Congo si salama kwa madereva

Muktasari:

  • Hofu ilitanda kuwa huenda wangetumiwa na waasi hao kama ngao wakati wa mapambano baina yake na majeshi ya Serikali.
  • Habari hii ni ya kushtua na kusikitisha hasa kwa kuwa hii si mara ya kwanza kwa madereva kutoka Tanzania kutekwa na waasi nchini humo.

Juni 29, madereva 24 wa malori ya mizigo kati yao 21 wakiwa Watanzania walitekwa na waasi wa Mai-Mai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Hofu ilitanda kuwa huenda wangetumiwa na waasi hao kama ngao wakati wa mapambano baina yake na majeshi ya Serikali.

Habari hii ni ya kushtua na kusikitisha hasa kwa kuwa hii si mara ya kwanza kwa madereva kutoka Tanzania kutekwa na waasi nchini humo.

Septemba 15, mwaka jana, madereva walitekwa wakiwa kwenye malori 12 katika eneo la Namoyo Jimbo la Kivu Kusini, nchini humo.

Utekaji huo pia ulitekelezwa na kikundi hichohicho cha waasi cha Mai Mai.

Madereva waliotekwa wakati huo ni pamoja na Hussein Mohamed, Athuman Fadhili, Mwamu Mbwana, Twaha Issa, Iddi Omari, Adam James, Juma Zaulaya, Bakari Shomari na Hamdani Zarafi.

Ilielezwa kuwa baada ya utekaji magari hayo, waliwashusha madereva na kuwapeleka porini kisha kuyateketeza kwa moto malori manne.

Awali kabla ya kuchoma moto magari hayo, waasi hao walitishia kuwaua madereva hao huku wakitoa masharti kuwa ndani ya saa 24 kuanzia jioni ya Septemba 14 walipwe fedha kiasi cha Dola za Marekani 4,000 kwa kila dereva.

Ni dhahiri kwamba safari za DRC zimekuwa ni hatari kwa maisha ya madereva, mali za wateja husika na wamiliki wa magari kutokana na matukio hayo ya utekaji.

Tayari Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetoa ushauri kwa wafanyabiashara na watu wengine wanaokusudia kwenda DRC kuwa waangalifu au kusitisha kwa muda safari zao.

Nina hofu kuwa wapo ambao wanaweza kukaidi kwa kuamini kwamba hao madereva wametekwa kwa bahati mbaya, hivyo wao wana bahati nzuri na wanaendelea kufanya shughuli za kusafiri kama kawaida.

Mkurugenzi wa kampuni ya Simba Logistics, Azim Dewji ambaye ni mmoja wa wamiliki wa malori yaliyokuwa yakiendeshwa na madereva 12 waliotekwa awali, alikaririwa na vyombo vya habari akieleza hasara waliyoipata kutokana na hatua ya waasi hao kuchoma moto magari.

Walipata hasara ya Sh1.5 bilioni kutokana na kitendo cha waasi hao kuchoma malori yake sita, ambayo alieleza kuwa hasara ingeweza kuzidi, hasa kama malori hayo yaliyokuwa yakirejea Dar es Salaam yangebeba mzigo.

Tunashukuru kwamba madereva hao wamerudi salama na sasa wameungana na familia zao, lakini wamiliki wa magari nao wanapaswa kutafakari kwa makini kuhusu safari za kuelekea kwenye nchi hiyo.

Hatari inaonekana kwa kuwa maeneo ya utekaji nayo yamekuwa yakibadilika, kwani tukio hili hivi karibuni, inabainishwa kuwa madereva hao walitekwa wakiwa Lulimba.

Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba waasi hao hawakupatwa na moyo wa ukatili wa kuwadhuru au kuwaua madereva hao, kwani baada ya kuwapora mali waliwaachia huru.

Siyo rahisi kutambua kiwango cha mateso na usumbufu waliopata madereva hao licha ya kwamba waliachiwa huru, lakini tujiulize je, walipata wapi chakula na malazi kwa sababu hawakuwa na fedha.

Mali inaweza kutafutwa na inawezekana wamiliki wa magari wamekatia bima malori hayo hivyo watalipwa, lakini uhai wa madereva hauwezi kurejeshwa kama wangeuawa.

Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa wamiliki wa malori kufuata ushauri wa Serikali kuwa baadhi ya maeneo ya DRC si salama kusafiri.

Kama hakuna ulazima wa kusafiri kwenda DRC, wamiliki wa malori wangesitisha safari za huko kuokoa roho za madereva.

Beatrice Moses ni mwandishi wa Mwananchi.