Sudan Kusini imewakatisha tamaa Waafrika kama Zuma

Muktasari:

  • Kati ya wote nilikuwa karibu zaidi na waandishi kutoka Sudan, Charles Ruganya Ronyo kutoka Juba na Abdelshafii Abdallah kutoka Khartoum.

Mwaka 2007 nikiwa kwenye mafunzo ya uandishi wa habari nchini Ujerumani, nilikutana na waandishi wengine kutoka, Zambia, Vietnam, Zimbabwe, Sudan, India, Mauritania na Laos.

Kati ya wote nilikuwa karibu zaidi na waandishi kutoka Sudan, Charles Ruganya Ronyo kutoka Juba na Abdelshafii Abdallah kutoka Khartoum.

Wasudani hawa wakati huo nchi yao ikiwa moja walikuwa wakifanya mambo yao pamoja, dukani (supermarket) wataenda pamoja, watapika pamoja, kula pamoja na mambo mengine.

Pamoja na ukaribu wao hali ilikuwa mbaya walipoanza kujadili mambo ya nchi yao, Charles alikuwa akiulaumu utawala wa Omar al Bashir kwa ubaguzi na kutowajali Wasudan walio Kusini jambo ambalo Abdelshafii alilipinga.

Mijadala yao ilifikia kutoleana lugha za ukali kiasi kwamba wakati mwingine waliacha kuzungumza Kiingereza na kuzungumza Kiarabu, mwisho wakanuniana, umoja wao ukatoweka, kila mmoja akawa anapika chumbani kwake na hata kuongozana ikawa ni mara chache.

Hoja kuu ya Charles ilikuwa ni kutaka nchi hizo zigawanywe kwani watu wa Kusini walichoka kunyanywaswa na utawala wa Al Bashir huku akidai Kusini kuna rasilimali nyingi lakini watu wake ni masikini na hata kwenye michezo wanabaguliwa, vijana wenye vipaji hawapewi nafasi.

Mwaka 2011 ilipoamuliwa Sudan Kusini iwe nchi huru na kujitenga na Sudan (Kaskazini) nilijiambia kwamba ndoto za watu wa Kusini zimetimia na tutarajie maendeleo baada ya kuipigania nchi yao kwa miaka mingi.

Hata hivyo, kilichotokea ni tofauti, hali Sudan Kusini ni ya hovyo, vita vya wenyewe kwa wenyewe vimeshika hatamu, ni kama vile Wasudani Kusini walipigania kujitenga ili wapate uhuru wa kupambana wao kwa wao na hata kuuana, hicho ndicho kinachoendelea sasa Sudan Kusini.

Awali waliona wanabaguliwa, wakataka kuwa na taifa lao, baada ya kupewa taifa lao mwaka 2011, mwaka 2013 wakaanza kupambana wao kwa wao kwa misingi ya kikabila na uchu wa madaraka.

Nchi hii yenye watu wasiozidi milioni 13, iliingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe baada ya Rais Salva Kiir ambaye kiasili ni wa kabila la dinka kutofautiana na aliyekuwa makamu wake, Riek Machar wa kabila la neuer.

Ugomvi wa watu hawa ambao iliaminika kwamba umoja wao ungekuwa silaha ya kuikomboa Sudan Kusini chanzo chake ni uchu wa madaraka huku ukabila nao ukiwa na nafasi yake, walitibuana baada ya kuibuka madai kwamba Machar alikuwa akijipanga kumpindua Salva Kiir katika urais.

Kuanzia hapo wamekuwa wakipambana, inasadikiwa tangu nchi hiyo iingie katika vita vya wenyewe kwa wenyewe wananchi wapatao 300,000 wamepoteza maisha wakiwamo waliouawa katika Mauaji ya Bentiu ya mwaka 2014 ambayo yalitokea katika mji wa Bentiu na kusababisha vifo vya watu 400. Hadi sasa haijulikani nani aliyehusika katika mauaji hayo ya raia wasio na hatia, upande wa Serikali unaulaumu upande wa Machar ambao pia umepinga kuhusika kwa namna yoyote.

Zipo habari kwamba mmoja wa viongozi aliyehusika na mauaji hayo aliwaonya watu ambao si wa kabila la Nuer, kauli iliyowafanya wananchi kukimbilia kwenye nyumba za ibada ili kujinusuru lakini walifuatwa huko huko wakauliwa huku wanawake wakibakwa na kuteswa kabla ya kuuliwa.

Rekodi kwa ujumla zinaonyesha kwamba wananchi milioni 3 waliyahama makazi yao kwa hofu ya kuuliwa, kati yao milioni mbili wanaishi kwenye makambi na wengine milioni moja wamehamia nchi jirani za Kenya, Sudan na Uganda.

Hao ni Sudan Kusini ambao wameipigania nchi yao kwa nguvu zote ikiwamo kulalamika kwenye jumuiya za kimataifa lakini baada ya kuipata wakaanza kupambana wao kwa wao huku matatizo ya wananchi wao yakiongezeka, umasikini, maradhi, njaa na mengineyo vimetamalaki. Ilitarajiwa uhuru wa mwaka 2011 ungewafanya wawe kitu kimoja lakini uhuru huo ni kama imekuwa sababu ya wao kutengana.

