Epuka mambo haya ili ngozi yako iwe na mvuto

Muktasari:

DONDOO

Ngozi inaweza ikapoteza ulaini na unyororo halafu mng’aro pia ukapotea kwa sababu nyingi tu ila chache kubwa ni kuishi katika maeneo yenye baridi kali, kushinda katika jua kali kwa muda mrefu kila siku,  kutumia sabuni na mafuta yenye kemikali hatari, kuoga maji ya moto kila siku bila sababu za msingi, kujikuna kwa kucha mara kwa mara, kuugua maradhi mazito kwa muda mrefu, kutumia dawa kali kwa matibabu pamoja na unywaji wa pombe unaopitiliza, na kuvuta sigara.

Ni ajabu lakini ndio ukweli wenyewe. Binadamu ana viungo vingi sana lakini ngozi ndio kiungo kikubwa kuliko vyote. Hii inatokana na ukweli kuwa ngozi ya binadamu inakadiriwa kuwa na ukubwa wa futi za mraba 14 hadi 18 kulingana na umri, jinsia yake, urefu na uzito pia.

Wapo baadhi ya wanasayansi walikwenda mbali zaidi na kusema, ngozi hufikia futi za mraba 20 lakini baadaye walionekana hawako sahihi sana kwa kuwa japo ni kazi ngumu kumpima binadamu ukubwa wa ngozi bila kumchuna, lakini uhakika hupatikana kwa kumpima urefu, uzito, kujua umri wake na jinsi yake tu, japo likichukuliwa karatasi jepesi ila gumu na kumvirigishia mtu kwa kuligundisha kila sehemu ya mwili wake akiwa mtupu, basi karatasi hilo likitolewa, likakatwa vipande na kuunganishwa, hupatikana jibu la ukubwa wa ngozi yake kwa usahihi zaidi.

Unene wa ngozi huzidiana pia katika maeneo tofauti ya mwili wa binadamu kwa mfano, ngozi ya mgongoni ni nene zaidi ya iliyopo kifuani huku usoni kukiongoza kwa kuwa na ngozi nyembamba katika kope kuliko sehemu zote mwilini.

Ngozi sio kama viungo vinavyoishi ndani ya mwili wa binadamu kama vile moyo, ubongo, mapafu n.k, bali ngozi ni nguo tuliyovishwa na muumba mwili mzima yenye uzito unaokadiriwa kuwa kati ya kilo takribani 4 hadi 6.

Bila kuwa na nguo hii, tungeonekana kama roboti maana viungo vingi vya mwili kama mifupa, mishipa na vinginevyo vingekuwa hadharani na tungekuwa tunafuka vitu vingi toka mwilini. Ukiachana na hilo, ngozi inafanya kazi nyingi sana kwa faida ya maisha ya binadamu.

Ngozi hufanya kazi ya kukinga joto la ziada toka nje, kuzuia miale ya jua na kemikali zisiharibu viungo muhimu mwilini, pia huzuia bacteria wasitudhuru kirahisi.

Ukiacha hilo, ngozi huzalisha vitamin D ambayo humsaidia binadamu kuyafanya madini ya kalisi (calcium) yaifanye mifupa kuwa imara.

Lakini ngozi pia hutoa msaada mkubwa wa kuupa ubongo taarifa za mambo yanayouathiri mwili kwa nje na pia, ngozi hutoa taarifa kwa madaktari kuhusu magonjwa anayougua binadamu kama malaria, ngozi inaposhika joto na maradhi mengine mengi.

Yote haya ngozi huyafanya kwa kuwa ngozi imetengenezwa katika sehemu kuu tatu ambazo ni ‘Epidermis’ ambayo ni ngozi ya nje tuionayo na kazi yake kubwa ni kuzalisha seli mpya tunazoziharibu, kuifanya ngozi isipoteze rangi na baadhi ya seli zake ni sehemu ya kinga ya mwili inayolinda maradhi.

Sehemu ya pili ya ngozi ni ile ya kati iitwayo ‘Dermis’, hii hufanya kazi nyingi zaidi ikiwa ni pamoja na kumfanya binadamu atokwe na jasho linalotengenezwa na ‘sweat glands’ kutokana na sumu za mwili na hulitoa kupitia mirija iitwayo ‘pores’ kuja nje ya mwili.

Dermis ni ngozi inayotunza mishipa ya fahamu ambayo humfanya mtu awe na hisia kwa kuwa mishipa hiyo hupeleka taarifa kwenye ubongo. Dermis pia hutengeneza nywele na vinyweleo, hutengeneza mafuta yanayolainisha mwili na pia husafirisha damu kwenda kwenye sehemu zote za ngozi mwilini.

Sehemu ya tatu ya ngozi ni ile ya ndani iitwayo ‘Subcutaneos fat’ ambayo ina tishu maalumu zinazo iunganisha ngozi na misuli pamoja na mifupa mwilini. Sehemu hii ndio inayokuwa na mishipa mikubwa ya damu inayotoka kwenye  ngozi na kusambazwa sehemu nyingine za mwili huku ikirekebisha kiwango cha baridi, joto na maumivu ambayo binadamu huyasikia kutoka nje na ndani ya mwili.

Lakini pia hiyo ni sehemu ya ngozi inayotunza sehemu kubwa ya mafuta ambayoo huyaviriga katika mishipa na mifupa ili iwe imara.

