Fainali za Kombe la Dunia zimewadia, wachezaji watumie fursa hiyo kujifunza

Muktasari:

  • Ujerumani imekwenda Russia wakiwa ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo, baada ya kutwaa mwaka 2014 katika fainali zilizochezwa Brazil.

Fainali za Kombe la Dunia zimeanza kutimua vumbi nchini Russia na timu 32 za mataifa mbalimbali duniani, zinamenyana kuwania ubingwa.

Ujerumani imekwenda Russia wakiwa ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo, baada ya kutwaa mwaka 2014 katika fainali zilizochezwa Brazil.

Michuano hiyo inajumuisha wachezaji 23 bora wa kila timu ambao wameonyesha viwango bora katika klabu zao kabla ya kuteuliwa kuwakilisha nchi zao.

Idadi kubwa ya wachezaji wanaokwenda Russia kushindana, wanazitumikia klabu zinazotamba katika medani ya soka Ulaya.

Hawa ni wachezaji bora ambao walipata nafasi ya kuzitumikia timu zao katika vikosi vya kwanza hatua iliyowavutia makocha wa klabu hizo.

Kimsingi fainali za Kombe la Dunia zinazochezwa kila baada ya miaka minne, ni michuano yenye hadhi kubwa duniani.

Kipindi cha michuano hiyo dunia nzima ‘inasimama’ kushuhudia mafundi wa soka wakichuana kutetea mataifa yao.

Mbali na kushuhudia ufundi wa kila aina kutoka kwa nyota wanaotamba duniani, michuano hiyo inatoa fursa kwa wachezaji wanaocheza soka ya ridhaa kujifunza mambo mbalimbali ndani na nje ya uwanja.

Pia ni fursa nzuri kwa wachezaji wa Tanzania kujifunza mbinu za uchezaji, nidhamu na aina ya ufundi ambao unahitajika kwa mchezaji aliyekamilika.

Tukirejea katika soka yetu ya bongo, nidhamu kwa wachezaji wengi ni tatizo na imekuwa ikiporomosha viwango vya ‘nyota’ wengi ambao walianza vyema kabla ya kupotea.

Wachezaji wengi hasa wanaocheza Ligi Kuu Tanzania Bara wanashindwa kujitambua na hawajui wanahitaji nini na kwa wakati gani.

Ingawa neno nidhamu lina wigo mpana, lakini wachezaji wetu wameshindwa kufuata miiko na misingi ya mchezaji.

Idadi kubwa ya mastaa wanaocheza Ligi Kuu wameshindwa kujitofautisha na vijana wanaocheza mchangani hatua inayochangia kuua mapema vipaji vyao.

Kuna ‘wimbo’ maarufu wa misumari unaotawala vinywa vya wadau wengi wa soka mchezaji anaposhuka kiwango chake ghafla hasa baada ya kuzitumikia kwa muda mfupi klabu kongwe za Simba na Yanga.

Wapo baadhi ya wachezaji viwango vyao vimepotea ghafla baada ya kucheza kwa muda mfupi Simba na Yanga ingawa waling’ara katika klabu zisizokuwa na majina makubwa.

Baada ya kuzimika ghafla kama mshumaa ndipo wimbo wa misumari unapoanza kuimbwa kwa nguvu zote ukichagizwa na mchezaji husika akitaka kuiaminisha jamii kwamba kuporomoka kiwango chake kuna mkono wa mtu.

Imani za ushirikina ndizo zimezaa neno misumari, mchezaji anaposhindwa kucheza kwa kiwango bora alichokuwa nacho awali, anahisi amefanyiwa ndumba ili kumdhoofisha.

Hata hivyo, ukichunguza kwa makini utabaini kuporomoka kiwango kwa mchezaji ni matokeo ya kukosa nidhamu baada ya kujiunga na Simba, Yanga au kupata namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza kwa timu yoyote.

Uzoefu unaonyesha idadi kubwa ya wachezaji waliopata umaarufu, lakini waliporomoka ghafla imetokana na mfumo wa maisha wanayoishi baada ya kupata jina.

Matukio ya ulevi wa kupindukia na starehe kadha wa kadha ni sababu kubwa inayoua vipaji vya wachezaji wetu ambao wanashindwa kujitambua.

Hapa hakuna sababu ya mchezaji kumtafuta uchawi kwa kisingizio cha kupigwa misumari. Bila shaka mchawi ni yeye mwenyewe kwa sababu ameshindwa kujitunza kwa kufuata misingi ya mchezaji anayotakiwa kuishi ili kulinda kiwango chake.

Kwa mantiki hiyo ujio wa fainali za Kombe la Dunia ni wakati mwafaka kwa wachezaji kuiga na kusimamia mazuri yanayofanywa na wachezaji wa kimataifa ndani na nje ya uwanja.

Kwa bahati njema michuano hiyo itaonyeshwa ‘live’ na televisheni tofauti nchini hivyo ni nafasi nzuri kwa wachezaji wetu kujifunza kutoka kwao.

Kupitia fursa hiyo, ni matarajio ya wadau wengi watawaona wachezaji wetu wanaocheza katika madaraja tofauti wakifuatilia kwa makini michuano hiyo kupitia televisheni au vifaa vingine vya kielektroniki ambavyo vitaonyesha fainali hizo.

Hatutegemei kuwaona ‘mastaa’ wetu wakitumia michuano hiyo kuiga mitindo ya unyoaji wa nywele au katika mavazi badala ya kujikita katika kujifunza mbinu mbalimbali za uchezaji.

Viongozi wa klabu zote nchini wana wajibu wa kuendelea kutoa elimu kwa wachezaji kuhusu umuhimu wa fainali hizi kwa kuwa watapata fursa nzuri ya kujifunza mambo ya kiufundi kutoka kwa nyota wanaoshindana Russia.