KONA YA MAKENGEZA : Fumbia fimbo za walimu

Muktasari:

  • Watu walipoozwa na asali hadi wakasinzia tena. Lakini awamu hii haina utani. Wakiona jambo ni sahihi, hakuna kusahihisha ni kusonga mbele moja kwa moja bila asali wala sukari ya Kilombero. Ndiyo.

Waishiwa kwa malumbano siwawezi siku hizi. Nashawishika kuamini kwamba awamu iliyopita ilifunika mikinzano kwa ahadi tamu kuliko asali, bila ulazima wa kugeuza ahadi kuwa vitendo.

Watu walipoozwa na asali hadi wakasinzia tena. Lakini awamu hii haina utani. Wakiona jambo ni sahihi, hakuna kusahihisha ni kusonga mbele moja kwa moja bila asali wala sukari ya Kilombero. Ndiyo.

Wanaoona uchungu, wafe na uchungu wao. Asali ya nini mbele ya usahihi wa mambo. Kwa njia hii, tofauti za misimamo na mrengo zinajitokeza waziwazi kabisa.

Labda ndiyo maana waishiwa wenzangu nao wanahemka kupita kiasi. Hata supu ya bure haiwezi kuwapooza. Ndiyo maana tuliona wiki jana Mwishiwa Supu na mwishiwa mwenzetu walilumbana vikali kidogo tuamini kwamba mwishiwa mwenzetu atafukuzwa sebuleni au angalau kunyimwa supu kwa kujenga chuki dhidi ya Msupu mwenyewe.

Kwa hiyo tulifurahi kuona kwamba bado yuko nasi wiki hii, licha ya kanuni za msupu za kulinda usupu wake. Safari hii mjadala ulizidi kuwa mkali ingawa mwishiwa Supu hakutaka kulumbana mwenyewe, bali aliwaachia wapambe wake kupamba moto kwa niaba yake huku yeye ametulia tuli. Mmoja akaamka na kumaka:

“Mwishiwa Supu, kwa kweli inabidi kuchukua hatua. Upotoshaji wa mwishiwa msomi wiki jana haukubaliki. Hebu angalia mifano ya mitandao ya ushambenga wiki hii.

Mara picha ya polisi wetu mpendwa akipokea rushwa waziwazi. Kakideo haka kanajenga chuki moja kwa moja dhidi ya watu wanaofanya kazi usiku na mchana kutulinda. Aliyepiga kideo hiki lazima achukuliwe hatua hata kama yuko nje ya nchi.”

Mwishiwa mwingine aliingilia.

“Hivi naomba kuuliza nani anajenga chuki, yule polisi anayekiuka maadili na miiko ya kazi yake katika kuwanyanyasa watu au mtu anayemfichua ili polisi wawaondoe wabaya na kurudishe hadhi yao.”

“Sawa, huyu kweli ameshusha hadhi ya polisi lakini kwa nini awekwe hadharani. Ni njama ya kujenga chuki dhidi ya polisi wote?”

“Sasa kama kuna wehu wanaoamini kwamba polisi wote ni wala rushwa kwa sababu ameonyeshwa mmoja tu, hili ni tatizo lao. Ni kama kuamini kwamba, kwa kuwa mtu mmoja wa kabila fulani ni mwizi, basi wote ni wezi.

Mitazamo finyu. Lakini ili wenzetu wapendwa waendelee kuheshimiwa lazima wawatambue na kuwaondoa wale wanaochafua jina lao kwa vitendo vyao vya hovyo kabla hawajazidi kuharibu jina.

“Hapana. Hapana. Ndiyo maana, iwapo malaika hapatikani maana anapigana na uhalifu mahali pengine, basi hata ibilisi aje alipue mitandao ya hii ya ushambenga.”

“Nakushangaa mwishiwa mwenzangu. Ina maana kwamba iwapo vitendo vya ukatili au uvunjifu wa sheria vinaendelea, visitangazwe hadharani?”

“Kabisa. Wakoloni walisema kisichoonekana na macho hakiumizi moyo.”

“Kwa hiyo watu waendelee kuteswa kimyakimya. Amani yetu ijengwe juu ya ujinga?”

“Si ujinga. Hebu ona kideo kile cha walimu tarajali kumtwanga mwanafunzi. Siku nzima watu wamewatukana walimu wote kutokana na kitendo hicho. Tena huyu aliyepiga kideo afungwe moja kwa moja kwa kosa la kujenga chuki dhidi ya walimu.”

