Siri iliyojificha kwenye nazi, muhogo na karanga mbichi

Muktasari:

  • Kama jibu pia ni ndiyo, basi ukae ukijua kuwa bidhaa hizo sasa ndiyo habari ya mjini kwani muhogo, karanga mbichi na nazi vinatajwa kuwa vyakula vya kuongeza urijali na kulinda heshima ya baba nyumbani.

Umewahi kukaa kwenye foleni? Kama jibu ni ndiyo, je, umewahi kuwaona kina mama wanaouza nazi, muhogo na karanga mbichi katika mabeseni?

Kama jibu pia ni ndiyo, basi ukae ukijua kuwa bidhaa hizo sasa ndiyo habari ya mjini kwani muhogo, karanga mbichi na nazi vinatajwa kuwa vyakula vya kuongeza urijali na kulinda heshima ya baba nyumbani.

Ni kawaida siku hizi kuwaona kina mama wakiwa wamebeba mabeseni yaliyojaa, muhogo, nazi na karanga. Muhogo huwa umesafishwa vizuri huku gamba la juu likiachwa, lakini likikwaruzwa na kusafishwa hadi kuwa jeupe.

Karanga hufungwa kwenye vifuko vya plastiki na nazi (mbata) hukatwa vipande vidogo vidogo na kufungwa katika vifuko pia.

Muuzaji aghalabu hutembea na kisu chake kwa ajili ya kukata muhogo kwa sababu, kuna kipande cha Sh100, 200 hadi cha 500. Karanga mbichi huuzwa Sh200 kwa pakiti na nazi ni Sh100 kwa pakiti.

Wauzaji hawa ambao wengi wao ni wanawake, hutega wateja wao katika foleni za magari ambako madereva wa daladala na wanaume wengine wengi walio kwenye magari hununua kwa wingi bidhaa hizo.

Kadhalika, wanaume wenye biashara zao katika masoko makubwa kama Kariakoo, Tandika au Buguruni nao huichangamkia mihogo, karanga na nazi.

Lakini, swali ni kwa nini bidhaa hizi huuzwa kwa pamoja na kwa nini zinapendwa zaidi na wanaume?

Mwandishi wetu aliwatafuta wauzaji hao, ambao walikuwa wametingwa kuuza bidhaa zao katikati ya magari yaliyo kwenye foleni yakielekea Buguruni.

Akiwa amebeba beseni lake lililosheheni bidhaa hizo kichwani, Magdalena Mwombeki, alisema anauza karanga mbichi na mihogo kwa sababu ni vitu ambavyo wanaume wamekuwa wakivikimbilia kwa wingi.

“Zamani nilikuwa nauza matunda na muhogo mibichi, lakini wateja wakawa wanaulizia na karanga na nazi, nikaamua kuanza kuuza hivyo tu na kwa kweli vina wateja,” alisema.

Alisema baada ya kuanza kuuza kwa wingi aligundua wanaume wanapenda zaidi bidhaa hizo kwa sababu zinaongeza hamu na nguvu ya tendo la ndoa, “Wanaponiita wakitaka kununua, wanasema hebu tuletee karanga hizo tuongeze heshima ya ndoa.”

Alisema baadaye wateja wake wengi wakawa wanaulizia nazi na ndipo akaanza kuziuza lakini alisema anaikata vipande vidogo vidogo na kuvifunga katika mifuko ya plastiki.

Muuzaji mwingine, Shyrose Kamunguye alisema sasa hivi wanawake wengi wameacha kuuza matunda na wamekimbilia kuuza karanga mbichi, muhogo na nazi kutokana na wanunuzi wa bidhaa hizo kuwa wengi.

“Hata nikijaza matango na maembe kwenye beseni bado wateja wanaulizia muhogo mbichi na karanga na hawa wa nazi nao wanakuja kwa kasi sasa,” alisema.

Mtaalamu wa chakula na lishe katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Pazi Mwinyimvua alisema manufaa ya muhogo, nazi na karanga yameibuliwa na ujuzi wa asili.

“Binadamu mwenyewe amekula vitu hivi na akaona faida zake ndiyo maana unaona vinahitajika kwa wingi na wanaume. Ni ajabu kuona wengine wanakanusha kuwa vyakula hivi vinaongeza nguvu wakati hata sayansi inaonyesha hivyo,” alisema.

Alisema kwa mfano karanga, ina wingi wa protini na inazalisha seli nyingi kwa hali ya kawaida anayekula lazima atazalisha pia manii kwa wingi. “Kwa upande wa muhogo huu una wanga na nishati kubwa kwa hiyo ukila unakusaidia kukupa nguvu na joto na mtu ambaye hajala na hana nishati, hawezi kuwa imara katika tendo la ndoa,” alisema.

Mwinyimvua alisema nazi nayo ni muhimu zaidi kwa sababu ina protini na mafuta na yote kwa pamoja husaidia kuufanya mzunguko wa damu uende sawasawa, hivyo kumfanya mwanamume apate hamu ya tendo la ndoa na pia kuwa na nguvu zaidi.

“Hatuhitaji hata maabara kupima umuhimu wa muhogo, nazi na karanga katika kuongeza nguvu za kiume. Kwa sababu nguvu za kiume siyo miujiza ni namna unavyoishi na kile unachokula,” alisema.

Daktari wa uchunguzi wa magonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Innocent Mosha alisema vyakula hivyo vinaongeza wingi wa mbegu za kiume kwa sababu vina mafuta na protini kwa wingi.

“Mafuta na protini vinazalisha seli na hivyo manii kuwa mengi. Kwa kifupi, hivi huweza kuongeza hamu ya tendo la ndoa, lakini kwa nguvu za kiume nadhani ni kwa sababu vyakula hivyo huongeza nguvu mwilini,” alisema.

Utafiti wa Mpemba

Mwandishi wetu pia alizungumza na Abeid Sultan Ghassani (81), mkazi wa Mjini Magharibi, Zanzibar ambaye kwa sasa anaishi Dar es Salaam.

Ghassani alisema wengi hawajui kuwa ili kuwa na nguvu za kiume huna haja ya kutumia dawa za hospitali, bali vyakula vya asili.

Ghassani ambaye ana wake watatu, alijisifu kuwa mpaka sasa ana nguvu za kutosha kwa kuwa katika maisha yake amekuwa akila muhogo, karanga, nazi na samaki vibua.

“Tunakula vyakula vya asili vilivyotoka shambani, muhogo mbichi na kila kitu hakijawekwa kemikali, kwa nini nisiwe imara kama simba?” alisema