Bodaboda, magari ya abiria vijijini yanaumiza wananchi

Muktasari:

  • Gharama ni kubwa kuliko uhalisia na ukweli wa maisha ya Watanzania wa vijiji vya mikoa karibu yote, ikiwamo ya Rukwa, Katavi, Songwe, Njombe, Morogoro, Kagera na Manyara.

Nauli za bodaboda na magari mengine kama Toyota Noah zinazofanya kazi ya kusafirisha abiria vijijini ni balaa tupu.

Gharama ni kubwa kuliko uhalisia na ukweli wa maisha ya Watanzania wa vijiji vya mikoa karibu yote, ikiwamo ya Rukwa, Katavi, Songwe, Njombe, Morogoro, Kagera na Manyara.

Kwa maana nyingine, nauli za vijijini zinaonyesha wazi kwamba wananchi vijijini ni kama wanatawaliwa na viongozi tofauti na wanaotawala watu wa mijini.

Wenye vyombo vya usafiri vijijini wanaonekana kuwa na uamuzi wao na si wa Serikali, kwa kuwa wanavyopanga nauli lazima itekelezwe bila kuangalia uhalisia, huku wakijaza abiria kuliko kawaida.

Vyombo vinavyohusika na usalama wa abiria pamoja na masuala ya usafiri ambavyo ni Polisi na Sumatra vimejisahau kuhusu nauli na usalama wa abiria vijijini.

Ni wazi watu wengi wanaweza kuamini kwamba Sumatra ipo kwa ajili ya kuangalia nauli za mijini na kuwaacha wananchi wa vijijini wakihangaika.

Kwa mfano, Sumatra imesimamia nauli za mijini ziwe Sh400 kutoka kituo hadi kituo katika umbali usiozidi kilomita 10, lakini nauli ya vijijini kwa umbali kama huo ni balaa.

Katika Jiji la Dar es Salaam, msafiri anatoka Posta anakwenda Ubungo kwa Sh400 umbali ambao kwa vijijini nauli yake kwa magari kama ya Noah, bodaboda au malori unatakiwa uzidishe Sh400 mara 10.

Kana kwamba haitoshi, hata nauli za mabasi mazuri yanayosafiri kati ya wilaya na wilaya au kati ya mkoa na mkoa ni ndogo ukilinganisha na za vyombo vya usafiri vijijini vinavyosafiri umbali mdogo.

Kwa mfano, mtu anatoka Mbeya hadi Tukuyu wilayani Rungwe umbali wa kilomita 70 analipa Sh3,000 lakini akitoka Tukuyu mjini kwenda Mwakaleli umbali wa kilomita 20 kwa ‘pickup’ au Noah analipa Sh4,000.

Hata wale wanaoteremkia Nditu au Suma, umbali wa kilomita 15 nao wanalipa Sh4,000, huku wenye bodaboda wakitaka Sh10,000 hadi Mwakaleli.

Kwa kweli nauli za vijijini zinawanyonya abiria. Bila shaka hali ni hiyohiyo hata ukitoka Moshi mkoani Kilimanjaro kwenda Kijiji cha Kishumundu au ukitoka Songea mkoani Ruvuma kwenda Kijiji cha Litapwasi au hata kutoka Bukoba mkoani Kagera kwenda Katerero.

Pamoja na kwamba usafiri wa bodaboda umechangia kwa asilimia kubwa kufikika kwa maeneo mengi ya nchi, lakini nauli yake iangaliwe upya.

Hakuna shaka kwamba ujio wa bodaboda nyingi nchini, mbali ya kuongeza ajira kwa vijana na kuwapatia kipato umepunguza au umetatua changamoto zinazowakabili wananchi zikiwamo za ugonjwa na shida zingine kwa haraka.

Pamoja na faida zake, lakini bodaboda zinachangia kudumaza vipato vya wananchi vijijini, kwa vile wanalipa fedha zote kwa usafiri na kubakiwa na kiduchu mfukoni.

Wapo wanaotoka mijini wakielekea kwenye misiba vijijini, lakini wakikodi pikipiki wanajikuta wametumia fedha nyingi zaidi kwenye usafiri kuliko huduma za misiba.

Ni wakati mwafaka kwa Serikali kupitia Sumatra kuweka nauli elekezi kwa bodaboda, bajaji na magari yote yanayobeba abiria vijijini kulingana na umbali kwa kuzingatia uzuri au ubovu wa barabara.

Kwa kawaida na kisheria, hivi sasa nauli ya kilometa moja kwenye barabara za vumbi ni Sh46.11 wakati kwenye lami ni Sh36.89 kwa kila kilomita.

Noah, malori na bodaboda vijijini zinapita kwenye barabara za umma, hivyo sioni sababu za kutoza nauli kubwa bila sababu za msingi.

0767338897