Fahamu wakati na faida ya kutumia dawa za ziada

Food supplements ni suluhisho kwa wenye upungufu wa baadhi ya virutubisho ili kuwarudisha kwenye hali ya kawaida.

Muktasari:

DONDOO

Lishe kamili ni hitaji la kila binadamu ili kujihakikishia siha njema. Wagonjwa, watoto, wazee na wajawazito ni makundi yanayokabiliwa na changamoto hii.

Food supplements ni suluhisho kwa wenye upungufu wa baadhi ya virutubisho ili kuwarudisha kwenye hali ya kawaida.

Kabla ya kutumia vyakula hivi, inashauriwa kupata maelekezo ya kutosha ili kuchagua itakayokidhi mahitaji ya mhusika.

Ni kawaida kusisitizwa kula kabla ya kumeza au kunywa dawa ambayo daktari ameipendekeza kwa mgonjwa.

Inapotokea mgonjwa ni mtoto, mzazi au mlezi huagizwa kuhakikisha amemlisha chakula cha kutosha  kabla hajampa dawa husika.

Tumezoea kusikia kauli hizi kutoka kwa madaktari wanapotoa maelekezo ya matumizi ya dawa kwa wagonjwa.

Lakini, swali la kujiuliza ni vyakula gani tunavyopaswa kuwapa wagonjwa kabla ya hawajatumia dawa hizo?

Watu wengi nchini na hata duniani hushindwa kulijibu swali hili.

Katika hali ya kawaida, binadamu tunakula vyakula kila siku ili tushibe, tujenge mwili na tujikinge na maradhi. Vipo vyakula vya aina nyingi; wanga, protini, vitamini na madini pia.

Maisha yameendelea kuwa hivyo kwa karne nyingi tukiishi kwa mazoea haya, lakini katika karne iliyopita, mambo yamegeuka.  Katika miaka ya 1990 kumegunduliwa aina mpya ya vyakula ambavyo viitwavyo ‘food supplements’ ambavyo tayari vimeanza kuenea katika maduka makubwa au maarufu supermarkets na yale ya dawa.

Food supplements ni tibalishe kama zinavyofahamika kwa wataalamu wa afya. Hii ni baada ya kuonekana kuwa vyakula hivi vina uhusiano mkubwa na dawa za kutibu maradhi mbalimbali tunazoandikiwa na madaktari hospitali.

Vyakula hivi vimeonekana vinasaidia dawa kufanya kazi vizuri na kwa haraka pale mgonjwa anapotumia pamoja na tiba za hospitali, yaani conventional medicines.

Vyakula hivi pia vilipewa jina la tibalishe ili kuonyesha kuwa siyo dawa, kwani watengenezaji wake walishaanza kuvinadi kama dawa halisi huku wakisisitiza kuwa vinaponya na kutibu maradhi kitu ambacho kilihofiwa na mamlaka za tiba, kuwa watumiaji wangepuuza dawa halisi na kuvitegemea.

 Kisayansi, vina uwezo tu wa kusaidia tiba rasmi zinazopendekezwa na daktari, lakini siyo kutibu kama ilivyodaiwa na watengenezaji hao.

Hivyo, ukinunua tibalishe na kusoma maelezo yake, utakutana na maneno yasemayo ‘bidhaa hii haitibu wala haiponyi na siyo mbadala wa dawa ila msaada wa tiba’ kwa kuwa hakuna mtengenezaji aliyeruhusiwa kuingiza sokoni bidhaa yake bila kuwa na maneno hayo na lazima yasomeke kiurahisi.

Vyakula vya ziada

Tunapoumwa hata kama ni ugonjwa wa kawaida, hakuna anayepewa chakula hata kiwe kizuri namna gani akala kwa furaha na akakimaliza.

Hii ni kwa sababu mgonjwa hupoteza hamu na nguvu ya kula. Kwa kuliona hilo, ndipo watafiti wa tiba walipokuna vichwa na kuja na jibu la vyakula mbavyo vingewafaa wagonjwa.

Baada ya utafiti wao, walikuja na maoni kwamba vyakula tulavyo kila siku ni vya ‘kiada’ na tibalishe ni ‘ziada.’

Food Supplements, hizi zilianza kunadiwa kuwa ni dawa duniani kote kutokana na kutengenezwa kwa kulenga maradhi ya aina mbalimbali, lakini kwa kawaida huwa ni mchanganyiko wa vitamini, virutubisho (nutrients), madini (minerals) na tindikali (Acids) za aina tofauti kulingana na maradhi tofauti.

Ukiacha hilo, tibalishe zinatengenezwa katika namna ambayo zinaonekana kama dawa halisi kwa kuwa zipo katika muonekano wa vidonge, maji (syrups), unga hata zenye vidonge vya vifuniko vya plastiki yaani ‘capsules.’

