Fanya haya kuepuka tumbo kujaa gesi

Dk Christopher Peterson

Tatizo la tumbo kujaa gesi linaelezwa kuwa husababishwa na mtu kumeza chakula pamoja na gesi inayotolewa na vyakula mbalimbali. Mara nyingi mtu uhisi tumbo kujaa wakati wote. Kila mmoja amewahi kupata hali hii mara kadhaa kwa nyakati tofauti.

Japo ni hali ambayo kwa kawaida inatokana na ulaji kupita kiasi, lakini kuna baadhi pia hawana tabia ya kula kupita kiasi, lakini bado wanakutana na hali hii ya kuhisi tumbo kujaa wakai wote. Hivyo ni vema tukafahamu kuwa, sambamba na tabia za ulaji, lakini kuna sababu zingine zinazochangia hali hii. Miongoni ni mwili kuhifadhi kiwango kikubwa cha maji au kutokana na matatizo mengine ya afya. Inaweza ikiwa ni dalili ya vidonda vya tumbo ambayo huambatana na uwapo wa gesi tumboni hivyo kuongeza ujazo wa tumbo na matatizo mengine yanayojitokeza kwenye mfumo wa chakula. Sababu nyingine zinazochangia kujaza tumbo na kusababisha kero ni “premenstrual syndrome”. Hili ni jina la kitaalamu linalotafsiri baadhi ya matatizo ya kiafya kama ya uchovu, maumivu na hata kichefuchefu yanayojitokeza kwa mwanamke anapokaribia kuingia kwenye mzunguko wa hedhi.

Premenstrual syndrome pia inasababisha mwili kuhifadhi kiwango kikubwa cha maji kutokana na mabadiliko ya mfumo wa homoni kwa wakati huo. Hivyo ndani ya kipindi hiki, ni kawaida kwa mwanamke kuhisi tumbo lake limejaa wakati wote. Sababu nyingine ni ulaji wa chumvi nyingi. Mwili wa binadamu unahitaji chumvi, lakini mara nyingi hujikuta akitumia zaidi ya kiwango kinachostahili kuingia mwilini.

Chumvi ikizidi mwilini, inaupa mfumo wa mwili kuhifadhi kiwango kikubwa cha maji na chumvi, pia inaweza kusababisha matatizo mengine makubwa ya kiafya kama vile shinikizo la juu la damu. Kwa siku za karibuni, matumizi ya vyakula vilivyosindikwa yameongezeka maradufu na ni muhimu kuzingatia kuwa, asilimia kubwa ya vyakula vilivyosindikwa vimewekwa kiasi kikubwa cha chumvi na hata kama usipohisi ladha ya chumvi kwenye vyakula hivyo, haina maana kuwa havijawekewa chumvi. Ni vema kusoma kwa umakini vibandiko vilivyowekwa kwenye vyakula hivyo kusudi kujua kiasi cha “sodium” kilichopo kwenye vyakula hivyo. Unywaji wa soda na vinywaji vingine vya kiwandani pia unachangia kulifanya tumbo muda wote liwe limejaa.

Soda na vinywaji vingine kama bia, shampeni au vinavyotumika kuongeza nguvu ya mwili vimewekewa kiasi fulani cha gesi katika utengenezaji wake. Unapokunywa moja ya vinywaji hivi vinaenda kuongeza ujazo kwenye mfumo wako wa chakula. Wakati ukiendelea kunywa, unaweza kutoa kiasi kidogo cha gesi, wengi wamezoe kuita kudukua au kubeua. Hii inatokea pale unapokunywa kinywaji chenye gesi na ghafla inakujia hali kama ya kucheua, lakini kinachotoka ni gesi.

Hii haimaanishi kuwa kwa kufanya hivyo, gesi yote uliyoipata kutoka kwenye kile kinywaji imetoka, hapana. Kiasi kikubwa cha gesi hiyo huendelea kubakia kwenye utumbo wa chakula na inaendelea kubakia ndani ya utumbo hadi hapo itakapo toka taratibu aidha kwa njia ya mdomo au kwa njia ya haja kubwa. Kukosa haja kubwa ni sababu nyingine inayochangia tumbo kujaa. Mwili una mfumo wa mmeng’enyo wa chakula mwilini. Kazi kuu ya mfumo huu ni kukichakata chakula chote kinachoingia mwilini ili kutenganisha kati ya virutubisho vya mwili na makapi. Makundi haya yote mawili yanapatikana kwenye kila chakula. Hivyo mfumo wa mmeng’enyo wa chakula unaondoa makapi yote tumboni kupitia njia ya haja kubwa. Kwa kawaida mtu anatakiwa apate haja kubwa mara mbili kwa siku, yaani ndani ya kipindi cha saa 24. Japo wengi wamekuwa wakipata haja kubwa mara moja kwa siku, haina madhara kwa afya.

Lakini kukosa haja kubwa kwa zaidi ya siku moja kunaweza kuashiria tatizo lingine la afya licha ya kusababisha tumbo kujaa. Ni vema kuzingatia sababu zinazosababisha kukosa haja kubwa kama kutokunywa maji ya kutosha, ulaji wa baadhi ya vyakula ambavyo havina nyuzi lishe na hata msongo wa mawazo ili kuweza kukabiliana nazo. Nashauri pia kujenga tabia ya kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara na kupata dawa za kusaidia kupata haja kubwa lakini kwa ushauri wa mtoa huduma wa daktari.