Kwa mtu kama Donald Trump ambaye anachukizwa na Afrika, kilichotokea Sudan Kusini anaweza kukitafsiri kwamba kinaakisi hoja yake ya kwamba Waafrika ni watu wa kutawaliwa, hawajawa tayari kujitawala wenyewe.

Vyovyote itakavyokuwa kama kuna tatizo katika nchi nyingi za Afrika basi tatizo hilo ni mtu wa kuwa kiongozi. Viongozi wa Afrika kama ukiamua kuiangazia Sudan Kusini unaweza kusema kwamba Trump alikuwa sahihi, hajakosea hata kidogo.

Viongozi wanaoangalia watu wao 300,000 wakifa kwa sababu ambazo wangeweza kuzizuia ni kwanini mtu wa nje asitilie shaka uwezo wa watu hao kujitawala? Tena viongozi ambao walikuwa wamoja wakitaka nchi yao baada ya kuona wanabaguliwa.

Unapoishangaa Sudan Kusini iangalie na Afrika Kusini, nchi ambayo ipo katika kundi maarufu la G Five linalojumuisha mataifa ambayo uchumi wao unakuwa vizuri, nchi nyingine ni Mexico, India, China na Brazil.

Baada ya Nelson Mandela kung’atuka mwaka 1999, Thabo Mbeki akachukua madaraka, uongozi wa Mbeki ulitawaliwa na mgogoro kati yake na aliyekuwa makamu wake Jacob Zuma.

Mgogoro huo ulikuwa mkubwa hadi Mbeki kumtimua Zuma kwa tuhuma za rushwa lakini Zuma alishinda mahakamani kabla ya kibao kumgeukia Mbeki ambaye alijiuzulu baada ya kukosa kuungwa mkono ndani ya chama chake ANC ambacho hata bungeni, wabunge wake hawakuwa wakimuunga mkono.

Wakati Mbeki akiandamwa kabla ya kujiuzulu mwenyewe mwaka 2008, wananchi wengi Afrika Kusini waliamini Zuma ndio kila kitu, fulana za kumuunga mkono Zuma zilivaliwa kwa wingi katika mikutano na hafla mbalimbali za ANC. Kung’oka kwa Mbeki ikawa mwanzo mpya wa Zuma kutawala Afrika Kusini.

Kama ilivyo kwa Mbeki, Zuma naye kabla ya kuwa rais alikuwa mwanaharakati aliyepambana kupiga vita ubaguzi wa rangi hadi kufikia hatua ya kuishi uhamishoni nchini Msumbiji hivyo kuingia kwake madarakani wananchi wengi wa Afrika Kusini waliamini wamempata rais mzalendo wa kweli huku wengine wakimtaja kwa jina la Rais wa Watu au People’s President.

Imani ya wananchi wengi ilikuwa kubwa kwa Zuma kwa sababu kama ilivyo kwa kipenzi chao, Nelson Mandela, Zuma naye aliwahi kufungwa Robben Island kwa miaka 10, jela ambayo Mandela alifungwa kwa miaka 27. Yote hayo yalitosha kuibua matumaini ya Peoples President na hivyo kung’oka kwa Mbeki haikuwa tatizo kwa wananchi wa Afrika Kusini hasa weusi.

Hata hivyo hali ikawa tofauti, Zuma hakuwa yule waliyemfikiria, akaanza kuingia katika kashfa za rushwa na matumizi mabaya ya ofisi.

Mwaka jana mahakama ya juu nchini Afrika Kusini ilifikia uamuzi wa Zuma kushitakiwa kwa makosa ya rushwa ikiwamo kashfa ya biashara ya silaha ya mwaka 1999.

Sambamba na hilo, Zuma pia anahusishwa na familia ya tajiri Gupta ambaye inadaiwa kwamba kwa kumtumia Zuma familia hiyo iliiweka mfukoni Serikali ya Afrika Kusini.

Kati ya kashfa nyingi za rushwa na matumizi mabaya ya ofisi zinazomuandama Zuma, iliyozungumzwa zaidi ni ile ya kutumia dola 15 milioni zaidi ya Sh 33 bilioni za Kitanzania kukarabati nyumba yake binafsi.

Ikumbukwe kwamba pamoja na Afrika Kusini kuwa ni nchi tajiri lakini wapo wananchi masikini wa kutupwa hivyo kwa kiongozi kutumia kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa matumizi binafsi ambayo hayakuwa na ulazima ni sawa na dhihaka kwa wananchi masikini hasa kwa mtu ambaye walijiaminisha kwamba angekuwa mkombozi wao.

Na ingawa alitakiwa kurudisha sehemu ya fedha hizo na mahakama, bado kashfa hiyo ilimtia doa kubwa Zuma na hivyo anaondoka akiwa anaingia katika orodha ya viongozi wa Afrika wanaoondoka madarakani kwa kashfa tofauti na matarajio ya awali.

Zuma ambaye inadaiwa ni baba wa watoto zaidi ya 20 ni dhahiri amewakatisha tamaa wananchi wa Afrika Kusini waliokuwa na matumaini naye, ni hivyo hivyo kwa Salva Kiir amewakatisha tamaa wananchi wa Sudan Kusini, matumaini makubwa waliyokuwa nayo kwa viongozi hao yamekuwa kinyume.