Mwanamke anayefundisha akiwa kitandani kwa miaka 18

Muktasari:

Kwa Joyce kitanda ndiyo maisha yake kwani tangu mwaka 1999 amejikuta karibu saa 23 anazitumia hapo. Anafanya kila kitu hapo kutokana na ulemavu alionao, lakini viungo vyote vya juu ya mwili vinafanya kazi ipasavyo.

Unapolalamika maisha magumu unatumia vigezo vipi? Soma simulizi hii ya Joyce Kantande kutoka kitandani. Wangapi hulalamika kuwa akilala muda mrefu anajisikia kuchoka au kuumwa? Umeshawahi kufikiria ugumu wa kulala kitandani kwa muda wa siku tatu mfululizo?

Kwa Joyce kitanda ndiyo maisha yake kwani tangu mwaka 1999 amejikuta karibu saa 23 anazitumia hapo. Anafanya kila kitu hapo kutokana na ulemavu alionao, lakini viungo vyote vya juu ya mwili vinafanya kazi ipasavyo.

Kinachomtofautisha Joyce na walemavu wengine ni ujasiri wake. Kwa kuwa alijua urafiki wake na kitanda utakuwa wa kudumu, alifikiria atakavyoweza kujikomboa kutoka hapo.

“Nilidhani ningekufa mwaka 1998 baada ya miguu yangu kugoma kabisa kutembea na kunilazimu kulala wakati wote. Nilijisemea moyoni natamani nife haraka ili nikimbie kadhia hii.”

Anaanza kusimulia Joyce huku mbele ya kitanda chake kukiwa na viti viwili viwili vilivyokaliwa na wanafunzi anaowatambulisha kwa majina ya Launack Ally na Godson John.

Mkasa wake unaanzia mwaka 1979 alipopata ajali ya gari ambayo ilichukua uhai wa mdogo wake na yeye kumuachia majeraha mgongoni.

Wakati huo akiwa binti wa miaka minane tu alitibiwa baada ya kugundulika kuwa aliteguka chini ya kiuno lakini kadri siku zilivyokwenda mbele maumivu yaliongezeka.

“Nilipata ajali wakati nikiwa shule ya msingi, nilitibiwa na kuendelea na masomo lakini maumivu hayakupungua ingawa hayakuwa makubwa sana kiasi cha kuleta hofu katika familia,” anasema.

Baadaye iligundulika kuwa pingili ziliachana isipokuwa zilipoanza kuungana ulijitokeza uvimbe ambao taratibu ulianza kusababisha mawasiliano katika mwili yasiwe mazuri.

Aliendelea na masomo ya sekondari na kumaliza kidato cha nne na baadaye kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano na sita katika Shule ya Wasichana Kilakala.

“Kutokana na maumivu na kuwa katika matibabu wakati wote ilibidi nihamishiwe Shule ya Sekondari Jangwani na baada ya hapo nilijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), hata hivyo nikiwa nimebakiza miezi miwili kuhitimu niliondolewa kutokana na kuzidiwa na maumivu.”

Maumivu na kuondolewa jeshini hakukuzima ndoto yake ya kutaka kujiendeleza kwani baada ya hapo alijiunga na Chuo cha Uhasibu Mbeya na kusomea masuala ya utunzaji stoo.

Alipohitimu ngazi ya cheti alirejea jijini Dar es Salaam akiwa na ndoto ya kutafuta kazi, lakini maumivu nayo hayakumuacha na safari hii miguu ikaanza kuwa mizito.

Taratibu ndoto za kufanya kazi zikaanza kufutika, badala ya kutumia muda mwingi kutafuta kazi aliumalizia hospitali kutafuta tiba. Siku zilivyozidi kwenda miguu ikamkatalia kuinuka, akajikuta amekwama kitandani.

Kwenda msalani, hospitali au kuzungumza na watu nje ya chumba chake aliihitaji usaidizi wa mtu kumfikisha huko. Kilichobaki kufanya kazi katika mwili wake ambacho angeweza kukiagiza kwa akili yake ni mikono, shingo, macho, mdomo na labda kuuzungushwa mwili wake kwa kubingirika… kinyume na hapo hakuna kiungo ambacho kingemtii.

“Mwanzoni maisha yalikuwa magumu kwa kuwa sikukubali sasa Joyce nimekuwa mlemavu. Nilitamani kufa baada ya kugundua kuwa nisingepona tena. Sikuyaona maisha yangu baada ya kupata ulemavu.”

Alianzaje kufundisha

Alianza kama sehemu ya kupoteza mawazo kwa kucheza na watoto chumbani kwake. Watoto wa ndugu na marafiki walifurika chumbani kwake kucheza naye ndipo jirani yake mmoja akamshauri kufungua darasa kutokana na maelewano yake na watoto.

Anasema wakati huo alikuwa akiishi Mwananyamala jijini Dar es Salaam katika nyumba ya kupanga kwa hiyo ndani ya chumba chake cha kulala ndimo lilimokuwa darasa.

“Jirani yangu nadhani aliona nimechukua jukumu la ulezi wa watoto bila malipo na kunishauri nifungue darasa. Wazazi wa wale watoto wa majirani zangu kwa moyo mkunjufu walikubali, nilianza taratibu na mwisho habari zangu zikaenea.”

Baada ya muda ikawa siyo tu anawafundisha watoto wa chekechea kwani jioni alianza kufundisha masomo ya jioni kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Maisha yamekuwa hivyo kwa miaka 18 sasa. Ukifika maeneo ya Ubena Mtaa wa Majumba Manne, Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam ukiulizia Mwalimu Joyce huwezi kupotea.

