VIDEO: Profesa Ndulu aagwa rasmi Ikulu

RAIS MAGUFULI ATENGA SH BIL 200 KUWALIPA WANAOIDAI SERIKALI

Muktasari:

Baada ya mazungumzo yao, Prof. Ndulu amemshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kufanya naye kazi tangu alipoingia madarakani na amebainisha kuwa anafurahi kumaliza kipindi chake huku uchumi wa nchi ukiwa mzuri.

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli, leo Januari 3 ameagana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) anayemaliza muda wake Prof. Benno Ndulu Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo yao, Prof. Ndulu amemshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kufanya naye kazi tangu alipoingia madarakani na amebainisha kuwa anafurahi kumaliza kipindi chake huku uchumi wa nchi ukiwa mzuri.

Prof. Ndulu amempongeza  Rais Magufuli kwa miongozo muhimu iliyosaidia kuimarisha uchumi ikiwemo kudhibiti mfumuko wa bei ambao  Novemba 2017 ulifikia asilimia 4.4 na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani  1.8bilioni  hadi kufikia Dola za Marekani 6 bilioni  hivi sasa, hali ambayo imeimarisha uwezo wa Serikali kujiendesha na kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo.

“Nimekuja kumuaga  Rais na kumshukuru, nafurahi kuwa naondoka wakati hali ya uchumi ikiwa nzuri, Taifa linakopesheka na kuna mazingira mazuri zaidi ya uchumi kuendelea kukua, nampongeza  Rais kwa kusimamia mambo mbalimbali muhimu ya kuimarisha na kukuza uchumi katika kipindi chote nilichofanya naye kazi”  amesema  Prof. Ndulu.

Pia  Gavana Mteule Prof. Florens Luoga amemshukuru  Rais Magufuli kwa uteuzi huo na kumhakikishia kuwa ataisimamia BOT ili iendelee kuwa chombo imara cha kusimamia uchumi wa nchi.

Pia ameahidi kusimamia fedha za Tanzania na kuhakikisha nchi inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na mradi wa umeme katika maporomoko ya maji ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).

Prof. Luoga ameungana na Prof. Ndulu kueleza kuwa taarifa zinazotolewa na BOT kuhusu ukuaji wa uchumi zinaandaliwa kitaalamu na kwa kushirikisha vyombo mbalimbali vikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na ameonya dhidi ya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipotosha ukweli kuhusu takwimu za uchumi zinazotolewa na BOT.

 Rais Magufuli amempongeza Prof. Ndulu kwa utumishi wake wa miaka 10 na kazi nzuri aliyoifanya kusimamia uchumi ambapo katika kipindi hicho kasi ya ukuaji wa uchumi imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 5 hadi kufikia asilimia 7.

Amesema kwamba Profesa Ndulu  ameimarisha usimamizi wa benki na maduka ya kubadilishia fedha, amesimamia ongezeko la akiba ya fedha za kigeni inayoiwezesha nchi kumudu kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi 6 na kuanza kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa reli, umeme, ununuzi wa ndege na mingine.