Hakuna chuma ulete, wengi hutumia ovyo mtaji wa biashara

Godius  Rweyongeza

Muktasari:

  • Hii ni kutokana na ukweli kwamba biashara nyingi hufa ndani ya miaka mitano ya kwanza ambazo ni sawa na asilimia 80 hata zinazosalia nazo asilimia 80 huteketea ndani ya miaka mitano inayofuata.

Moja kati ya vitu vinavyopendwa na kila mtu ni kuanzisha biashara inayofanya vizuri na kudumu muda mrefu ikihudumia wateja wasiokwisha. Hata hivyo siyo kila biashara inaweza kufikia viwango hivyo.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba biashara nyingi hufa ndani ya miaka mitano ya kwanza ambazo ni sawa na asilimia 80 hata zinazosalia nazo asilimia 80 huteketea ndani ya miaka mitano inayofuata.

Kwa ufupi ni kwamba ndani ya miaka 10 baada ya biashara nyingi kuanzishwa, asilimia 99 huwa zimetoweka na nyingine hata waliozianzisha huwa hawakumbuki kama walikuwa na biashara.

Sasa, kama unahitaji biashara yako idumu kwa muda mrefu kuna vitu vinne unavyopaswa kuvizingatia wakati wote na ikiwezekana kuwahamasisha wote wanaokusaidia kuisimamia kuvipa kipaumbele.

Jambo la kwanza ni kuhakikisha biashara yako inajitegemea kimapato. Usitoe mapato yanayopatikana nje ya mzunguko. Inashauriwa urudishe walau asilimia 80 ya mapato hayo kwenye biashara.

Najua wengi huanzisha biashara wakiitegemea kwa matumizi ya kila siku hasa nyumbani kukidhi chakula, kinywaji, usafiri, karo ya watoto na mahitaji mengine lakini isiwe sababu. Ilinde biashara yako.

Endapo utaitegemea biashara yako kwa mahitaji hayo yote itaelemewa. Itashindwa kupumua, hivyo itaanguka. Na usipofanya juhudi za ziada itakufa kabisa. Ni lazima ife kwa sababu biashara yenyewe inakuwa bado haijajitegemea vya kutosha.

Ndiyo maana biashara nyingi hudumu kwenye viwango hivyohivyo kwa muda mrefu na hatimaye hudhoofu na hapa ndipo watu huanza kufikiria juu ya chuma ulete kwenye biashara. Ukweli ni kwamba chuma ulete ya biashara ni mmiliki mwenyewe.

Ukilijua hili na ukalifanyia kazi mambo yatabadilika. Anza kwa kurudisha asilimia 80 ya kipato kwenye biashara yako ili uikuze zaidi. Ukifanya hivi kwa zaidi ya miaka mitano utaongea lugha nyingine.

Mmoja wa wajasiriamali wakubwa Afrika ni Dk Strive Masiyiwa. Yeye alirudisha faida yote kwenye biashara kwa miaka kumi mfululizo. Hii ndiyo kusema kwamba kwa miaka kumi hakuwahi kuchukua hata senti moja kutoka kwenye biashara yake.

Unajua nini kilitokea. Biashara yake ilizidi kung’ara kila siku. Nawe unapaswa kufanya kitu kama hiki kuipaisha biashara yako.

Jambo jingine muhimu ni kutoa huduma inayodumu muda mrefu. Kwa kawaida biashara inaweza kuwa ya msimu au ya muda mfupi. Kuna msimu wa sikukuu mfano Nanenane, Krismasi, Pasaka au Idd ambazo biashara fulani hushamiri ilhali miradi kama ufyatuaji wa matofali au uchimbaji mchanga zikidumu mwaka mzima.

Vilevile kuna biashara za muda wa kati. Hizi ni zile ambazo hudumu kati ya siku chache na miaka isiyozidi mitano. Na mwisho kuna biashara za muda mrefu ambazo zinaenda muongo hadi muongo.

Sasa kabla hujaingia kwenye biashara unapaswa kujiuliza unachotaka kufanya ni biashara ya muda mfupi, kati au mrefu ili kujiandaa kukabiliana na changamoto zake.

Kama lengo lako ni kuanzisha biashara itakayodumu kwa muda mrefu, basi fikiria juu ya kuweka mazingira na miundombinu itakayodumu muda mrefu.

Bila kujali biashara yako ni ya muda gani unatakiwa kutanguliza masilahi ya wateja kwanza kabla ya yale ya yako.

Najua upo kwenye biashara ili upate faida. Hivyo, kama faida ndiyo lengo kuu basi itakuwa vigumu kuwahudumia wateja. Unahitaji kusukumwa na kitu zaidi ya faida kuingia katika biashara. Sukumwa na kutoa huduma kwa wateja kuliko unavyotarajia kupata faida.

Kuwa bega kwa bega na mteja wako tangu anapochukua bidhaa hata anapoitumia. Fahamu kama bidhaa ile ilimsaidia au la. Kama haikumsaidia ni kitu gani kilisababisha ili uondokane nacho siku nyingine kisije kikakukosesha wateja ambao ni muhimu kwa biashara yako.

Bila shaka umeshawahi kuona kampuni zinazota warantii na kukupa fursa ya kubadilisha au kutengeneza pindi bidhaa uliyonunua inaposumbua. Hii ni kutokana na ukweli kwamba watu hawa wanatanguliza masilahi ya mteja mbele kuliko faida wanayotakiwa kuipata.

Pamoja na mambo hayo matatu muhimu, unatakiwa kujitofautisha. Unaweza kukuta una duka la bidhaa fulani na jirani yako kuna duka la bidhaa za namna ileile. Kwa mazingira haya lazima uwape wateja sababu ya kununua dukani kwako, jambo linalowezekana endapo utajitofautisha.

Tuwasiliane kwa 0755848391