Anasema mwaka 2008 alihamia, Gongo la Mboto baada ya mama yake mzazi aliyekuwa mwalimu kustaafu na hivyo ikabidi aanze upya kutafuta wanafunzi katika maeneo hayo.

“Nashukuru Mungu kwa baraka zake huku walinipokea vizuri na nimekuwa nikipata wanafunzi si haba kwani angalau kwa mwaka watoto 50 wanaweza kupita katika mikono yangu,” anasema.

Anafundishaje?

Ndani ya nyumba anayoishi kuna chumba na sebule, kitanda chake amekisogeza karibu na mlango wa sebuleni naye hujilaza hapo wakati akiwafundisha wanafunzi waliopo sebuleni.

Pembeni ya kitanda chake kuna feni na viti viwili vya watoto, huwaita mmoja mmoja na kumfundisha kile kinachohitajika kwa siku hiyo, kwa mfano kushika kalamu, kuchora au kuunda maneno. Akiwa kitandani hapo anawafundisha kuimba, kucheza na kusoma kwa pamoja.

“Siku za Jumamosi na Jumapili huwa ndefu, hawa watoto ndio maisha yangu. Wananifariji na kunifanya niendelee kuishi. Sijioni nikiendelea kuishi bila kuwa na hawa watoto, wameifanya miaka 18 bila miguu kuwa yenye maana,” anasema.

Anasema kwa muda huo wa miaka 18 amekuwa akifundisha kuanzia saa 3.00 asubuhi na kuendelea kulingana na wingi wa watoto.

Hata hivyo, kwa watoto wa chekechea hakuna darasa ambalo linadumu kwa zaidi ya saa tatu kwa kuwa hawezi kuwahudumia muda mrefu.

“Watoto huwa wanakuja na vyakula kutoka nyumbani kwao, hapa wanasoma, wanacheza na muda wa mapumziko wanakula vyakula walivyokuja nao,” anaeleza.

Kwa wanafunzi wa masomo ya ziada huanza masomo yao jioni wakishatoka shuleni, ninakaa nao mpaka saa 12.00 au saa 1.00 jioni.”

Anasema anafurahi kuwafundisha na kwamba anajivunia kuwa baadhi ya waliopita mikononi mwake sasa hivi wengine wapo vyuo vikuu na wengine wameajiriwa.

Walemavu waache kuwa ombaomba

Joyce anasema kila mlemavu ana nguvu mahali fulani iwapo ataamua kuitafuta na kuitumia vilivyo ili kuepuka kuwa omba omba maisha yako yote.

“Mtu anaweza kuwa ombaomba kwa kuwa hajui pakuanzia, nashauri waombe kwa mipango, yaani awe anatafuta mtaji halafu aondoke barabarani na akazalishe mahali fulani,” anasema.

Anasema ingawa kwa miaka 18 amefundisha bado fedha anayopata imemwezesha kupata mlo na mahitaji madogomadogo lakini angetamani kuwa na shule yake.

Bado ana ndoto ya kumiliki shule na kuajiri Watanzania wengine: “Ninatamani sana kuanzisha shule, niwe na wanafunzi wengi zaidi na nitoe ajira kwa wenzangu,” anafafanua.

Ugumu anaokutana nao

Pamoja na kujitahidi Joyce anashindwa kufanya vitu vingi kama vile kuwahudumia watoto kwa mambo mengine ndiyo maana hata madarasa yake hudumu kwa saa tatu tu.

“Ninapenda kukaa muda mrefu na watoto lakini inabidi niwaruhusu mapema kwa kuwa baada ya saa tatu mtoto atataka kujisaidia, kula au kufanya kitu chochote kilicho nje ya uwezo wangu,” anasema.

Ugumu anaoupata ni pamoja na kuwahudumia watoto pale inapotokea kwa bahati mbaya amejisaidia au kutapika akiwa mgonjwa na kwamba hulazimika kumuita ndugu yake amsaidie kumsafisha.

Msaada anaohitaji

“Nahitaji kiti cha magurudumu (wheelchair) ili niweze kutembea angalau kuwapunguzia mzigo wa kunibeba ndugu zangu pale ninapohitajika kubebwa,” anasema.

Anasema tangu miguu ilipokataa kutembea hajawahi kutoka kwa matembezi ya kawaida isipokuwa anapokuwa mgonjwa au kufuatilia jambo lolote la muhimu.

Kuna wakati huwa analazimika kukodi kiti hicho pale anapotaka kutoka nyumbani kwaajili ya matibabu ili kuwapunguzia ndugu zake mzigo wa kumbeba.

Pia, anasema kutokana na hali yake anahitaji msaada ili ajenge choo anachoweza kukitumia tofauti na sasa.

“Sipendi kusema hivi lakini kutokana na hali yangu inabidi wakati mwingine nitumie mipira maalumu ya kujisaidia kwa sababu nahitaji kuwa na choo maalumu.”

Ili kuiendeleza shule yake ya chekechea aliyoipa jina la Amani Nursery School anasema zaidi anahitaji choo kwaajili ya watoto ili angalau waweze kukaa muda mrefu zaidi.

“Kwa watoto wanaosoma masomo ya jioni sina tatizo nao, wengi ni wakubwa wanaweza kujihudumia wenyewe, tatizo ni hawa wadogo,” anaeleza.

Umeguswa na mkasa wa Joyce na ungependa kumsaidia, wasiliana naye kwa simu 0654323341.