Bajeti ya mwaka huu iguse maisha ya wananchi

Muktasari:

  • Wengi wanafuatilia kujua mwenendo wa kodi na ushuru wa bidhaa muhimu kama vile mafuta na chakula ambavyo kwa kiasi kikubwa vinagusa maisha yao ya kila siku, hasa wale wa maisha ya chini.

Hivi sasa Bunge la bajeti linaendelea na vikao vyake mjini Dodoma. Ilizoeleka kwamba ikifika kipindi kama hiki wananchi wanakuwa na shauku ya kufuatilia mijadala ya Bunge ili kufahamu bajeti yao ina mambo gani yanayowagusa moja kwa moja.

Wengi wanafuatilia kujua mwenendo wa kodi na ushuru wa bidhaa muhimu kama vile mafuta na chakula ambavyo kwa kiasi kikubwa vinagusa maisha yao ya kila siku, hasa wale wa maisha ya chini.

Utaratibu wa bajeti ni wa kibunge na unafanyika kuanzia kwenye vitengo, idara na wizara, kisha kuidhinishwa na Bunge kwa ajili ya utekelezaji. Bajeti ya nchi inatakiwa kuwa na sura ya kumsaidia mwananchi wa kawaida.

Mwaka wa fedha wa 2017/18, Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kuongeza fedha za maendeleo ambazo zililenga kusaidia miradi mbalimbali kwa wananchi katika maeneo mbalimbali.

Licha ya changamoto mbalimbali za utekelezaji wa bajeti, Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ununuzi wa ndege, ujenzi wa barabara za juu na mradi wa umeme wa Kinyerezi II.

Miradi yote hiyo ni muhimu kwa uchumi wa Taifa hili. Itachochea uzalishaji na kuleta matokeo chanya kwa wananchi hasa katika kipindi hiki ambacho dira ya Taifa ni kuwa nchi ya uchumi wa kati utakaotokana na viwanda.

Hata hivyo, sasa ni wakati wa kuwageukia wananchi ambao wanalalamika maisha yao yamekuwa magumu, vijana hawana ajira, uzalishaji wa mazao ya kilimo unasuasua na wafanyabiashara wanalia utitiri wa kodi.

Bajeti ya mwaka huu wa 2018/19 inatakiwa kutoa majibu ya changamoto hizi kwa kutafuta namna ya kuwasaidia wananchi ambao ndiyo walipakodi ili nao wajikwamue na ugumu wa maisha unaowakabili.

Iwe ni ajenda ya kila wizara kuhakikisha kwamba inatengeneza ajira za kutosha kwa ajili ya kupunguza idadi kubwa ya vijana ambao wanakaa mitaani bila ajira licha ya kwamba wana ujuzi na maarifa ya kufanya kazi.

Bajeti itoe unafuu kwa wakulima kwa kuwawezesha kupata pembejeo za kilimo kwa uhakika na gharama nafuu. Kumekuwa na urasimu mkubwa kwenye suala hili licha ya dhamira njema ya Serikali, watendaji waongeze usimamizi ili pembejeo hizo ziwafikie walengwa.

Suala la kodi nalo limekuwa mwiba mchungu kwa wafanyabiashara hasa wenye viwanda. Wengi wao wanalalamikia kutozwa kodi nyingi pamoja na tozo nyingine zinazotozwa na mamlaka mbalimbali za Serikali kama vile ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Ofisi ya Mkemia Mkuu au Shirika la Viwango (TBS).

Serikali ina jukumu la kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara ikiwemo kuunganisha huduma zinazotolewa na taasisi hizo kuwa chini ya mwavuli mmoja badala ya kuwafanya wafanyabiashara kuzunguka ofisi zote hizo kutafuta vibali au kulipia tozo mbalimbali.

Kadhalika, Serikali ina jukumu la kudhibiti mfumuko wa bei na kusaidia wananchi wake kupata mikopo ili waweze kuanzisha biashara au kujiajiri wenyewe kwenye shughuli mbalimbali za kijasiliamali.

Bajeti ni ya wananchi, ni muhimu wakaona inawapa unafuu wa maisha na kutatua changamoto zao. Bajeti haitakuwa na uwakilishi kama haitaakisi maisha ya Watanzania na kutoa majawabu kwa changamoto zao.

Ni wajibu wa kila mwananchi kulipa kodi kwa sababu Serikali inaendeshwa kwa kodi hizo. Serikali pia ina wajibu wa kutengeneza mazingira mazuri na wezeshi ya kukusanya kodi bila kuwaumiza walipakodi. 0763891422.