Wapinzani kuendeleza maandamano Kenya

Muktasari:

  • Wapinzani wakuu wamedai hawajaridhishwa na uchaguzi huo tangu awali kwani ulikumbwa na wizi wa kura ambazo zilimpatia Uhuru Kenyatta ushindi

Muungano Mkuu wa Upinzani Nchini Kenya, ambao umeshindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, umeapa kuendelea na maandamano yenye nia ya kubatilisha kile ambacho wanachodai kuwa, matokeo "feki" ya uchaguzi mkuu.

Raila Odinga, amedai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na wizi mkubwa wa kura.

Seneta James Orengo ameliambia Shirika la Habari la   BBC kuwa chama chake, kinachoongozwa na Raila Odinga, hakitapinga matokeo ya uchaguzi mkuu mahakamani, huku akisema kuwa Uhuru Kenyatta tayari ametoa vitisho kwa majaji.

Mpaka  sasa watu 11 wameuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi mkuu, ambazo zilianza mara baada ya Uhuru Kenyatta kushinda na  kutangazwa mshindi kwa muhula wa pili mnamo usiku wa kuamkia Jumamosi.

Tume ya taifa ya kutetea haki za kibinadamu nchini Kenya, imetoa orodha ya juu ya waathiriwa wa ghasia hizo huku ikisema kuwa ni watu 24 ndio ambao wameuwawa katika visa vinavyohusiwa na uchaguzi huo, huku ikiongeza kuwa polisi wanatumia nguvu kupita kiasi.