Wakili Kibatala awasili Mbeya

Muktasari:

Sugu na Masonga wanakabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli ambayo wanadaiwa kuitoa Desemba 30 mwaka jana

Mbeya. Wakili Peter Kibatala amefika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa ajili ya kuwawakilisha mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za juu Kusini, Emmanuel Masonga.

Sugu na Masonga wanakabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli ambayo wanadaiwa kuitoa Desemba 30 mwaka jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge.

Kibatala amewasili jijini hapa leo asubuhi kwa ndege na anawatetea Sugu na Masonga baada ya mawakili wao wa awali, Boniface Mwakubusi, Sabina Yongo na Hekima Mwasipu kujitoa katika kesi hiyo.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa Sugu na Masonga kuanza kutoa utetezi wao chini ya wakili wao mpya Kibatala.

 

Hata hivyo, wakati watu wakiwa ndani ya chumba cha Mahakama hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande ameingia na kuwaambia kesi hiyo itaanza saa tano kamili leo.

 

“Msione kimya hadi sasa, kesi itaanza saa tano, hivyo mnaweza kwenda kupumzika kwanza badala ya kuendelea kukaa tu humu ndani,” amesema Pande.