Bodi ya Stamico ifufue Mgodi wa Kiwira

Godfrey Kahango ni mwandishi wa gazeti hili anayepatikana mkoani Mbeya. Wasiliana naye kwa 0715 059 107 au [email protected]

Muktasari:

  • Bodi hiyo ilitembelea mgodi huo pamoja na machimbo mengine ya makaa ya mawe ya Kibulo yote ya wilaya hiyo hiyo na kujionea utajiri wa kutosha ambao Tanzania imejaaliwa.
  • Mgodi wa Kiwira ulioanzishwa mwaka 1988 kabla haujasimamisha shughuli zake miaka 20 baadaye, mwaka 2008. Ni mgodi unaomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia Stamico.

Hivi karibuni, Bodi ya Shirika la Madini (Stamico) ilitembelea Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira uliopo Wilaya ya Ileje mkoani Songwe.

Bodi hiyo ilitembelea mgodi huo pamoja na machimbo mengine ya makaa ya mawe ya Kibulo yote ya wilaya hiyo hiyo na kujionea utajiri wa kutosha ambao Tanzania imejaaliwa.

Mgodi wa Kiwira ulioanzishwa mwaka 1988 kabla haujasimamisha shughuli zake miaka 20 baadaye, mwaka 2008. Ni mgodi unaomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia Stamico.

Lengo la kuanzishwa kwa mgodi huo ilikuwa kuzalisha tani 150,000 za makaa ya mawe kwa mwaka kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya umeme kuendesha viwanda nchini hasa Kiwanda cha Saruji kilichopo Mbeya, Kiwanda cha Karatasi cha Mgololo, viwanda vya chai; Katumba na Musekela vya Tukuyu.

Ukweli usiopingika ni kwamba tangu mgodi huo usitishe shughuli zake kisha wafanyakazi kuondolewa, wapo wanaoendelea kulalamikia kupunjwa mafao yao hadi leo.

Kumekuwa na matamko mbalimbali ya viongozi wa Serikali juu ya kuufufua mgodi huu ingawa utekelezaji bado haujafanywa na ziara ya bodi hii kuonekana kama sehemu ya kuwafaraji wananchi.

Bodi hii mpya ambayo iliteuliwa mwaka jana imekuja na mtazamo mpya wa kuhakikisha mgodi huo unafufuliwa ili fursa zilizopo ziweze kuwanufaisha wananchi.

Kwa mujibu wa maelezo ya Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Kiwira, Mhandisi Aswile Mapamba kwa wajumbe wa bodi hiyo mpya, licha ya kusimama uzalishaji, miundombinu yote muhimu bado ipo vizuri kutokana na utunzaji uliopo na kuiomba bodi kuwapatia fedha kwa ajili ya matengenezo ya baadhi ya mitambo.

“Tunaomba bodi itusaidie kupata mtaji wa kufufua mgodi,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Balozi Alexandar Muganda alisema kipaumbele cha kwanza ni kuufufua mgodi huo ambao unahitaji Sh9 bilioni ili uanze kuchimba makaa ya mawe wakati mchakato wa kufufua mitambo ya kufua umeme ukiendelea.

Muganda alisema endapo bodi hiyo ingekuwa na uwezo wanatamani kuona mgodi unaanza kazi ya kuchimba makaa ya mawe hata ndani ya mitatu au minne ijayo ili fursa zilizopo ziwanufaishe wananchi.

Kwa kauli ya bodi hii mpya inaonesha dhahiri kwamba matumaini ya wananchi kuanza kupata fursa mbalimbali zitokanazo na uzalishaji wa mgodi huo zinaanza kuonekana.

Wananchi wanategemea kuona hakutakuwa na kauli zenye maneno matamu ambayo walishazoea kupewa kutoka kwa viongozi mbalimbali waliotangulia bila ya utekelezaji wowote.

Hivyo wanaamini kabisa kauli na dhamira iliyooneshwa na bodi hii, mgodi huu sasa umepata wasimamizi wenye nia ya dhati kuuona unafanya kazi kwani miundombinu yote muhimu ipo katika hali nzuri, kinachohitajika ni matengenezo kwa baadhi ya mitambo tu kutokana na kukaa muda murefu bila kufanya kazi kama ilivyobainishwa na mtendaji wake mkuu.

Ni matumaini yangu kwamba ziara ya bodi hii mpya kwenye mgodi huu na kutazama utajiri uliopo sasa umepata mwarobaini wake.

Naamini, bodi haitakuwa na kauli za kisiasa kwenye utekelezaji wa mpango wa kuufufua mgodi huu mapema iwezekanavyo ili kuwanufaisha wananchi wanaoutegemea.

Kufufliwa kwa mgodi huu kutaimarisha mzhunguko wa fedha.

Kahango ni mwandishi wa gazeti hili anayepatikana mkoani Mbeya. Wasiliana naye kwa 0715 059 107 au [email protected]