Fahamu hatua za kumchukulia mkopaji msumbufu

Muktasari:

Wakopaji wasumbufu wapo wa aina mbili. Aina ya kwanza ni wale ambao wanawasiliana na wewe na kuendelea kukupa ahadi kuwa watalipa.

        Mkopaji msumbufu huwa hataki kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa mkataba au makubaliano. Wakati anakopa hutumia lugha nzuri ya upole na unyenyekevu, lakini baada ya kupata mkopo hubadilika na kuwa mbogo; hasikii, haelewi, hapatikani, hubadilisha njia na wakati mwingine anaweza hata kubadilisha namba ya simu.

Wakopaji wasumbufu wapo wa aina mbili. Aina ya kwanza ni wale ambao wanawasiliana na wewe na kuendelea kukupa ahadi kuwa watalipa.

Ukipiga simu wanapokea, ukiwaita wataitika na watatoa ahadi za kulipa wakati mwingine hata kwa maandishi lakini cha ajabu ikifika tarehe waliyoahidi hawaonekani, hawapatikani na hawatimizi ahadi zao. Hawa ni watu wa ahadi zisizotekelezeka kila siku.

Aina ya pili ya mkopaji msumbufu ni yule ambaye mnawasiliana, mnaonana na kuongea wakati anapohitaji mkopo tu, akishapata haumwoni tena. Hafiki tena kutoa taarifa yoyote, haleti marejesho yoyote na akileta ni kwa mbinde au kwa kubabatizwa na unaweza kukuta marejesho yenyewe hayajatimia.

Akipigiwa simu hapokei. Atapokea tu akiona namba ngeni na akishaigundua tu kuwa ni yako hapokei tena. Hubadilisha njia, majina kwenye mitandao ya kijamii na anaweza hata kuhama anapoishi.

Usipofahamu hatua unazopaswa kuchukua dhidi ya mkopaji msumbufu unaweza kuugua. Wakati mwingine hatua unazozichukua badala ya kukusaidia kupata fedha zako zinaweza kukufanya uingie kwenye gharama kubwa zaidi hivyo kuongeza hasara.

Unaweza kukuta mkopaji huyo anatumia udhaifu wa hatua ulizozichukua dhidi yake ili apate sababu za kumfanya asilipe deni au akufanye umlipe fidia badala ya yeye kulipa deni.

Kwa kutambua uwepo wa wakopaji wasumbufu, unashauriwa kuchukua tahadhari mapema kabla hujamkopesha mtu kwa kufahamu mambo ya msingi yanayomhusu ikiwamo mikataba, anwani, mawasiliano na makazi yake.

Vilevile, unapaswa kufahamu biashara au shughuli anayofanya, mahali anapofanyia kazi, watu wake wa karibu na mawasiliano yao, dhamana aliyoweka, vyanzo vyake vya mapato, familia yake, viongozi wake mtaani, wadhamini wake na taarifa nyingine za msingi.

Umuhimu wa taarifa hizi utauona pindi atakapoanza kuwa msumbufu. Taarifa hizo ndizo zitakazokusaidia kufahamu hatua za kuchukua. Zitakuwezesha kufahamu wapi uanzie na nini kifuate.

Jihadhari sana kwenda nyumbani kwa mkopaji msumbufu na kuanzisha vurugu, kutumia lugha za matusi, udhalilishaji, uharibifu wa mali au hatua zozote zilizo kinyume cha sheria. Epuka kuchukua sheria mkononi kwani itakugharimu.

Jambo la msingi ni kumpata mhusika na kusikiliza kauli yake kuhusiana na malipo ya mkopo. Kumbuka bado una wajibu wa kutunza heshima ya mkopaji wako hivyo haitapendeza kama hujamtaarifu na ukatoa taarifa kwa watu wengine au kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari au kukamata mali yake, utakuwa umevuka hivyo kukugharimu.

Baada ya kufanya jitihada za kumtaarifu unaweza kuwataarifu wadhamini wake na kuwaeleza hali halisi ikiwemo hatua unazopanga kuchukua endapo fedha hizo hazitalipwa ndani ya muda ulioutoa.

Ni muhimu taarifa kwa mkopaji zikatolewa kwa barua au notisi ya madai ambayo inaweza kuandikwa na wewe mwenyewe au wakili ili kuleta uzito wa madai yako.

Baada ya jitihada za kumpata kushindikana na hatua yoyote kutochukuliwa, pitia vipengele vya mkataba wa mkopo ili ujiridhishe juu ya haki zako.

Mkataba unaweza kueleza kuwa haki yako ni riba kuongezeka ndani ya kipindi fulani na baada ya hapo kuuza mali.

Unaweza kukabidhi jukumu la kudai deni lako kwa dalali wa mahakama kuchukua hatua dhidi ya mdaiwa ikiwamo kukamata mali zake na kuzipiga mnada ili kufidia deni unalodai.

Endapo taratibu za kumtumia dalali zinaweza zisizae matunda ipo hatua nyingine ya kufungua kesi mahakamani ili itoe hukumu ya malipo ya fedha hizo pamoja na gharama zilizotumika kuendesha kesi hiyo au kudai deni hilo.

Unaweza kuiomba mahakama imfunge mdaiwa endapo atashindwa kulipa deni lako.

Kuhusiana na dhamana iliyowekwa ya mali inayohamishika kama vile gari au mali nyingine yoyote baada ya kumtaarifu mkopaji kwa barua au notisi na kwa kuzingatia vipenglele vya mkataba wa mkopo unaweza kuvitaifisha kisha kuviuza ili kufidia fedha unazodai.

Hata akikimbilia mahakamani, atawajibika kukulipa fedha zako na gharama za kesi.

Mwandishi anapatikana kwa namba 0755 545 600.