UCHAMBUZI: Afcon hii ya 2019, ukweli Tanzania washindwe wenyewe tu

Dk Mshindo Msolla

Muktasari:

  • Kiwango kilichoonyeshwa na Stars wakati ikicheza na Uganda na moyo wa kujitolea, kucheza kwa nguvu moja muda wote wa mchezo na kwa nidhamu ya hali ya juu, kilionyesha kwamba Tanzania tunaweza kufuzu.

Tanzania ilikuwa na mchezo wa kuwania kufuzu kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ambazo zitafanyika Cameroon mwakani. Mpaka sasa Tanzania imecheza michezo miwili na kupata alama mbili baada ya kutoka sare na Lesotho na Uganda.

Kiwango kilichoonyeshwa na Stars wakati ikicheza na Uganda na moyo wa kujitolea, kucheza kwa nguvu moja muda wote wa mchezo na kwa nidhamu ya hali ya juu, kilionyesha kwamba Tanzania tunaweza kufuzu.

Aidha, kiwango hicho kilionyesha kwamba kama kocha atapata muda wa kutosha na wachezaji wakaendelea na juhudi walizozionyesha, Tanzania inaweza kufuzu kwa kufanya vizuri kwenye michezo iliyobaki dhidi ya Uganda, Lesotho na Cape Verde.

Pamoja na kujipa matumaini hayo, hesabu inaweza isiwe rahisi kama ambavyo tunafikiria kwa sababu mpira wa miguu una matokeo yasiyotegemewa kama maandalizi stahiki hayatafanyika.

Benchi la ufundi na wachezaji wamedhihirisha kwamba Tanzania tunao wachezaji mahiri ambao wakipewa nafasi na kuaminiwa, wanaweza wakafanya vizuri.

Mambo yafuatayo yanaweza kutupatia matokeo chanya kama yakitekelezwa ipasavyo:

Kocha aendelee kusimamia suala la nidhamu:

Msimamo imara aliouonyesha kocha kwa kuwaengua wachezaji saba waliochelewa kuripoti kambini ulionyesha ni kwa namna gani amejipambanua kuwa ni mtu mwenye msimamo thabiti.

Kuenguliwa kwa wachezaji hao kulileta mijadala mingi miongoni mwa wadau kwa sababu kwao halikuwa jambo la kawaida. Kiwango cha kujituma na kucheza kwa nidhamu ya kimchezo bila shaka kulichagizwa na msimamo wa kocha na kila mmoja aliyepewa nafasi aliitumia kikamilifu kumwonyesha kocha kwamba alistahili kuchaguliwa hii ikiwa ni pamoja na wale ambao waliteuliwa mara ya pili ambao walipata nafasi ya kucheza.

Kocha apewe muda wa kutosha wa maandalizi:

Nafahamu kanuni kwa wachezaji wanaocheza nje haziruhusu mchezaji kuitwa kambini kwa kipindi kirefu na hili nadhani ni sahihi kwa sababu utaratibu wa maisha za wachezaji wa kulipwa ni za kinidhamu zaidi ndani na nje ya kiwanja.

Pamoja na ukweli huo, wachezaji wanaocheza ligi za ndani wapewe muda wa maandalizi wa kutosha ili wanapokuja kujiunga na wale wanaocheza mpira wa kulipwa, watengeneze timu ya ushindi.

Nafahamu timu yetu kuwa kambini kwa kipindi kirefu kutasababisha ligi kusimama, lakini kwangu, kama wadau watafahamishwa sababu ya kufanya hivyo, kwamba ni mkakati wa Tanzania kufuzu kwenda Afcon, bila shaka wataunga mkono jitihada hizo kwa sababu itaondoa ile historia ya kuukumbuka mwaka wa 1980 tulipofuzu mara ya mwisho.

Nashauri, kama uwezekano upo, wapewe kambi hata nje ya nchi ambako watapata mazingira mazuri na hivyo kujiandaa.

Wachezaji na semina elekezi:

Hakuna jambo muhimu kama kuwaandaa wachezaji kisaikolojia ili watambue umuhimu wa mechi zilizobaki, kwamba lazima wabadilike na wajipange kwa matokeo ya ushindi na si vinginevyo. Hili linaweza kufanyika kwa kuwatafuta wataalamu wa saikolojia, wanasiasa wanamichezo, makocha waandamizi na wachezaji wa zamani.

Ninaamini kundi hilo likijipanga vizuri, linaweza kuamsha ari ya wachezaji wetu kupigania ushindi katika mazingira yoyote yale. Baada ya makundi hayo kuifanya kazi hiyo kikamilifu, waziri mwenye dhamana ya michezo pamoja na Waziri Mkuu ambaye ana taaluma ya ukocha, wanaweza kuongeza morali ya wachezaji kwa kuzungumza nao na kuwapa hamasa inayotakiwa.

Watanzania nao waendelee kuwapa hamasa.