Dart iharakishe mchakato wa kadi za malipo mabasi yaendayo haraka

Muktasari:

  • Mkurugenzi mtendaji wa Udart, Charles Newe wakati wa kuyapokea mabasi hayo katika Bandari ya Dar es Salaam yakitokea nchini China amesema kwamba yataongeza nguvu katika kutoa huduma ya usafiri huo ambao mahitaji yake yanazidi kuongezeka siku hadi siku.

Juzi, kampuni ya mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (Udart), iliingiza mabasi mapya 70 kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma hiyo mpya na ya aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mkurugenzi mtendaji wa Udart, Charles Newe wakati wa kuyapokea mabasi hayo katika Bandari ya Dar es Salaam yakitokea nchini China amesema kwamba yataongeza nguvu katika kutoa huduma ya usafiri huo ambao mahitaji yake yanazidi kuongezeka siku hadi siku.

Mabasi hayo yataongeza nguvu kutokana na uwezo wake, kwani kwa mujibu wa maelezo ya Newe, kila moja linaweza kubeba abiria 150 hadi 160.

Tangu usafiri huo ambao kwa sasa unatoa huduma katika njia za Kimara, Kinondoni Morocco, Gerezani na Feri na nyingine chache za pembezoni, ulipoanza rasmi Jumatatu ya Mei 16, 2016 umewavutia wananchi wengi hata wale waliokuwa na usafiri binafsi ambao waliacha magari yao na hivyo kusaidia kupunguza foleni katika jiji la Dar es Salaam.

Lakini kama alivyokaririwa kiongozi huyo wa Udart akisema, bado wapo ambao wameendelea kutumia magari binafsi kutokana na mabasi hayo kujaa na kwamba lakini ujio huo utawafanya wayaache nyumbani na kupunguza sio foleni tu, bali hata gharama alizosema kutoka Sh8,000 hadi Sh2,000 kwa siku kwa usafiri binafsi.

Kimsingi, usafiri huo umekuwa na changamoto nyingi zikiwamo hizo za abiria kujaa kupita kiasi, kukaa vituoni kwa muda mrefu na usumbufu katika ukataji wa tiketi na wakati mwingine kurudishiwa chenji.

Hayo yamewafanya baadhi ya wananchi waliokuwa wameacha kutumia usafiri binafsi kuurejea na hata wengine kuamua kutumia mabasi mengine ya kawaida jambo ambalo haliendani na dhamira ya kuanzishwa kwake.

Wakati Udart ikipambana na changamoto hiyo ya uchache wa mabasi ya kutolea huduma, ipo nyingine ya kadi za malipo ambayo tunadhani nayo inahitaji kutatuliwa kwa haraka.

Ilielezwa kwamba kadi hizo za malipo ni chache kiasi kwamba ni asilimia 30 tu ya abiria ndio wanaozimiliki na hilo linadhihirishwa na foleni za kukata tiketi asubuhi na jioni katika vituo vingi vya mabasi hayo.

Wiki iliyopita mkurugenzi mkuu wa Wakala wa Usimamizi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Ronald Lwakatare alikaririwa na Mwananchi akisema kuwa tayari mchakato wa kumpata mzabuni wa kadi za usafiri huo umefikia hatua nzuri lakini hakusema lini hasa utakamilika.

Pamoja na unyeti wake, tunadhani kwamba ipo haja kwa wahusika ‘kukesha’ wakitafuta njia zitakazowezesha kupatikana kwa kadi hizo mapema iwezekanavyo kutokana na umuhimu wake.

Kuwapo kwake kutaokoa mambo mengi yakiwamo foleni hizo vituoni, kero ya chenji hivyo kuwapunguzia abiria muda wa kukaa vituoni kama ilivyo dhamira ya usafiri huo.

Ilipotangaza kuanza matumizi ya kadi hizi za malipo, tuliamini kwamba kasi yake itakuwa kubwa na ufanisi wake utaigwa na mashirika mengine ya kutoa huduma hasa ikizingatiwa changamoto nyingi ambazo wananchi wanakabiliana nazo wanapotembea na fedha taslimu.

Wito wetu kwa Dart ni kulifanya suala hili la kadi za malipo kipaumbele chake kikubwa, lifanywe kwa kasi inayostahili ili huduma hiyo ya usafiri iwe ya haraka kwelikweli kama ilivyokusudiwa.