Changamoto za elimu bure zijadiliwe

Muktasari:

  • Ni onyo lilitokana na taarifa za kuwepo kwa walimu wakuu wanaoendelea kuwatoza wazazi michango kinyume na agizo la Serikali la kuzuia michango yote ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa elimu bure.

        Juzi Rais John Magufuli alitoa onyo kali akitaka walimu kusitisha michango wanayowatoza wazazi shuleni.

Ni onyo lilitokana na taarifa za kuwepo kwa walimu wakuu wanaoendelea kuwatoza wazazi michango kinyume na agizo la Serikali la kuzuia michango yote ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa elimu bure.

Tangu iingie madarakani, Serikali ya Awamu ya Tano, imekuwa ikisimamia utekelezaji wa mpango wa elimu bure, unaotokana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Onyo hili linatupa picha ya Serikali iliyo makini katika kusimamia mamuzi yake. Kwetu sisi pia hii ni ishara ya Serikali inayowajbika, kwa kuhakikisha inatekeleza kile inachokipanga na kuamini kuwa kina manufaa kwa wananchi.

Hata hivyo, tunapotekeleza agizo hili, kuna haja pia ya kuangalia uhalisia katika shule zetu hasa sababu zinazowasukuma walimu kutoza michango. Tunakubali kuwepo kwa walimu wanaotumia michango hiyo kama vyanzo binafsi vya mapato, lakini uhalisia pia unaonyesha kuwa katika shule nyingi hali si shwari. Mazingira ya kutolea elimu siorafiki, hivyo kuwalazimu walimu kutafuta namna ya kunusuru hali shuleni.

Hali hii imekuwa mbaya zaidi baada ya kuanza kwa elimu bure kulikochangia ongezeko la wanafunzi. Kumeibuka changamoto kadhaa ambazo uzoefu unaonyeha Serikali pekee haiwezi kuzikabili.

Walimu wanaochangisha wazazi, wanafanya hivyo kwa sababu hata ruzuku inayotumwa shuleni ama haitoshi au haifiki kwa wakati.

Novemba 2016, asasi isiyo ya kiserikali ya Twaweza, ilitoa ripoti ya utafiti iliyoonyesha kati ya Sh10,000 zinazotumwa kwa mwanafunzi wa elimu ya msingi kwa mwaka, ni wastani wa Sh2000 iliyofika shuleni.

Lakini pia ruzuku hiyo haijumuishi baadhi ya mambo hivyo kuwalazimu walimu kutafuta njia za kupata kipato ikiwamo michango.

Tusipokuwa tayari kuangalia mazingira halisi, tunaweza kuwa na jibu lilelile kuwa walimu wanataka kujinufaisha, halafu tukawa hatuwatendei haki. Katika shule nyingi walimu wanalalamika kuwa fedha wanayopata haikidhi mahitaji ya uendeshaji wa shule hasa katika mambo ambayo hayajaainishwa kama matumizi ya fedha za ruzuku. Mfano ulinzi, ziara za kimasomo, chakula na mengineyo.

Kwa upande mwingine, tamko la Rais na kinachoendelea sasa katika baadhi ya shule, ni ishara tosha ya kuwapo kwa mkanganyiko kuhusu dhana na utekelezaji wa elimu bure. Kunahitajika uchambuzi wa kina wa changamoto zinazojitokeza na sababu za walimu kuanzisha michango hiyo ili kupata suluhisho badala ya kuwatuhumu walimu kuwa wanaendesha michango hiyo ili kujipatia fedha tu.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa wazazi bado wanachangia vifaa kama madaftari, nauli, sare na hata chakula kwa shule zilizo mbali na makazi na hivyo baadhi hawaoni tatizo wanapoambiwa wachangie vitu vingine na uongozi wa shule.

Ni wakati sasa wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji pamoja na Tamisemi kukaa na wadau wa elimu na kujadili changamoto hizo ili kupata njia bora ya kutekeleza mpango wa elimu bure kwa ushirikishwaji na hivyo kuondoa kero kwa wazazi.

Kama Rais alivyosema, bado kuna changamoto katika elimu zinazotokana na elimu bure hivyo, kuna haja kubwa ya kujadili changamoto hizo pamoja na hizi zinazosababisha kuibuka kwa michango kinyume cha maagizo.