Utata wa utambuzi wa food supplements kama dawa, huja pale mgonjwa anapotumia na kujikuta amepata nafuu huku mamlaka za tiba zikiendelea kukataza wagonjwa kuzitambua kama dawa.

Aina

Nchini kuna kampuni nyingi zinazoingiza tibalishe na kuzisambaza katika maduka ya vyakula au dawa na Watanzania wengi huzinunua na kuzitumia.

Lakini tatizo linakuja, namna mgonjwa anavyoweza kuzitambua bidhaa hizo, hasa ikizingatiwa kuna uhaba wa wataalamu wa tiba na lishe nchini, hivyo kuchangia watu wengi kukosa elimu ya kina.

Kutokana na changamoto hiyo, wengi hununua na kutumia vyakula hivi kwa utashi wao binafsi na kutopata mafanikio kwa kuwa hufanya hivyo kimakosa na kujikuta wanachagua bidhaa isiyoendana na ugonjwa anaougua. Ipo mifano mingi ya vyakula hivi.

Nutrishake

Hii ni aina ya tibalishe iliyo kwenye muonekano wa unga ambayo ni chakula kinachomfaa mtu yeyote anayeumwa kwa muda mrefu na hana hamu ya kula.

Hii ni lishe yenye ladha ya maziwa ambayo mgonjwa hukoroga unga wake katika glasi ya maji na kuinywa.

Mgonjwa akiimaliza glasi hiyo, kisayansi anafanana na mtu aliyekula milo yote mitatu kwa siku nzima.

Wataalamu huiita ‘Recommended Daily Allowance’ kwa kifupi RDA. Wagonjwa wengi hupoteza maisha kutokana na njaa isababishwayo na kushindwa kula kwa muda mrefu.

Ukiacha nutrishake, zipo bidhaa zinazofana nayo kama ensure, lifegain, powerfood na replace.

Immune complex

Hii ni aina ya tibalishe iliyo kwenye mfumo wa vidonge ambavyo huwa msaada kwa watu wanaougua maradhi ya muda mrefu kiasi cha kwenda hospitalini mara kwa mara.

Tibalishe hii husaidia kuimarisha kinga za mwili na kusaidia kupona haraka. Angalizo ni kuwa, hizi siyo dawa ila ni msaada kwa dawa anazopewa mgonjwa.

Ukiiacha hii, zipo aina nyingine tofauti za aina hii kama vile immunace.

Osteo Care

Tayari Wizara ya Afya nchini imeshaiingiza katika mtalaa wa tiba nchini na zinapatikana kwenye hospitali za Serikali na binafsi.

Bidhaa za Osteo zina majina mengi kulingana na kampuni inayozitengeneza. Hivyo, utakutana na Osteo care, Osteo eze, Osteomin na nyinginezo nyingi ambazo hazina majina yanayofanana na hizo kama Flexa ambazo ni mahususi kwa wenye maumivu ya viungo, mgongo na magoti pamoja na maungio ya viungo kwa ujumla.

Ni msaada mkubwa kwa waliopata ajali pamoja na wazee hasa wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 50 ambao mifupa yao huwa dhaifu.  Bidhaa hizi huwa katika mfumo wa  vidonge, jeli za kuchua au juisi japo ufanisi wa aina moja na nyingine hutofautiana pia.

Visionace

Ni kawaida hivi sasa kuona watu wengi wamevaa miwani hasa wafanyakazi hata katika umri mdogo.

Kwa kawaida, macho hutakiwa kupepesa kila baada ya sekunde mbili hadi tano ili yajisafishe. Kwa kulitambua hilo, tibalishe za kurekebisha tatizo hilo zipo sokoni japo hazina uhakika wa kurejesha uwezo kwa waliowahi kufanyiwa ukwanguaji wa ngozi ya jicho.

Hizi nazo zipo za aina nyingi.

Kidz Vitachewz

Ukuaji wa watoto ni changamoto kubwa kwa wazazi hasa anapokataa kula kiasi cha kupoteza uzito wake hata kuanza kushambuliwa na maradhi.

Kidz Vitachewz na nyinginezo ni tibalishe zinazotumika kutatua matatizo ya afya za watoto.

Pregnancy Care

Hizi ni tibalishe zinazowahakikishia wajawazito kujifungua salama.

Inafahamika kuwa wajawazito wengi huwa hawapati lishe ya kutosha, hivyo kutishia afya zao na watoto walionao tumboni.

Hii imetengenezwa mahususi kwa ajili ya kumpatia mjamzito kila kinachohitajika mwilini katika kipindi hicho.

Mwandishi ni mtaalamu wa lishe na tiba. Anapatikana kwa 0768 215 956