Mawe yenye madini yawapeleka rumande watu sita

Muktasari:

Yalikuwa kwenye visanduku au matenga 370 ya mbao yanayofanana na ya kusafirishia nyanya.

Shinyanga. Watu sita wakiwemo raia wanne wa China wanashikiliwa na polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kusafirisha shehena ya mawe yanayoaminika kuwa ni madini bila leseni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule amesema raia hao wa China na Watanzania wawili walikamatwa jana Jumatano Desemba 6,2017 wakisafirisha madini hayo yakiwa yamehifadhiwa katika visanduku au matenga 370 ya mbao yanayofanana na ya kusafirishia nyanya.

Amewataja wanaoshikiliwa kwa mahojiano kuwa ni Bai Tao, Chen Dunlu, Huanran Liu na Jianhua Xiong ambao ni raia wa China.

Wengine ni Watanzania Anwar Shaaban na Joseph Kapooi ambao ni madereva wa magari yaliyotumika kusafirisha shehena hiyo.

"Katika mahojiano ya awali, watuhumiwa walisema bidhaa hiyo ilikuwa ikipelekwa katika kiwanda cha mafuta ya kula cha Jielong kilichopo mjini Shinyanga," amesema Kamanda Haule leo Alhamisi Desemba 7,2017.

Amesema uchunguzi wa polisi kiwandani hapo umebaini kuwepo masanduku mengine 2,730 yaliyosheheni mawe yanayoaminika kuwa ni madini yakiwa yamehifadhiwa.

“Tunaendelea kuwashikilia kwa uchunguzi ili kujua aina ya madini hayo," amesema.

Katika mahojiano ya awali, amesema watuhumiwa wameshindwa kuonyesha vibali vya kuwaruhusu kumiliki na kuhifadhi madini hayo kiwandani.

Polisi pia inachunguza ni wapi mawe hayo yanayoaminika kuwa ni madini yalikopatikana au kuchimbwa.

Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati Magharibi, Hamisi Kamando amesema kuna uwezekano mkubwa wa  mawe hayo kuwa na madini ya thamani ingawa hawezi kutaja ni aina gani hadi uchunguzi wa kimaabara ufanyike.

Amesema kitendo cha watuhumiwa hao kukutwa na mawe hayo bila kuwa na leseni wala kibali cha kujihusisha na biashara ya madini ni kinyume cha kifungu cha 6 cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017.