Haki, amani vitawale uchaguzi mdogo kesho

Muktasari:

  • Mbali na majimbo hayo, pia utafanyika uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata tisa za Isamilo wilaya ya Nyamagana, Manzase (Chamwino), Madanga (Pangani), Mitunduruni (Singida), Kanyelele (Misungwi), Buhangaza (Muleba) na Donyomurwak, Gararagua na Kashashi wilayani Siha.

        Kesho Jumamosi, wananchi katika majimbo mawili ya uchaguzi – Siha mkoani Kilimanjaro na Kinondoni jijini Dar es Salaam watafanya uchaguzi mdogo wa wabunge kuziba nafasi zilizo wazi.

Mbali na majimbo hayo, pia utafanyika uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata tisa za Isamilo wilaya ya Nyamagana, Manzase (Chamwino), Madanga (Pangani), Mitunduruni (Singida), Kanyelele (Misungwi), Buhangaza (Muleba) na Donyomurwak, Gararagua na Kashashi wilayani Siha.

Uchaguzi huo unatokana na majimbo na kata hizo kuwa wazi kwa sababu mbalimbali, kubwa ikiwa ni kujiuzulu kwa waliokuwa wabunge na madiwani na kuhamia katika vyama vingine.

Kutokana na uchaguzi huo, tayari vyama 12 vya siasa vilivyosimamisha wagombea vimefanya kampeni kwa zaidi ya wiki tatu, shughuli ambayo inakamilika leo.

Katika kipindi hicho, kwa wastani shughuli za kampeni zimefanyika kwa utulivu na amani, ingawa katika siku za mwisho yameripotiwa matukio ya machache likiwamo la kada mmoja wa Chadema kuuawa na mwingine kujeruhiwa, huku pia kukiwa na matukio ya polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa baadhi ya vyama.

Pia, yamekuwapo madai ya baadhi ya vyama kuwa mawakala wao wanawekewa vizingiti katika kupewa barua za utambulisho, mambo ambayo tunaamini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itayamaliza kabla ya shughuli hiyo kufanyika.

Pamoja na kuwa uchaguzi huu unachukua sehemu ndogo tu ya nchi yetu, tunaamini kuwa unatoa picha pana kitaifa, inayoeleza kiwango cha ukuaji wa demokrasia ya nchi yetu kwa miaka 26 ya mfumo wa vyama vingi tangu mwaka 1992.

Ni uchaguzi mdogo wa kwanza kufanyika baada ya ule wa majimbo matatu ya Longido, Singida Kaskazini na Songea Mjini wa Januari ambao baadhi ya vyama vya upinzani vilisusa kutokana na madai ya kuwapo kwa kasoro katika uchaguzi mdogo wa kata 43 wa Novemba mwaka jana.

Pia ni uchaguzi ambao unafanyika katika mazingira ya ushindani mkali huku baadhi ya wagombea wakiwa wale waliovihama vyama vyao na kupoteza nyadhifa zao na kisha kuteuliwa na vyama shindani walikohamia kuwania tena nafasi hizohizo.

Ni kutokana na mazingira hayo, tunaamini kuwa vyombo vinavyohusika na usimamizi wa uchaguzi na vile vya dola, hasa Jeshi la Polisi, vinavyoangalia suala la usalama na amani, vitahakikisha haki, amani na usalama vinaimarishwa kwa kiwango kinachostahili katika maeneo yote unakofanyika uchaguzi.

Hatutarajii kuona mazingira yaliyokuwa yanalalamikiwa katika uchaguzi mdogo wa Novemba au chaguzi nyingine zilizopita yakijirudia na kuendelea kuiweka demokrasia ya nchi yetu katika majaribu.

Miaka 26 ambayo nchi yetu imepita tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe, tukiwa tumepita katika uchaguzi mkuu ulioshirikisha vyama vingi vya siasa mara tano, inatosha kujifunza, kujirudi, kusahihisha makosa na kuboresha mifumo na jinsi tunavyoendesha chaguzi zetu ili kuweka mazingira ya haki na usawa.

Ni imani yetu kuwa kila mtu kuanzia NEC, wasimamizi wa uchaguzi na vyombo vya usalama, anatambua kuwa jukumu lake ni kukaa katikati kuhakikisha mchezo unachezwa kwa haki, wananchi wapiga kura, zinahesabiwa kwa usahihi na mshindi anatangazwa bila upendeleo wowote.

Tukumbuke jambo la msingi ni utendaji wa haki kwa kuwa amani ni tunda la haki na pale inapokosekana vurugu huibuka na kuhatarisha amani.

Tunasihi wananchi wa maeneo hayo kujitokeza kwa wingi kutimiza wajibu wao huo wa kidemokrasia wa kuchagua viongozi wawatakao.