Fanya mazoezi haya chumbani au ofisini

Muktasari:

  • Faida kubwa ya kufanya mazoezi ni kusaidia kuupa mwili afya njema, hivyo kuuepusha na maradhi yasiyoambukiza ikiwa-mo kisukari, magonjwa ya moyo, kiharusi na unene uliokithiri.Mazoezi hayo ni yale mepesi ambayo huju-likana kitaalamu kama Aerobic exercise; yaani ufanyaji wa mazoezi mepesi huku ukiende-lea kupata hewa safi ya oksijeni pasipo kusiti-sha upumuaji.

Yapo mazoezi mepesi yanayoweza kufanyika ukiwa nyumbani au ofisini ambayo ni rahisi kuyafanya ili kuweza kuwa na mwili imara wenye afya njema.

Unapokuwa nyumbani kwako au ofisini jenga mazoea ya kuushughulisha mwili wako na mambo yanayoufanyisha kazi mwili ili misuli ya mwili kwa ujumla ifanye kazi.

Unapoamka tu asubuhi cha kwanza unapaswa kukaa angalau dakika tano huku ukivuta pumzi ndefu na kutulia, kisha ukaanza kuunyoosha viungo vya mwili wako kwa dakika kadhaa.

Kisha unaweza ukatumia chumba unacholala kutembea umbali mfupi mara nyingi, kwenda na kurudi. Anza kidogo kidogo ili kujenga mazoea mpaka iwe ni kawaida yako.

Tumia nusu saa kila siku ukiwa ndani kwako kwa kutembea chumbani kwako au nje ya nyumba yako ukawa unazunguka maeneo hayo. Unaweza pia ukachanganya na mazoezi mengi ikiwamo kuruka kamba au kuruka ruka mara nyingi ukiwa ndani kwako.

Kama uko ofisini unaweza ukajenga mazoea kwa kutembea, unaweza ukaepuka kutuma mtu mwingine kama vile kuchukua kikombe kwa ajili ya kahawa unaweza ukatembea mwenyewe kufuata kilipo.

Badala ya kutumia zaidi rimoti kuwasha TV, AC na feni unaweza ukawa huitumii ukawa unakwenda kuwasha kwa kutembea kila mara unapohitaji kubadili chaneli au kuongeza joto au kuongeza kasi ya feni.

Tumia ngazi kupandia ghorofani, unaweza ukajenga mazoea ya kupandisha ngazi za ofisini au nyumbani angalau kwa dakika 20 kila siku. Epuka kutumia lifti badala yake tumia ngazi za kawaida.

Matembezi ya umbali mfupi kama vile kwenda ofisi ya jirani unaweza pia ukayafanya ili kuushugulisha mwili.

Kama unatumia usafiri wa kawaida unaweza ukawa unashukia mahali ambapo ni mbali na kwako ili kuweza kutumia muda huo kutembea kufika kwako.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo ukiyafanya kwa pamoja unajikuta umeufanyisha mwili mazoezi mepesi pasipo kutumia gharama yoyote. Mambo haya yanawafaa watu ambao wana umri mkubwa, wanaotingwa na kazi nyingi kiasi cha kushindwa kushiriki mazoezi na wajawazito.

Inashauri kujenga tabia ya kufanya mazoezi ya mara kwa mara yakutembea kilomita mbili angalau kwa siku dakika 30-45 mara tano kwa wiki.