande wa Jamhuri ukipinga.

Mabishano kati ya pande hizo mbili yalimlazimu hakimu mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite kuahirisha kesi kwa muda na kuwataka mawakili hao kwenda ofisini kwake ili wakajadiliane.

Awali, Kibatala aliieleza Mahakama hiyo kwamba wapo tayari kuendelea na utoaji ushahidi na ataanza na (RCO).

“Mmh! Naona kama kuna ukakasi, eti wakili upande wa Serikali?” alihoji hakimu Mteite.

Wakili wa Jamhuri, Joseph Pande alipinga shahidi huyo kuwa wa kwanza kuhojiwa tena akisisitiza kwamba, watuhumiwa ndio wanaopaswa kuanza.

“Kimsingi anayetakiwa kuanza ni mtuhumiwa kujitetea na kama atakuwa na mashahidi ndipo wataitwa... Sasa itakuwa ni jambo la ajabu kutokea kama ataanza shahidi tofauti na mhusika mkuu (mshtakiwa),” alisema Pande.

Kibatala alisimama na kupinga akidai hakuna kifungu cha sheria kinachozuia kufanya hivyo na wala hakuna athari yoyote.

“Hapa tutakuwa tunapoteza muda bure. Hakuna katazo lolote kisheria,” alisema Kibatala.

Baada ya kurejea, Sugu alianza kutoa ushahidi wake lakini hata hivyo, uliibuka ubishani mwingine baada ya wakili Pande kumuuliza mshatakiwa huyo kuwa ni Mkinga wa wapi.

Wakili Pande alianza kwa kuumuliza, “Ni vizuri kwa mbunge kuwa mwongo?

Sugu akajibu “Sio vizuri.” Wakili Pande akauliza tena, “Wewe ni Mkinga wa wapi?.”

Kabla ya kujibu swali hilo, Kibatala alisimama na kuomba mwongozo wa Hakimu akitaka wakili asiulize swali aliloita la kijinga na halina faida.

“Maswali gani kuulizana kabila? Uliza maswali ya maana,” alisema.

Hata hivyo, Pande alisema ni haki yake kuuliza swali lolote.

Waliendelea na mabishano hadi pale, hakimu Mteite alipoingilia kati na kusema, “Jamani yaani mnataka niiahirishe tena kesi turudi kule chemba tukafundane? Haya ninaahirisha twendeni.”

Baada ya kurejea, Sugu alikana kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Sugu akiongozwa na Kibatala akisaidiana na Fajari Mangula alidai kwamba hata ushahidi wa sauti uliotolewa na mashahidi wa Jamhuri sio sauti yake na hakuwahi kutamka maneno hayo kama inavyodaiwa na upande wa Jamhuri. Alisema hayo baada ya Kibatala kumuuliza, “Kuna madai ile sauti ni ya kwako, wewe unasemaje.”

“Sio sauti yangu…. Nilishangaa sana yule askari (shahidi) anachezesha sauti ile eti anasema ni yangu,” alijibu.

Pia, Sugu alikana Masonga kuwapo katika siku ya mkutano huo akidai kuwa hakumuona, bali alikuwa na viongozi wengine wa Chadema.

“Hata nilipomaliza mkutano wangu niliona respond (mwitikio) wa wananchi ulikuwa mzuri sana na hili lipo siku zote hata wabunge wenzangu wengine huwa wananiuliza namna ninavyopendwa na wananchi wangu.”

Masonga pia alikana kutamka maneno hayo popote huku akidai kwamba siku ya mkutano huo hakuwepo.

Wakili Kibatala alimuuliza Masonga kwamba ni lini na wapi hakushiriki mkutano huo, na Masonga alijibu, “Kwa sababu sio lazima mimi kushiriki ila taarifa zake nilikuwa nazo kwani ni utaratibu kwamba lazima ofisi yangu itambue hilo. Na siku yenyewe mimi nilikuwa ofisini asubuhi na saa saba mchana nilipigiwa simu kutoka nyumbani kwamba mke wangu anaumwa hivyo nikaondoka kulelekea nyumbani kwangu.”

Baada ya utetezi huo, hakimu Mteite aliiahirisha kesi hiyo hadi leo, huku wakili Kibitala akiiambia Mahakama kwamba Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Mpinga na RCO, wataanza kutoa ushahidi upande wa utetezi.