Changamoto ya viwanja inaepukika

Muktasari:

  • Msimu uliopita na mingine, mechi kadhaa za ligi hiyo zilipangwa kufanyika katikati ya wiki kutokana na sababu mbalimbali.

Mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zimepangwa kuchezwa kila wikiendi msimu huu, baada ya marekebisho kadhaa yaliyofanywa.

Msimu uliopita na mingine, mechi kadhaa za ligi hiyo zilipangwa kufanyika katikati ya wiki kutokana na sababu mbalimbali.

Lakini, mabadiliko ya msimu huu yameonyesha kuwa hakuna sababu ya msingi ya kucheza mechi hizo katikati ya wiki, huku pia timu nyingi zikinufaika na mapato ya milangoni.

Mechi ambazo huchezwa katikati ya wiki inakuwa na shida ya mapato kutokana na mashabiki wengi kuwa kwenye majukumu mengi ya uzalishaji mali hivyo, kushindwa kupata fursa ya kwenda viwanjani.

Lakini, kuna changamoto nyingine ambayo imekuwa kama tatizo sugu katika ligi kubwa tatu zinazosimamiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa maana ya Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na la Pili.

Msimu huu, changamoto ya viwanja imekuwa kubwa hasa kwa kituo cha Arusha baada ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kufungwa ili kupisha ukarabati.

Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ni miongoni mwa viwanja vinavyomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wamiliki hao wameamua kuufunga kwa muda na kuzifanya timu za Arusha za Daraja la Kwanza na la Pili kuhamia Moshi kwenye Uwanja wa Ushirika.

Timu kama Pepsi, JKT Oljoro, AFC zimeshindwa kuwa mbele ya mashabiki wao wa nyumbani kutokana na uwanja huo kufungwa, jambo ambalo pia liliathiri ratiba za mechi za kituo hicho.

Lakini, TFF pia imeshindwa kukaa mezani na wamiliki wa viwanja hivyo kutatua tatizo la viwanja, ambalo limekuwa likisogeza ama kurudisha nyuma mechi kadhaa za ligi husika.

Katika Ligi Kuu, mchezo wa Mbao FC dhidi ya Mbeya City msimu huu ulilazimika kuchezwa Ijumaa badala ya wikiendi, huku pia mchezo mwingine kabla ya huo ukipisha tamasha la muziki la Fiesta.

CCM Kirumba ulikodishwa kwa ajili ya tamasha la Fiesta na kusababisha wamiliki kuwapa waandaaji wa tamasha hilo uwanja na kufanya mchezo wa Simba dhidi ya Mbao FC kuahirishwa.

Kwa mujibu wa mameneja wa viwanja hivyo, wamiliki wanahitaji viwanja vyao viingize mapato kwani ni moja ya vyanzo vyao, hivyo ofa za matamasha huja mapema na kutoa nafasi ya kujiingizia fedha zaidi.

Lakini, shirikisho limeshindwa kukaa na kuzungumza na wamiliki juu ya umuhimu wa michezo yao na kutafuta njia sahihi ya kutohamisha siku sahihi za mechi zilizopo katika ratiba yake.

Kama suala ni ukarabati nadhani TFF inaweza kukaa na baadhi ya makampuni na kuingia ubia na wamiliki kwa lengo la kuvikarabati na kupewa kipaumbele kwanza katika michezo yao badala ya matamasha.

Lakini, kinachoonekana ni kutokuwa na utayari wa kufanya suala la viwanja kuwa sehemu ya ushiriki wa TFF, ambayo imewaachia viongozi wa klabu kuzungumza na wamiliki wa viwanja huku wao wakijiweka pembeni.

TFF inaonekana kujitoa katika suala hilo na kuacha wamiliki kuamua watakavyo, kwanza kabla ya mechi kuwa suala la mwisho wanapokosa tenda nyingine katika ukodishaji wa viwanja.

Inawezekana kabisa TFF ikakaa na wamiliki wa viwanja hata kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi na kupanga nao ratiba, lakini hapo hapo wakawaambia nini wanataka katika kurekebisha viwanja.

Kukiwa na ushirikishwaji kama huu sidhani kama kutakuwa na mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara, Daraja la Kwanza wala la Pili utakaobadilishwa ili kupisha shuguli zingine.

Ushirikishwaji wa wamiliki wa wa viwanja katika upangaji wa ratiba na kuzungumzia changamoto za viwanja kabla ya msimu kuanza, ni jambo la msingi sana kwa sasa.