Elimu ya biashara isisitizwe kukuza ujasiriamali

Muktasari:

  • Benki ni taasisi muhimu kwa maendeleo ya biashara na uchumi kwa ujumla. Nchini, kuna benki zaidi ya 50 lakini ni wananchi wachache wanatumia huduma zake. Elimu ya umuhimu wa huduma za fedha ikiwafikia wajasiriamali wadogo wakazitumia fursa zilizopo kwenye sekta hiyo itasaidia kukuza biashara zao na kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa.

Wakati Serikali ikisisitiza kujenga uchumi wa viwanda, sekta binafsi inatakiwa kushiriki kwa kiasi kikubwa kufanikisha ndoto.

Mazingira rafiki ya uwekezaji na uanzishaji biashara yanahitajika kuwashawishi wananchi kutumia rasilimali walizonazo kuanzisha miradi au kushirikiana na kampuni za nje kuwekeza nchini.

Juhudi kadhaa zinafanywa na kila upande. Serikali inarekebisha sera na sheria zilizopitwa na wakati ili kuhamasisha uwekezaji katika sekta tofauti.

Mafunzo ni sehemu muhimu kufanikisha uendeshaji na usimamizi wa viwanda. Kwa miaka ya karibuni limeibuka kundi la taasisi au vituo vya mafunzo na elimu za ujasiriamali.

Hili ni jambo jema na zuri katika kuwaandaa wajasiriamali wanaoweza kupambana ndani hata kimataifa.

Ushindani wa sasa unaenda kasi kulingana na mabadiliko ya uchumi wa dunia. Yapo maeneo mengi ambayo watoa huduma wanasisitizwa kujikita kuwasaidia wajasiriamali wadogo wanaohitaji zaidi mafunzo hayo kukuza biashara zao.

Mafunzo yanayotolewa yanapaswa kusaidia kutambua umuhimu wa huduma za fedha, changamoto inayowagusa zaidi wafanyabiashara wadogo. Mafunzo haya yatoe majibu ya kero hii na kuonyesha njia zitakazosaidia kuimarisha mtaji na kutanua biashara.

Sekta ya fedha ni muhimu sana kufanikisha ujenzi wa viwanda. Fedha hufanikisha mradi wowote ulioandaliwa vizuri.

Watu wachache nchini wanatumia huduma hizi. Takwimu zinaonyesha ni asilimia 16.9 ya Watanzania wote wanahudumiwa na zaidi ya benki 50 zilizopo nchini.

Pamoja na namna nyingine za kukuza mtaji, mikopo ya benki hizi ni muhimu na wajasiriamali wanapaswa kuzitumia kufanikisha malengo yao.

Kitu muhimu kwa wajasiriamali ni kuwa na mpango-biashara. Kuna ulazima mkubwa wa kuwafundisha wajasiriamali wadogo namna ya kuandaa mpango biashara hata kwa biashara ndogo utakaowawezesha kunufaika na huduma za benki.

Kutambua na kufuata sheria muhimu za ndani na kimataifa. Kufanya biashara kuna taratibu zake za kisheria ambazo ni vizuri sana kuzifuata ili kuepuka usumbufu.

Kutokana na ukweli kwamba si wafanyabiashara wote wanazifahamu sheria na kanuni tofauti za biashara, ni vizuri wakufunzi wa ukuzaji biashara wakatoa tafsiri kwa kuwajulisha wajasiriamali mambo hayo.

Kwa kufahamu sheria gani zipo na namna ya kuzifuata itawasaidia kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa usalama. Sheria hizi zinajumuisha za kodi, urasimishaji biashara, mazingira na nyingi nyingine. Ni muhimu wajasiriamali wazifahamu japokwa uchache.

Ukosefu wa masoko ni kilio cha wajasiriamali wengi nchini. Hii ni taaluma inayojitegemea na ndio sehemu ya mwisho kwenye mnyororo wa thamani kwani ndipo watumiaji huduma na bidhaa wanapatikana.

Moja kati ya maeneo yanayokua kwa haraka sanjari na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ni masoko. Wakufunzi wa ukuzaji biashara wanatakiwa kuweka nguvu kubwa kwenye mbinu za uzalishaji, kuhimili ushindani nje na ndani, kuongeza wateja, ubunifu na uvumbuzi na uongezaji wa thamani wa bidhaa na huduma.

Watu wengi hukosa uthubutu wa kuanza biashara. Kundi kubwa linakwama hapa kwa kushindwa kubaini njia gani bora ya kuanza na kusimamia biashara inayoweza kufanikiwa.

Mafunzo ya kiufundi yanahitajika pia. Ni vyema kusimamia weledi kwa kuhakikisha yanatolewa na watu wa taaluma husika mfano masoko, fedha, ujenzi, madini na gesi.

Mwandishi ni mtaalamu wa sekta ndogo ya fedha. Kwa maoni, anapatikana kwa 0657 157 122 au 0628 535 117