Elimu pasipo mchujo haina ushindani wala tija

Muktasari:

Ni taifa gani linaloweza kusimama katika maendeleo pasipo kuwa na ushindani? Tungewapata wapi watu waliosimama katika vizingiti vya mafanikio pasipo ushindani?

Uliwahi kufikiria dunia bila ushindani? Ushindani wa kiuchumi, kisayansi, kisiasa na kijamii?

Ni taifa gani linaloweza kusimama katika maendeleo pasipo kuwa na ushindani? Tungewapata wapi watu waliosimama katika vizingiti vya mafanikio pasipo ushindani?

Kwa maana hii, ni dhahiri kuwa ili dunia iende, lazima kuwe na ushindani miongoni mwa nchi, taasisi, jamii, watu na mambo mengine.

Katika kuleta maendeleo, elimu inabaki kama msingi wa maendeleo katika mataifa mengi. Nchi nyingi zinashindana katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu.

Hawa wanasukumwa na imani kuwa elimu bora itatoa wahitimu bora wanaoweza kuwa kioo ndani ya jamii na taifa, hasa katika kutatua changamoto na kuweza kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Wakati wenzetu wapo mbioni kuboresha viwango, miundombinu, mazingira na sekta zao za elimu ili ziendane na kasi ya ulimwengu. Tanzania bado hatujitambui.

Hatujang’amua nini kinakwamisha maendeleo ya elimu yetu. Kibaya zaidi, hatujui nini kifanyike kuboresha elimu yetu ili iendane na kasi ya maendeleo ya ulimwengu.

Ukweli ni kuwa tumebaki kusota katika wimbi la viongozi wasioweza kutafuta suluhu ya changamoto za elimu, badala yake wamekuwa wakiongeza maswali badala ya majibu.

Viongozi wengi katika sekta ya elimu, wanaendeleza utamaduni wa viongozi waliotangulia; hawa ni wale waliokuwa wakitoa matamko yasiyo na manufaa yoyote kwa mustakabali wa elimu yetu.

Kwa kukumbusha msomaji wa makala haya, hivi karibuni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imetoa agizo la wamiliki wa shule kutokaririsha wanafunzi wala kuwarudisha nyumbani pale wanaposhindwa kufikia viwango vilivyowekwa na shule zao.

Kwa mtazamo wangu, agizo hili silioni kama ni hatua kuelekea katika kutatua changamoto za elimu.

Ni ukweli Serikali tangu sera ya ubinafsishaji ianze ilishindwa kudhibiti ubora wa elimu hasa katika shule za umma, hali iliyochangia shule zake nyingi kupotea kwenye ramani ya elimu.

Tujiulize ziko wapo leo hii shule kama Ilboru, Kibaha, Mzumbe, Msalato na nyinginezo zilizokuwa bora kitaaluma miaka ya nyuma?

Kuibuka kwa shule binafsi zikawa ndiyo mbadala wa elimu bora. Hii inatokana na namna wamiliki wa shule walivyojenga misingi na taratibu katika kusimamia elimu katika shule hizo, ikiwamo kuwachuja au kuwakaririsha wanafunzi wasiokidhi viwango vya ufaulu. Mfumo huu ulikuwepo tangu zama za shule za umma zilipokuwa zikifanya vizuri.

Leo Serikali inaamua kufuta utaratibu huo, viongozi wanasahau kuwa mchujo huwafanya wanafunzi wasome kwa bidii.

Najiuliza, Serikali inataka kuboresha elimu au ndiyo kwanza inazidi kuimomonyoa? Ni dhahiri wasomi wetu watashindwa kushindana na wasomi wa mataifa mengine. Wanafunzi walioshindwa kufikia wastani na viwango wangetafutiwa elimu mbadala.

Elimu ni uwekezaji unaoatazamiwa kutoa wahitimu bora, na elimu bora haiwezi kukosa kuchuja wanaofaa na wasiofaa katika dunia ya ushindani. Mchujo wa wanafunzi unabaki kuwa chachu ya kuongeza ushindani.

Rai yangu ni vema kuwe na chombo maalumu kitakachoundwa kusimamia na kudhibiti huduma za elimu nchini; Serikali iondokane na usimamizi wa moja kwa moja wa elimu.

Aidha, viongozi wa wizara ya elimu wasiwe wasemaji wa wizara, kuwepo na chombo au kamati ya kushauri kwa ajili ya kutoa maamuzi. Waziri abaki kama mtoa taarifa tu.

Noel Shao ni mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa nchini. 0769735826