Gonjwa ripoti za CAG linataka operesheni

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad

Muktasari:

  • Juzi, Profesa Assad aliwasilisha bungeni ripoti yake nyingine ya mwaka, ambayo kama ile iliyotangulia na nyingine za awali, mambo bado ni yale yale au pengine yamekuwa makubwa zaidi.

Mwaka jana, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad alipotoa ripoti yake ikionyesha udhaifu mkubwa katika matumizi ya fedha na mali za umma, tuliandika maoni hapa tukisema “Tunataka kuona mabadiliko katika ripoti za CAG”.

Juzi, Profesa Assad aliwasilisha bungeni ripoti yake nyingine ya mwaka, ambayo kama ile iliyotangulia na nyingine za awali, mambo bado ni yale yale au pengine yamekuwa makubwa zaidi.

Kinyume na matarajio yetu kwamba katika awamu hii ambayo Rais amejipambanua kwa kupambana na rushwa, ubadhirifu na kupiga ‘dili’ serikalini mambo yangebadilika, CAG Assad amesema mambo bado na kuwa kati ya mapendekezo 234 yaliyotolewa, 32 pekee (asilimia 14) ndiyo yametekelezwa kikamilifu.

Miongoni mwa kasoro zinazobainishwa katika ripoti hiyo ni kukua kwa Deni la Taifa kwa asilimia 20 na kufikia Sh41 trilioni, ambalo CAG ameonya iwapo hakutakuwa na udhibiti, litaathiri uwezo wa Serikali kwenye matumizi ya maendeleo kwa miaka ijayo.

Licha ya ukuaji wake, deni hilo halijajumuisha Sh3.2 trilioni ambazo ni madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii na madeni mengine ya Sh225.6 bilioni ambayo hayajalipwa na yana dhamana ya Serikali.

Vilevile, CAG amebainisha pia matumizi mabaya ya misamaha ya kodi, kuyeyuka mapato ya ushuru, ufisadi katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa na malipo ya Sh7.3 bilioni kwa wafanyakazi hewa.

Ripoti hiyo pia kati ya mengi inaonyesha ukata katika ofisi za ubalozi, kushuka kwa uwekezaji kwa mifuko ya hifadhi ya jamii, udhaifu katika usimamizi wa fedha za Serikali na Serikali kuwa mdaiwa mkubwa wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Vilevile, CAG amebainisha jambo ambalo wabunge wamekuwa wakilisema kuhusu uhalisia wa Bajeti ya Serikali na ameishauri Serikali kuwa na bajeti inayoakisi uhalisia kuliko ilivyo sasa, ili kupunguza nakisi ya bajeti na madeni.

Mathalani, Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 ilipanda hadi Sh29.5 trilioni kutoka Sh22.5 trilioni ya mwaka 2015/16 huku wabunge wakisema fedha zilizotolewa kwenye shughuli za maendeleo ni chini ya nusu ya zilizotengwa.

Kinachoshangaza katika ripoti hii ni hali kuendelea licha ya mapambano ya Rais John Magufuli dhidi ya uozo huo tangu aingie madarakani.

Nani asiyejua kuwa hadi sasa Rais amekuwa akitengua uteuzi au kusimamisha watumishi wa Serikali wanaobainika kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za umma, wazembe, wafanyakazi hewa na kuchukua hatua kupunguza Deni la Taifa?

Na haya yanatokea kipindi ambacho tunaelezwa kuwa bajeti ya ofisi ya CAG imepungua na hivyo kushindwa kuyafikia baadhi ya maeneo ya ukaguzi, pengine yangefikiwa tungeona makubwa zaidi.

Tunadhani hatua za ziada zitatakiwa kufanyika kwa operesheni maalumu ili kukomesha upungufu unaojitokeza katika kila uchao.

Miongoni mwa hatua hizo ni kuwekeza katika maadili ya mtu mmoja mmoja na maadili ya Taifa, kuhakikisha watumishi wanalipwa kiwango kinachostahili kulingana na gharama za maisha, huku Serikali ikifanya kila linalowezekana kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha upatikanaji wa hudumu muhimu kwa gharama nafuu.

Endapo hayo yatafanyiwa kazi tunaweza kuondokana na uozo huo kwa kudhibiti rushwa, ufisadi na kusimamia vizuri mikataba ya uwekezaji.