Elimu bure iwakumbuke watoto wenye mahitaji maalumu

Muktasari:

Ni darasa lenye zaidi ya wanafunzi 40 wenye mahitaji maalumu na bila kuangalia upekee wake, nao wanatajwa kama wanafunzi wanaofaidi matunda ya elimu bure.

Kutana na Gozibert Godwin(13), mwanafunzi mwenye ulemavu wa kutosikia anayesoma Shule ya Msingi Tumaini iliyopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Ni darasa lenye zaidi ya wanafunzi 40 wenye mahitaji maalumu na bila kuangalia upekee wake, nao wanatajwa kama wanafunzi wanaofaidi matunda ya elimu bure.

Hii sio shule sahihi kwa Gozibert, kwa kuwa tatizo lake ni ulemavu wa kutosikia na sio mlemavu wa akili kama walivyo wengine wote katika darasa lake.

Aliletwa na wazazi wakiamini ana tatizo la akili na baada ya ushauri alitafutiwa nafasi kwenye shule ya Mugeza yenye walemavu wa kundi lake.Hakupata nafasi ya kusajiliwa kwa hoja kwamba amezidi umri.

Walemavu walioko Tumaini ni kitengo maalumu.Hawapandi darasa kama ilivyo kwa walemavu wa kundi lake waliopo Mugeza wanaovuka hatua kwa hatua hadi vyuo vikuu.

Tofauti ya mlemavu na mtu mwenye mahitaji maalumu ni kwamba mtu wa mahitaji maalumu tayari ana ulemavu na wakati huo anahitaji nyenzo nyingine kama baiskeli,fimbo au kofia kwa wenye ulemavu wa ngozi.

Hivyo Gozibert ataendelea kuwa katika shule ya Tumaini katika darasa lilelile lisilo na vifaa wala mwalimu maalumu kwa ajili yake.

Mafanikio ya elimu bure yanatajwa kwa ujumla.Ndani yake kuna kundi la wanafunzi wenye changamoto za maumbile wanaotakiwa kugawana fursa sawa na wengine. Matunda yake ni pamoja na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wanaosajiliwa darasa la kwanza.Ufutaji wa michango nao unatajwa kupunguza mzigo kwa wazazi na walezi.

Badala yake sasa shule zinapokea ruzuku ya Serikali kulingana na idadi ya wanafunzi, ingawa matokeo ya utafiti wa Twaweza April,2017 unasema mzigo sasa umehamia kwa walimu.

Kwa mujibu wa utafiti huo, mwalimu anayeshiriki mpango wa elimu bure anafundisha wanafunzi 164 ikilinganishwa na wastani wa wanafunzi 99 mwaka 2015. Waraka wa elimu namba 5 wa mwaka 2015, unafuta michango shuleni na kusisitiza kuwa ni azima ya Serikali kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila kikwazo cha ada na malipo mengine.

Hata hivyo, nia njema ya Serikali imewaweka kando watoto wenye ulemavu na mahitaji maalumu,ambao hata kabla ya kutangazwa kwa mpango huo, tayari walikuwa wanapambana na changamoto za kimaumbile.

Mpango wa elimu bure uliofichua maelefu ya watoto mijini na vijijini haukutoa kipaumbele kwa kundi hilo kama kuwatambua na kuchambua mahitaji yao. Ni wazi kuwa shule nyingi hazina miundombinu rafiki kwa ajili ya walemavu, ambao hupata adha wanapohitaji huduma za vyoo na hata madarasa kuwa na ngazi ambazo kwao ni vikwazo. Wapo wanafunzi ambao kwa muda wote wanahitaji msaada wa wenzao, ili waweze kuyamudu mazingira na kuzifikia huduma mbalimbali wakiwa shuleni.

Mwanafunzi mwenye ulemavu wa macho ambaye mpango wa elimu bure haujakidhi hitaji lake la kuwa na fimbo nyeupe, kwa vyovyote vile anahitaji msaada kutoka kwa wenzake.

Hata hivyo, mwanafunzi yule yule kama akitambuliwa kupitia mpango wa kutoa elimu bure, sio jambo gumu kwa Serikali kuongeza fungu kwa shule husika kwa ajili ya mahitaji yake.

Gharama za kumtunza mwanafunzi mwenye ulemavu anayesoma shule ya bweni kwa vyovyote vile ni kubwa ikilinganishwa na wengine.

Mahitaji yao yalitakiwa kubebwa moja kwa moja na tamko la mpango wa elimu bure, ili kuwajengea mazingira rafiki ya kujifunza badala ya kuona wanaweza kuwa kundi sawa na wenzao.

Rejea kwa Renatha Leonard mwanafunzi asiyeona wa kidato cha pili shule ya sekondari Rugambwa Manispaa ya Bukoba ambaye Januari 2016 alisajiliwa kuanza kidato cha kwanza.

Hata mwalimu Denice Bishungisa aliyekuwa anasajili alijikuta kwenye mshangao, kwa kuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kupokea mwanafunzi asiyeona shuleni hapo.

Shule hiyo kwa muda sasa inapokea wanafunzi wenye changamoto za kimaumbile na walemavu wa ngozi ambao hujumuika kwa pamoja ndani na nje ya darasa.

Hakuna mwalimu mwenye mafunzo kwa ajili ya walemavu wasioona na kubwa zaidi hakuna hata kifaa kimoja kwa ajili ya kufundishia walemavu wa kundi hilo. Fikiria hali ya Renatha katika safari yake ya maisha ya bweni akiwa ni mwanafunzi pekee asiyeona katika darasa ambalo mwalimu anaandika ubaoni.

Kimsingi, kama mwanafunzi huyu angekuwa ameibuliwa na mpango wa elimu bure, mahitaji yake yangefahamika na kupangiwa shule kulingana na ulemavu alionao.

Wakati tukijivunia mafanikio ya elimu bure, walemavu wapimwe kwa jicho la pekee na tujiulize kama kweli ni sehemu ya wanafunzi wanaofaidi matunda ya mpango huo.

0767489094