Alichosema Jenerali Mabeyo tukiunge mkono

Muktasari:

  • Pia, Jenerali Mabeyo amewata maofisa hao wapya zaidi ya 400 kuzingatia, kuheshimu, kuthamini na kutunza kiapo cha utii ambacho kinalinda Sheria ya Ulinzi wa Taifa ambayo ndiyo imetoa kanuni mbalimbali zikiwamo za maisha ya kila siku ya mwanajeshi.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Mabeyo amewakumbusha maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliopata kamisheni jana kuwa kitendo hicho ni ishara ya kupewa dhamana ya uongozi.

Pia, Jenerali Mabeyo amewata maofisa hao wapya zaidi ya 400 kuzingatia, kuheshimu, kuthamini na kutunza kiapo cha utii ambacho kinalinda Sheria ya Ulinzi wa Taifa ambayo ndiyo imetoa kanuni mbalimbali zikiwamo za maisha ya kila siku ya mwanajeshi.

Aliwataka maofisa hao kuishi kanuni hizo kwa maana ya kuilinda nchi, watu na mali zao dhidi ya tishio lolote la nje na ndani ya nchi. Pia, alisisitiza kwamba wanajeshi hao wana wajibu wa kutii Katiba ya nchi na kumtii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumlinda.

Jenerali Mabeyo aliwataadharisha maofisa hao kwa kuwataka wakae mbali na mambo ya kisiasa, mitandao ya kijamii na waimarishe uhusiano mzuri na wananchi kwa kuwa hilo ndiyo jeshi lao.

Mbali na kutoa tahadhari hiyo kwa maofisa hao, pia aliwataka wananchi kuonyesha upendo na ushirikiano kwa askari hao ili kazi yao ya kulinda nchi, raia na mali zao ifanyike kwa ufanisi.

Kauli ya Jenerali Mabeyo imetokana na hali ya sasa ya kisiasa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii nchini. Nasi tunaiunga mkono tukisema inapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa pekee kwani ni ukweli kwamba kuna baadhi ya askari wamewahi kutuhimiwa kujihusisha na masuala ya siasa ilhali ni kinyume na kiapo cha utii ambacho wanatakiwa wakiishi.

Lakini, si hivyo tu matumizi ya mitandao ya kijamii nayo imekuwa ikitumiwa vibaya na baadhi ya watu wakiwamo wanajeshi kwa kupeana habari zenye upotoshaji au kuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.

Tunaamini Jenerali Mabeyo ameyasema hayo baada ya kujiridhisha kwamba baadhi ya askari wake wameonekana wakijihusisha na upotoshaji wa masuala ya kitaifa kupitia mitandao ya kijamii.

Siku zote wanajeshi wamekuwa msaada kwa wananchi pale yanapotokea maafa au shida fulani, mfano Jeshi linapokuwa kwenye maadhimisho ambayo hufanyika Septemba ya kila mwaka, wanajeshi hushiriki shughuli za kijamii ikiwamo kutoa huduma za afya bure kwa na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali.

Hivyo tunaamini wanajeshi wote wakiwamo waliopata kamisheni jana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, wakikiishi kiapo cha utii, amani tuliyonayo itaendelea kudumu kwa muda mrefu na hata haya matukio ya uhalifu yanayojaribu kujitokeza yanaweza yakawa historia kabisa.

Matumaini ya Watanzania yapo kwa jeshi lao, ndiyo maana likaitwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, hivyo kauli ya Jenerali Mabeyo imeongeza matumaini ya Watanzania kwa jeshi lao.

Jenerali Mabeyo ameonyesha dhahiri kwamba anataka kujenga jeshi lenye nidhamu, linalotii Katiba na vilevile utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwamo kumlinda, kuilinda nchi na kuwalinda wananchi na mali zao dhidi ya tishio la aina yoyote, liwe la nje au ndani ya nchi.

Tunasema ni wajibu kwa Watanzania kumuunga mkono Jenerali Mabeyo kwa kutoa ushirikiano kwa wanajeshi pale unapohitajika kwa madhumuni ya kujenga Taifa madhubuti, kiusalama na kimaendeleo.