Dalili saratani ya matiti huchelewa, vidonge uzazi huchangia

Muktasari:

  • Ingawa dalili za saratani hii hazijitokezi kirahisi, zipo ishara za awali ambazo zinapaswa kukupa tahadhari. Hizi zinajumuisha  uvimbe kwenye matiti au kwapa, mabadiliko ya umbo la titi.
  • Wakati mwingine chuchu hutoa maji yasiyo na rangi au uchafu mwinginekama vile usaha, damu au maji yenye rangi ya njano au kahawia.
  • Kupata ujauzito ukiwa na zaidi ya miaka 30 inaelezwa kuchangia maambukizi ya saratani hii kwa wanawake wengi ambayo huwakumba zaidi ambao hawajazaa au kunyonyesha.

Tofauti na magonjwa mengine kama malaria ambayo dalili zake hueleweka, saratani ya matiti hushambulia kimya kimya. Kutokana na hilo, ndiyo ugonjwa unaoongoza kwa kusababisha vifo miongoni mwa aina nyingi zilizopo.

Ni rahisi kufahamu una malaria pindi utakapohisi maumivu ya viungo, homa na kukosa hamu ya kula kitu ambacho haitokei ukiwa na saratani ya matiti, dalili hazijitokezi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari, saratani hii ndiyo iliyochukua uhai wa Katibu wa Chama Cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata), Dk Subilaga Kasesela-Kaganda.

Kuenzi juhudi zake ambazo zitaendelea kuishi, makala ya leo itatoa ufahamu wa saratani ya matiti ikiwa ni moja ya mambo aliyokuwa akiyapigania Dk Kaganda tangu 2005.

Saratani ya matiti ni moja ya saratani inayochukua uhai wa maelfu ya wanawake kila mwaka ikiwa ya pili kwa kusababisha vifo vya wanawake duniani. Asia na Afrika, husababisha vifo vya mapema zaidi kutokana na kutogundulika kwa wakati.

Saratani hii hutokea katika titi ambalo lina sehemu ya kutengenezea maziwa ijulikanayo kitabibu kama lobules na katika aina mojawapo ya mishipa inayounganisha yanapotengenezwa maziwa na chuchu.

Saratani ya matiti inapotokea husababisha kubadilika kwa ukuaji wa chembe hai za mwili na kuwa wa kiholela pasipo kufuata utaratibu wa kawaida.

Sababu yake ni nini?

Bado sababu ya moja kwa moja inayosababisha saratani hii kwani kwa wanasayansi na matabibu wanadai bado ni fumbo.

Lakini yapo mambo ambayo yanaaminika kwa namna moja au nyingine, yanachangia tatizo hili ikiwamo aina fulani ya chembe za urithi inayosababisha chembe hai zipoteze ufanisi wake.

Hali hii husababisha zigawanyike kwa kasi isiyo ya kawaida, kuvamia na kushambulia tishu nyingine na kuepuka kuharibiwa na mfumo wa kinga kutokana na hitilifu ilizonazo.

Baadaye chembe hizo huvamia, kushambulia na kuharibu viungo vingine vya mwili hatimaye kusababisha kifo.

Watu waliohatarini kuugua

Yapo mambo yanayomuweka mtu katika hatari ya kupata saratani ya matiti. Haya ni pamoja na umri. Inaelezwa kuwa kadiri umri unavyosonga, ndivyo hatari ya kupata saratani hii inavyokuwa kubwa. Wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 50 wapo kwenye hatari mara mbili mpaka tatu kuliko walio chini ya miaka 45.

Jinsi ni sababu nyingine

Saratani hii inaweza kuwapata wanaume lakini wanawake ni waathirika wakilinganishwa na wanaume.

Kutokana na sababu za kinasaba, historia ya familia nayo ni muhimu kuizingatia. Watu hasa wanawake wanaotoka katika familia zenye historia ya ndugu kuugua saratani hii wako katika hatari ya kuupata pia.

Asili ya mtu pia ni kihatarishi kingine. Takwimu zinaonyesha saratani hii huwapata zaidi wanawake wazungu kuliko weusi.

Uzazi ni suala jingine. Inaelezwa kwamba wanawake ambao hawajazaa au kunyonyesha wapo katika hatari zaidi ya kupata saratani hii kuliko waliofanya hivyo. Vile vile wanawake wanaopata ujauzito wa kwanza wakiwa na umri wa miaka 30 au zaidi, wapo katika hatari ya kupata saratani hii.

Wasichana wanaovunja ungo kabla ya miaka 12 wapo kwenye hatari ya kupata saratani hii. Hili hujitokeza pia kwa wanawake wanaochelewa kufika ukomo wa hedhi wapo katika hatari ya kupata saratani hii.

Kuwa na uzito au unene uliopitiliza pia ni kujiweka kwenye hatari ya kupata maambukizi ya saratani hii. Takwimu zinaonyesha wanawake wanene wana hatari zaidi ya kupata saratani hii wakilinganishwa na wale wenye uzito wa kawaida.