“Duh, mwishiwa mwenzangu, badala ya kuchukia kitendo kile cha kikatili unachukia aliyewafichua watu wanaovunja sheria.”

“Ndiyo. Walimu wangapi wanavunja sheria ya viboko kila siku bila kuchukuliwa hatua? Unataka kila mmoja aanikwe kwenye mitandao ya washambenga?”

“Kumbe na wewe unajenga chuki dhidi ya walimu. Kumbe unajua wanaovunja sheria ni wengi.”

“Acha hizo bwana. Unajua hata na wewe. Hata utafiti wa Serikali ulionyesha kwamba watoto wengi walitaja walimu kama wapigaji wa kwanza na hata wanyanyasaji kijinsia. Nani hajui?”

“Sasa kwa nini hutaki ionekane hadharani? Ikae tu katika taarifa za utafiti? Kwa nini kideo hiki kisiwe chanzo cha kurudisha maadili na sheria.”

“Hapana. Iachie Serikali ipate nafasi ya kushughulikia kimyakimya.”

“Tangu lini Serikali ishughulikie kimyakimya? Bila mitandao ya jamii, kesi zote hizi mbili, ya rushwa na ya ukatili, zisingefahamika na hakuna hatua ambayo ingechukuliwa.”

“Sijali. Ukishafungua mlango huu wa kuwaonyesha wahalifu wa mfumo hadharani, itaishia wapi. Malaika njoo na ibilisi njoo, ukimya kolea.”

Waishiwa tukabaki tumepigwa butwaa wasiwasi. Mtu angeamua kutupiga kideo pale ungeweza kujua nani amepiga mswaki asubuhi ile na nani hakupiga. Hivyo mwishiwa mpambe akazidi kupamba moto katika kupamba.

“Tena wengine wa hii mitandao ya ushambenga wanazidi kuweka video vya ukatili. Wanathubutu hata kuonyesha jinsi wehu wanaoandamana walivyokamatwa kwa mateke na magumi wakati hawakuwa na silaha wala nini. Hii inazidi kujenga chuki dhidi ya vyombo vya dola. Ushambenga!”

“Lakini mwenzangu, hebu nikuulize. Katika sheria zetu, katika katiba yetu yenye viraka tele, ni wapi ambapo kupiga kiholela kumeruhusiwa? Ni wapi ambapo imetajwa kwamba ukatili ni silaha halali ya watu wa mfumo?

Mimi binafsi nafurahia vitu hivi vionyeshwe hadharani kwa sababu vinasaidia Serikali yetu pendwa kukomesha vitendo hivyo ambavyo vinadhalilisha Serikali.”

“Wewe unataka kuvunja amani tu. Kuonyesha vitendo hivi ni kuvunja imani na amani.”

“Hapana. Wanaofanya vitendo vya ukatili wanavunja amani na imani. Hakuna amani wala imani bila kukomesha ukatili huo. Ndiyo maana nataka Serikali ianze mpango maalumu wa kukomesha ukatili nchini mwetu, barabarani, vituoni, shuleni, nyumbani, kila mahali. Tanzania bila ukatili inawezekana …ili mradi tunadhamiria hivyo.”

“Tanzania bila ushambenga inawezekana.”

“Sawa bwana. Ukiamini hivyo, hatuwezi kuendelea kudai hii ni nchi ya amani. Wenye kulinda sheria, shuleni, barabarani, vituoni wakiamua kuchukulia sheria mkononi na kuipondolea mbali unategemea wengine wafanyeje?

Wanafuata mkumbo. Kwa hiyo tukitaka nchi ya amani, wenye kusimamia amani wawe wa kwanza kabisa kuonesha mfano bora, kama ambavyo wanakuwa wa kwanza kabisa kukomesha ufisadi. Hadi hali hii itokee, nitaendelea kufurahia watu jasiri wanaotumia mitandao kufichua wahalifu wanaoharibu jina na sifa ya vyombo vyetu muhimu na Serikali kwa ujumla.”

“Shauri yako bwana. Ngoja ukamatwe kwa uchochezi wako.”

“Ninavyojua mimi, wanaostahili kukamatwa kwanza waficha uhalifu popote ulipo. Enzi za wapigwe tu zimekwisha.”

Wakati wote huo, Mwishiwa Supu alikuwa amekaa kimya. Hatimaye aliamka na kusema.

“Malumbano yametosha. Hatuwezi kufunga mitandao ya ushambenga, lakini ole wake atakayenishambenga mimi. Atakosa supu miezi mitatu.”

Wacha waishiwa wakauke kucheka, hadi wengine wakapaliliwa.