Haki ya mtoto ilindwe, utaratibu ufuatwe

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile

Muktasari:

Pia, Dk Ndugulile alisema ni muhimu kufuata utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya kijamii ambayo kiutaratibu hufanyika kwa njia ya faragha na kwa kufuata mifumo sahihi.

Katika toleo la jana la gazeti hili kulikuwa na habari inayomnukuu Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile akikemea udhalilishwaji wa watoto kwa watu wenye malalamiko ya kutelekezwa na wazazi wenzao yanayowasilishwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Pia, Dk Ndugulile alisema ni muhimu kufuata utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya kijamii ambayo kiutaratibu hufanyika kwa njia ya faragha na kwa kufuata mifumo sahihi.

Dk Ndugulile hakuishia hapo. Pia alitoa rai kwa wananchi wote wenye malalamiko kufuata taasisi zinazohusika kwa ajili ya kutatua migogoro inayohusu wenza waliohitofautiana. Tunakubaliana na alichokikumbusha Dk Ndugulile kuhusu haki za mtoto kwamba kila mmoja wetu anapaswa kuzilinda, hivyo kinachofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuwaonyesha hadharani watoto waliofuatana na wazazi wao hakikubaliki kisheria.

Hata kitendo cha baadhi ya vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii cha kuchukua picha za watoto hao na kuwaonyesha hadharani, si cha kimaadili na hakikubaliki kisheria.

Pia, kitendo cha walalamikaji kuwatuhumu hadharani wanaowalalamikia ni ukiukwaji wa utaratibu wa namna ya kutatua matatizo katika jamii.

Tunaamini dhamira ya mkuu wa mkoa ni njema na amelenga kuwasaidia wanawake wenye matatizo katika jamii ambao ni wengi. Lakini kwa mtazamo wa wengi dhamira hiyo njema imeonekana kugeuka kama njia ya kukomoana na kuaibishana mbele ya jamii. Viashiria vya kukomoana na kuaibishana vinajionyesha kwa namna walalamikaji wanavyotoa tuhuma nzito hadharani dhidi ya wenza wao, lakini namna nkuu wa mkoa alivyotoka hadharani na kutaja idadi ya wabunge na viongozi wa dini akidai wamewatelekeza wanawake waliozaa nao, jambo hilo halikutakiwa kufanyika kwa kuwa bado ni tuhumu na zimeelekezwa kwa watu kutoka chombo taasisi zenye heshima kwa jamii.

Ingekuwa bora kama angetangaza idadi ya migogoro aliyofanikiwa kuitatua na iliyoshindikana na hatua gani zimechukuliwa zaidi.

Pia mkuu wa mkoa angeufanya mchakato huo kwa njia ya faragha na kuwazuia walioenda kupeleka tuhumu dhidi ya wenzao kuzungumza nje ya eneo lililokusudiwa ili kuepusha watu kuchafuliwa.

Pia, ushauri uliotolewa na Dk Ndugulile wa kuwataka wananchi wenye malalamiko kufuata taasisi zinazohusika, ungeenda sambamba na kuangalia upya utendaji wa taasisi hizo. Maelezo ya walalamikaji wengi yanaonyesha wamezifikia taasisi hizo, lakini hakuna msaada walioupata zaidi ya kusumbuliwa na pia kuwapo madai ya rushwa.

Umati wa walalamikaji uliojazana kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa tangu Jumatatu ni kielelezo kwamba tatizo ni kubwa na kuna haja taasisi husika kutathmini utendaji wao kama kweli una ufanisi.

Serikali kupitia Wizara ya Afya ina kitengo cha ustawi wa jamii ambacho kazi yake kubwa ni kushughulikia migogoro ya ndoa na haki za watoto, lakini kwenye vituo vya polisi kuna madawati ya jinsia.

Hatuwezi kuwahukumu ustawi wa jamii wala dawati la jinsia la polisi, lakini wanapaswa kujiangalia upya wajue wapi kuna kasoro ili wazirekebishe kwa lengo la kuboresha utendaji wao.

Tunaamini tatizo hili lipo maeneo yote nchini, hivyo rai yetu kwa wakuu wa mikoa mingine ni kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi wao kuhusu njia za kutatua matatizo ya matunzo ya watoto, ndoa na mengine kwa kutumia vyombo viloivyowekwa kisheria ili kuepuka athari zinazoweza kusababishwa na kuwekwa hadharani kwa matatizo yao.