Ngozi yenye afya ni ipi?

Kwa kawaida ngozi laini, nyororo, yenye unyevu na iliyobana mwili bila kulegea huku ikiwa na mng’aro wa kuvutia, ndio ngozi yenye afya njema na bora.

Kila tunapoongezeka umri sote tunagundua kuwa vitu hivyo hupotea taratibu au haraka pengine kutokana na namna tunavyoishi, tunavyokula na hata tunavyoshughulika na utunzaji wa ngozi zetu.

Ila unapoona ngozi yako imepoteza sifa hizo hapo juu, unatakiwa uchukue hatua za ziada ili kuirudisha katika hali yake iweze kukutumikia vizuri.

 Ngozi inaweza ikapoteza ulaini na unyororo halafu mng’aro pia ukapotea kwa sababu nyingi tu, ila chache kubwa ni kuishi katika maeneo yenye baridi kali, kushinda katika jua kali kwa muda mrefu kila siku,  kutumia sabuni na mafuta yenye kemikali hatari, kuoga maji ya moto kila siku bila sababu za msingi, kujikuna kwa kucha mara kwa mara, kuugua maradhi mazito kwa muda mrefu, kutumia dawa kali kwa matibabu pamoja na unywaji wa pombe unaopitiliza sambamba na kuvuta sigara.

Ngozi kavu isiyovutia

Hata hivyo, bado kuna tatizo la ngozi kutoubana mwili na kulegea (skin firmness) ambalo huwakuta zaidi wazee na kulegea kwa ngozi huko husababisha pia makunyanzi yaani ‘Wrinkles’ ambazo huwaudhi sana bila kujua zinaweza kudhibitiwa kwa namna gani.

Kadiri mtu anavyozeeka, ngozi hupoteza baadhi ya seli zake kama ‘collagen’ na ‘elastin’ na hata tindikali iitwayo ‘hyaluronic acid’ pia hupungua na kuifanya ngozi ilegee na kutengeneza makunyanzi na kusinyaa kisha baadaye hupoteza hata rangi nzuri ya ujana.

Ufanyeje kuilinda ngozi yako?

Kuoga mara kwa mara na kuipaka mafuta ngozi ndicho kitu cha msingi na muhimu kwa mtu yeyote anayependa kuwa na ngozi yenye afya na inayovutia.

Hakika, ukiongeza safari za kuoga na kupaka mafuta tu, hutakawia kujiona umebadilika kwa muda mfupi, hata wiki mbili hutofika kwa kuwa kuzeeka, kufadhaika mara kwa mara (stress) hali mbaya ya hewa na mazingira pamoja na vipodozi na sabuni zenye kemikali hatari, uharibu ngozi hasa maeneo ya usoni, shingoni na kifuani ambayo ndiyo maeneo yanayoathirika kwa haraka zaidi kuliko mengine.

Tumia mafuta ya nazi

Mafuta ya nazi ni kimbilio la watu wengi wanaotaka kutengeneza ngozi iliyoharibika kwa maradhi na vidonda.

Wapo watu wengi wanaoyatumia mafuta hayo kupaka kwenye nywele ili kuua mba kwa muda mfupi.

Kuna kabila linawaweka ‘wanawali’ ndani kwa muda mfupi tu wakiwachua kwa machicha ya nazi, na mabinti hao hutoka wakiwa wamependeza na wameng’ara bila madhara  na wengi wao mpaka hii leo hawajui sayansi iliyojificha nyuma ya machicha hayo ya nazi.

Hii ni kutokana na nazi kuwa na tindikali ziitwazo ‘MCFA’ yaani Medium Chain Fat Acids ambazo hupambana na bacteria, virusi na fangasi wote waliopo juu ya ngozi huku ikiondoa pia seli za ngozi zilizokufa na kumfanya mtu aonekane mwenye mvuto tena.

Zipo kampuni na wajasiriamali wengi ambao hutengeneza mafuta ya nazi na kuyauza madukani.

Lakini ni vema mtu akayatengeneza mwenyewe kwa kuwa wengi sio waaminifu, kwani huweka aina nyingine ya mafuta na kukuvutia kuyanunua kwa kuongeza kiasi kidogo cha mafuta halisi ya nazi ili kupata harufu tu.

Hata hivyo, wengi huwa hawaipendi harufu kali ya mafuta ya nazi hivyo wanaweza wakatumia mafuta ya mmea wa jojoba ambao hufanya kazi takriban sawa na mafuta ya nazi, ila hayana madhara.

Tumia mafuta ya Jojoba

Mafuta ya mmea wa jojoba si maarufu sana hapa nchini. Ni maarufu nchini Arizona, Mexico, California na Asia ya Kusini hasa India. Jina jingine huitwa ‘Simmondsia Chinensis’ au ‘Hohoba’ na huzalisha mbegu zinazokamuliwa mafuta ambayo hayana rangi wala harufu.

 Mafuta haya yanashika chati Duniani kote kwa kufuta makunyanzi ya uzee na makovu, kulainisha ngozi kavu, kuponya ngozi iliyoharibika kwa vipodozi vikali na kurudisha mng’aro wa ngozi kwa muda mfupi kwa kuwa huanza kufanya kazi ndani ya saa sita toka mtu anapoanza kuyatumia tena bila madhara yoyote.

Imeandaliwa na DkJohn Haule (Dietician)  +255 768 215 956

Facebook/john.haule4