Haipingiki, Tanzania ina fursa nyingi za soka

Muktasari:

  • Hilo limeshindikana na halifanyiki kwa sababu fedha zote zinazopatikana katika soka nchini au zinazozunguka katika soka hazirudi katika kuhakikisha kunakuwa na maendeleo ya mchezo huo kutoka ngazi za chini.

Bado mafanikio ya soka la Tanzania hayaaminiki kwa sababu ya kukosekana kwa mfumo wa kuhamasisha watoto kucheza soka au kushiriki katika michezo kutoka ngazi za chini (grassroots).

Hilo limeshindikana na halifanyiki kwa sababu fedha zote zinazopatikana katika soka nchini au zinazozunguka katika soka hazirudi katika kuhakikisha kunakuwa na maendeleo ya mchezo huo kutoka ngazi za chini.

Ni kweli, kuna juhudi za hapa na pale za kuhakikisha kunakuwa na maendeleo katika soka la Tanzania, lakini juhudi hizo hazijaleta maendeleo ya soka nchini.

Kuna miradi mingi ya Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA) iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa barani Afrika huku Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zinazonufaika na miradi hiyo, lakini miradi hiyo nayo haijaleta maendeleo ya soka nchini.

Miradi hiyo ya FIFA ni ‘Win in Africa with Africa’ kwa ajili ya kutengeneza viwanja (sehemu ya kuchezea), ‘Goal’ wenye lengo la kusaidia miundombinu kama sehemu za kuchezea, vifaa, malazi na vituo vya ufundi, pia FIFA inatoa mafunzo mbalimbali kama kozi mbalimbali za makocha, waamuzi, utabibu na utawala lengo likiwa ni kuhakikisha mafunzo hayo yanasaidia maendeleo ya soka la Afrika huku Tanzania ikiwa moja ya nchi hizo.

FIFA imetoa mamilioni ya dola kwa miradi hiyo, lakini tujiulize, je, soka la Tanzania limeendelea kutokana na miradi hiyo ya FIFA?

Ni wazi miradi hiyo inatekelezwa kwa ajili ya watu fulani kujinufaisha kisiasa au kiuchumi hivyo kushindwa kuleta maendeleo ya kweli ya mchezo wa soka katika ngazi ya chini na taifa.

Watanzania tunatakiwa kuambiana ukweli, kwamba viongozi na watu wengine matajiri wenye nguvu nchini wamekuwa wakitumia soka kupata utajiri, nguvu za kibiashara au umaarufu wa kisiasa badala ya kuendeleza soka katika ngazi ya chini.

Ukiacha suala hilo la miradi, tatizo lingine linaloua soka la Tanzania ni kwamba Serikali imejiweka kando na maendeleo ya michezo (soka likiwamo), suala hili linaligharimu taifa hasa katika maendeleo ya miundombinu ya mchezo wa soka.

Pia, suala la rushwa serikalini na miongoni mwa wanajamii nalo linaua maendeleo ya mchezo wa soka kwani fedha ambazo zingepelekwa kwenye miradi mbalimbali ya maendelo kama kuendeleza soka katika ngazi ya chini, fedha hizo zinaingia katika mifuko ya baadhi ya viongozi wa Serikali na wanajamii.

Tatizo lingine kubwa ni kwamba viongozi wa shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nao wamekuwa wakijihusisha na rushwa, kutumia vibaya fedha zinazopatikana katika soka na kujinufaisha wenyewe badala kuendeleza mchezo wa soka nchini.

Kuna vikwazo vingi vinavyozuia maendeleo ya soka nchini, lakini pia upo mwanga wa maendeleo kama viongozi wa Serikali, shirikisho la soka na wafanyabiashara nchini wataacha ubinafsi wa kutumia fedha za soka na kupigania maslahi ya soka nchini.

Ikumbukwe kwamba, maendeleo ya kweli ya mchezo wa soka nchini hayatapatikana kwa kuwa na wachezaji wachache wanaocheza soka Ulaya, ila kwa umoja wa viongozi nchini katika kuhakikisha kunakuwa na miradi endelevu ya mchezo soka.

Ni wazi hapa nchini inahitajika miundombinu ya mchezo wa soka katika ngazi ya grassroots, unahitajika utawala bora wa mchezo wa soka, makocha wazuri, mafunzo mbalimbali, siasa safi nchini, Ligi Kuu imara na ligi za umri tofauti ili kuongeza ushindani na kuibua vipaji.

Kuwa na ligi imara itazaa timu ya taifa imara, ikiwa legelege, Stars itakuwa hivyo.