Mwanamke aliyewahi kuugua saratani hii katika titi moja yupo kwenye hatari zaidi ya kuliambukiza la upande wa pili baada ya muda.

Hata aina ya vyakula anavyotumia navyo ni miongoni mwa sababu za maradhi haya. Utafiti unaonyesha wanawake wanaokula zaidi vyakula vyenye mafuta mengi ndiyo wapo katika hatari yakupata saratani hii tofauti na wasiofanya hivyo. Matibabu yanayohusisha mionzi nayo yanafaa kuepukwa ikibidi. Pamoja na kwamba mionzi ni tiba ya saratani,  lakini wanawake waliowahi kutibiwa kwa mionzi wakati wa ukuaji wa matiti, ndiyo wapo katika hatari ya kupata saratani hii.

Baadhi ya kemikali hasa za viwandani zikiwamo polychlorinated biphenyls, olycyclic aromatic hydrocarbons na dawa za kuulia wadudu hurahisisha maambukizi ya saratani hii. Kwa walioajiriwa viwandani, hukumbana moja kwa moja na kemikali hizo zina hatarisha kupata saratani mbalimbali.

Wanawake wanaokunywa zaidi ya chupa moja ya pombe kwa siku, wapo kwenyehatari zaidi ya kupata saratani hii kwa zaidi ya asilimia 20. Pombe huongeza uwezekano wa kutumia vyakula vyenye mafuta mengi na kupandisha uzito wa mnywaji.

Baadhi ya utafiti unaonyesha uhusiano uliopo kati ya wanawake wanaovuta  sigara na uwezekano wa kupata saratani ya matiti. Ikumbukwe kuwa uvutaji ni moja ya kihatarishi cha kupata saratani za aina nyingi zilizopo.

Vidonge vya kupanga uzazi navyo vinawekwa kwenye kundi la vihatarishi. Upo ushahidi wa kitafiti kuwa saratani ya matiti ina uhusiano na matumizi ya muda mrefu ya vidonge vya kupanga uzazi.

Kingine ni vichochezi vya mwili. Uwapo wa kiwango kikubwa cha vichochezi au hormons za oestrogen na progestrone huongeza hatari ya kupata saratani ya matiti.

Vile vile watu walio na viwango vya juu vya kichochezi kinachodhibiti kiwango cha sukari mwilini (insulin) na kiwango cha chini cha kichochezi cha usingizi kijulikanacho kitabibu kama melatonia hali inayojitokeza zaidi kwa wanawake wanaofanya kazi za usiku, wako katika hatari hii.

Ukubwa wa matiti pia hutoa angalizo kwa saratani hii. Wanawake wenye matiti makubwa wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani hii kwa sababu huwawia vigumu madaktari kubaini uvimbe katika matiti yao wakati wa uchunguzi wa mwili.

Viashiria

Dalili za saratani hii huwa ni ngumu kuzibaini isipokuwa kwa vipimo, mgonjwa anaweza kuanza kuhisi tofauti saratani hii ikiwa kwenye hatua za mbele zaidi.

Moja ya dalili za awali ni uvimbe katika mojawapo ya matiti au kwapa, mabadiliko ya umbo la titi na chuchu kutoa maji yasiyo na rangi au wakati mwingine uchafu mfano usaha au damu au maji yenye rangi ya njano au kahawia.

Pia, chuchu kuwa na vinundu mfano wa maganda ya machungwa, chuchu kuwasha au kuhisi kuchoma, kubadilika kwa ngozi ya matiti kwa kututumka na chuchu kudidimia ndani ni miongoni mwa ishara muhimu kuitambua saratani hii. Hapo baaadaye saratani hii inaweza kusambaa kupitia mkondo wa damu, mfumo wa kinga unaochuja vimelea ujulikanao kama lymph na tishu zilizo jirani na sehemu iliyopata maambukizi ya saratani hii.

Mara nyingi viungo vinavyovamiwa na saratani ni pamoja na mapafu, ini, ubongo, mifupa. Dalili za saratani kusambaa ni pamoja na kuongezeka kwa mabadiliko ya  matiti, kupanda kwa joto la mwili, kovu kwenye chuchu, maumivu ya mifupa, maumivu kwenye matiti, kuvimba mikono, kupungua uzito wa mwili au kuwa na vidonda kwenye ngozi.

Dalili nyingine zinaweza kujitokeza kulingana na kilipo kiungo kilichoshambuliwa na saratani hii. Kuna wanawake wengine wana viashiria vya asili vinavyojulikana kama Her2 positive breast cancer ambacho husaidia seli kuongezeka, kugawanyika na kujirekebisha pale zinapoharibika.

Kiashiria hiki kinaaminika ndicho kinasababisha wanawake hawa kuwa na saratani ya matiti yenye madhara zaidi na kuwa na uwezekano mkubwa wa kujirudia baada ya tiba tofauti na wale ambao hawana.