Mkutano Mkuu CCM umeanza asubuhi hii mjini Dodoma

Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wakiendelea na kikao chao leo.

Muktasari:

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anasoma taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

10.30: Mkutano Mkuu wa CCM ulioahirishwa jana umeendelea tena leo mjini Dodoma, hivi sasa kunasomwa taarifa za utekelezaji mbalimbali wa kazi Serikali.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anasoma taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

12:43: Baada ya upigaji kura kwa wagombea wote watatu ili kumpata mmoja, Rais Jakaya Kikwete ameahirisha Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa hadi saa nne asubuhi.

12:11 Mgombea wa mwisho wa CCM Dk John Pombe Magufuli amemaliza kujinadi mbele ya Mkutano mkuu wa CCM.

amesisitiza kuwa atakwenda kuilinda na kuisimamia ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Amesema ataulinda Muungano na kuhakikisha kuwa anakisaidia Chama Cha Mapinduzi kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba

12:01 Mgombea Dk Asha-Rose Migiro amemaliza kujinadi kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM akieleza hisia zake na nia yake thabiti ya kutaka kuliongoza taifa la Tanzania

Amesema atahakikisha anaulinda umoja wa kitaifa, kuulinda Muungano, Kuyalinda kipekee Mapinduzi ya Zanzibar, kupata Katiba Imara, pamoja na kusimamia yale yote yaliyomo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

11:51 Mgombea wa kwanza wa nafasi ya urais Balozi Amina Salum Ali ameanza kujinadi mbele ya wajumbe wa Mkutano mkuu wa CCM.

Amezungumzia suala la kulinda Muungano, kutekeleza  yale mazuri na kuyatafutia ufumbuzi yale yote yaliyoachwa na Rais Kikwete. pia kusimamia majukumu ya chama imara kitakachokuwa na viongozi bora wanaosimamia maadili Serikalini.

Hakuulizwa swali lolote

11:37: Rais Jakaya Kikwete amemaliza kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu mjini Dodoma akimfagilia Katibu Mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana kwa madai kuwa amekifikisha chama katika eneo salama.

10: 59 Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, anaanza kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho

10:56 Mkutano Mkuu wa CCM umeanza mjini Dodoma na Muda huu Katibu Mkuu wa chama Hicho Abdulrahman Kinana anazungumza. Pamoja na mambo mengine Anaeleza jinsi walivyoweza kufanya ziara katika mikoa yote nchi.

8.20 Halmashauri Kuu ya CCM imemaliza kikao chake na imewachagua Dk John Magufuli, Dk Asha Rose Migiro na Balozi Amina  Salum Ali kuingia katika tatu bora.

Taarifa hizo zimewekwa katika Ukurasa wa Twitter wa CCM.

Majina hayo sasa yatapelekwa katika Mkutano Mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura na kupata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi wa Oktoba.

12:18 Halmashauri Kuu ya CCM inayokutana mjini Dodoma leo imemuidhinisha rasmi Dr Ali Mohamed Shein kuwania urais wa Zanzibar kwa awamu ya pili.

Kwa maana hiyo, Dr Shein atachuana kwa mara nyingine na Maalim Seif Shariff Hamad anayewania nafasi hiyo kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

 Wawili hao waligombea mwaka 2010 na kukabana koo katika uchaguzi Visiwani Zanzibar na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU), Shein akiwa Rais na Maalim Seif, Makamu wa Kwanza wa Rais.

Wajumbe wa Halmashauri Kuu wanapiga kura mjini Dodoma jioni hii kupata majina matatu yatakayowasilishwa kwenye Mkutano Mkuu saa 3 usiku leo.


11:03 Kundi la Sauti Salama Z'bar lasambaza vipeperushi Unguja leo kupinga wakongwe kuenguliwa Dodoma, wataka wanaCCM wajiondoe chamani kuanzia kesho.

Vipeperushi hivyo vinasema uteuzi wagombea urais ndani ya CCM umekuwa ukigubikwa na mizengwa kwa muda mrefu sasa, na kwamba wagombea wasiokubalika ndiyo wanaoteuliwa huku wanaokubalika na wananchi wakiachwa ili kulinda maslahi ya watawala wanaomaliza muada wao.


04:45 Kikao cha Halmashauri Kuu bado kinaendelea, taarifa zilizotufikia muda sio mrefu zinasema kuwa inaonesha mvutano ni mkali kuhusu kuchagua majina matatu ambayo yatapelekwa kwenye Mkutano Mkuu kwa ajili ya kuyapigia kura lipatikane moja.


Taarifa zinasema kutokana na mvutano huo, muda wa Mkutano Mkuu itabidi usogezwe mbele. Ulitarajiwa kuanza saa nane mchana


14:13 Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM umeanza saa chache zilizopita, baadhi ya wajumbe wamempokea Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete kwa nyimbo kuwa wana imani na Lowassa.

Kikwete awatuliza wajumbe hao kisha afungua kikao na kuanza kusoma ajenda za kikao hicho.

Taarifa zaidi kuhusu kikao hicho edelea kuwa nasi


11:50 Mheshimiwa Edward Lowassa amezungumza kwa ufupi na Wanahabari kuhusu jina lake kukatwa, Lowassa amesema hajasikia taarifa hizo na kuahidi kuwa akipata taarifa hizo atazungumza.

10:27 Katibu wa Itikadi na Uenezi azungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, awaambia kuwa hana sababu ya kuyataja majina yaliyotoka kamati kuu kwa sababu tayari yameshajulikana

1:32 Tovuti ya CCM imeyatangaza majina matano yaliyopitishwa na Kamati ya CCM (CC) kuwa ni Bernard Membe, John Magufuli, Asha-Rose Migiro, January Makamba na Amina S Ali

12:55 Kikao cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) kimemalizika hivi punde mjini Dodoma na Katibu wa Itikadi na Ueneze Nape Nnauye ameshindwa kutaja majina matano ambayo yatapelekwa kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC)

Badala yake amewaambia waandishi wa habari kuwa majina hayo yatatangazwa saa nne asubuhi.

Aidha kwa mujibu wa Matangazo yaliyorushwa moja kwa moja na kituo cha redio Uhuru, Sophia Simba alisikika akisema kuwa mvutano mkali ulikuwemo ndani kikao hicho na wajumbe, Adam Kimbisa, Dk Emmanuel Nchimbi na yeye mwenyewe hawakukubaliana na maamuzi ya kikao yaliyofikiwa.

10:10 Bado kikao cha Kamati Kuu (CC) kinaendelea taarifa zilizopo ni kwamba kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kimeahirishwa hadi kesho saa nne asubuhi

8:12 Kikao cha Kamati Kuu kinarudi kuendelea na kitatoa taarifa ya majina matano ambayo kwa sababu ya muda yatajadiliwa kesho na Kikao cha Halmashauri na Mkutano Mkuu utafanyika kesho mchana, Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.


7:00 Kamati Kuu ya CCM imeeenda mapumziko mafupi kwa ajili ya Kufuturu na watarejea tena majira ya saa mbili usiku.

4:30 KUMEKUCHA Dodoma, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeanza mkutano wake wa Kamati Kuu saa chache zilizopita.

Taarifa kutoka Dodoma zinasema watu wote wameondolewa ndani ukumbi mpya wa CCM ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari ambapo hivi sasa wanasubiri taarifa hizo nje ya ukumbi huo.

Endelea kuwa nasi kwa habari zaidi kutoka Dodoma ......